Jamii imeaswa kutambua kuwa jukumu la kuwalinda watu
wenye ualbino na kuhakikisha usalama wao si la serikali pekee na wafadhili bali
ni jukumu la kila mmoja zaidi katika familia zao.
Rai hiyo imetolewa na Katibu Tawala wa Halmashauri ya
Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza Elius Nyakia
kwa niaba ya mkuu wa wilaya hiyo, wakati akifungua Warisha ya
kutathimini mafanikio na changamoto za kampeini ya kutokomeza mauaji na ukatili
dhidi ya watu wenye ualbino, iliyokuwa ikitekelezwa na vyombo vya habari vya kijamii Tanzania chini
ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Sayansi Elimu na Utamaduni(UNESCO) iliyofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Maendeleo Mitindo Wilaya ya
Misungwi Mkoani Mwanza.
Amesema kuwa Serikali inakabiliwa na changamoto kubwa kutoka
kwa jamii juu ya ulinzi na usalama wa watu wenye Ualbino na kuomba wadau na
vyombo vya habari kuongeza nguvu katika kuelimisha Jamii.
Hata hivyo Nyakia
ameiomba jamii kuepuka Imani potofu na kuacha tabia ya kuibua mitazamo hasi juu
ya watu wenye ualbino na kutambua kuwa vitendo hivyo vinahatarisha usalama wa
maisha yao.
Aidha amesema kuwa wazazi na jamii itambue kuwa
kuwahifadhi watu wenye ualbino ni hatua ambayo inawasababisha kujiona
wametengwa na wenzao pamoja na familia zao kwamba wamenyanyapaliwa.
Amebainisha kuwa uelewa mdogo juu ya masuala ya watu
wenye Ualbino pia ni changamoto hata kwa viongozi ngazi mbalimbali za serikali
na kusisitiza juhudi za makusudi kuchukuliwa katika kutoa Elimu.
Ametoa wito kwa wazazi wanaowapeleka watoto wao wenye
ualbino katika vituo mbalimbali kujenga tabia ya kuwatembelea na kuwapatia
mahitaji muhimu na kuondoa dhana ya kwamba jukumu hilo ni la Serikali.
Post a Comment