Maafisa watendaji wa kata
wilayani Karagwe mkoani Kagera
wametakiwa kuhamasisha wananchi kuhakikisha wanachangia michango ya mbio za
mwenge na utaratibu wa kuchangisha michango hiyo tayari umeshaanza wilayani
humu.
Wito huo umetolewa leo na
mkuu wa wilaya ya Karagwe Deodatus Kinawiro katika kikao cha maandalizi ya mbio
za mwenge kilichofanyika katika ukumbi
wa halmashauri ya wilaya ya Karagwe.
Kinawiro amesema kuwa ni
jukumu la maafisa watendaji wote wa kata kuhakikisha wanahamasisha wananchi
kuchangia michango ya mbio za mwenge
kama ilivyopangwa na kupitishwa na wajumbe wa mbio za mwenge mwaka huu
2016 ambapo kila mwananchi,taasisi, na mashirika binafisi watatakiwa kuchangia kama watakavyoelekezwa
ili kuhakikisha mapokezi ya mbio za mwenge mwaka huu yanafanikiwa.
Amesema kuwa mwaka huu
mwenge wa uhuru utakesha katika mji
mdogo wa Nyakaiga katika kata ya Kibondo wilayani humu huku akieleza kuwa wameamua
kufanya hivyo ili wananchi wengine nao waweze
kuona mwenge wa uhuru na sio kukaa wanausikia katika sehemu moja tu.
Hata hivyo amewataka madiwani
nao kwa nafasi yao kutochanganya siasa na mwenge kwani mwenge wa uhuru ni kwa
ajili ya maendeleo na ni kwa watanzania wote.
Akieleza katika kiko hicho
cha maandalizi ya mbio za mwenge mratibu wa mbio hizo wilaya ya Karagwe Aloyce Mjungu
ameeleza kuwa mwaka huu mwenge wa uhuru kwa wilaya ya Karagwe utapokelewa tarehe 25 mwezi wa 07 mwaka huu katika kijiji
cha Msabanga wilayani Ngara na ukiingia wilayani humu utatembelea miradi
mbalimbali ya maendeleo inayopatikana katika wilaya hii na kuukabidhiwa kwa
watu wa wilaya ya Kyerwa tarehe 26 mwezi
07 mwaka huu katika kijiji cha Ilega wilayani Kyerwa.
Mjungu ameshukuru wananchi,na wadau wote
waliofanikisha mbio za mwenge mwaka jana ambapo amesema kuwa wilaya ya Karagwe
ilikuwa ya 6 kati ya wilaya 8 za mkoa huu wa Kagera, na nafasi ya 31 kwa
ngazi ya kanda kati ya 35,Pia wilaya ya Karagwe ilikuwa ya 78 kitaifa ambapo amesema hatua hiyo ni nzuri na wanatamani mwaka huu
wavuke katika hatua hiyo kama ushirikiano wa wananchi utakuwepo.
Post a Comment