Waziri Mkuu wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa awasili Mkoani Kagera kwa ziara ya
siku tatu kuanzia Machi 13 hadi 15, 2016
katika Manispaa ya Bukoba, Wilaya za Missenyi, Karagwe na Ngara.
Akitaja malengo ya ziara
yake mara baada ya kuwasili Mkoani Kagera alisema lengo kuu la ziara yake ni
kwenda katika ranchi za Missenyi na
Kitengule Wilayani Karagwe ili kujionea zinafanyaje kazi na kuona jinsi ya kutatua changamoto mbalimbali ili kuwepo
ufugaji bora na kuondoa migogoro ya wafugaji na wakulima.
Lengo la pili la ziara ya
Mhe. Majaliwa alisema ni kutembelea
Gereza la Mwisa Wilayani Karagwe na Ngara ili kujionea maendeleo ya
wakimbizi wafungwa wanajeshi walioletwa na Serikali katika Magereza hayo ili
kuwafunza wawe raia wema mara baada ya
kubainika katika kambi ya wakimbizi iliyopo mkoani Kigoma wakiendesha mafunzo
ya kijeshi kwa wenzao kambini.
Mara baada ya kusomewa
taarifa ya Mkoa wa Kagera na Mkuu wa Mkoa John Mongella Waziri Mkuu Mhe. Kassim
Majaliwa alitoa rai kwa wananchi na viongozi wa Mkoa kuhakikisha wanaulinda Mkoa
ili usiingiliwe na wahamiaji haramu kutoka nchi jirani ikiwa ni pamoja na ardhi
kutouzwa kiholela kwa wageni kutoka nje.
Aidha, Waziri Mkuu Mhe,
Majaliwa aliwaonya Wakuu wa Wilaya za Missenyi, Kyerwa na Ngara kuhakikisha
wanaziba mianya ya udhaifu ilipo kwa kuingiza mifugo na uuzwaji wa ardhi holela
katika Wilaya hizo huku wao wakiwepo kama vingozi wa Serikali, alisema
wanatakiwa kuchukua hatua haraka sana kuziba mapungufu hayo.
Pia alitoa agizo kwa Afisa
Uhamiaji wa Mkoa na Maafisa Uhamiaji wa Wilaya kuhakikisha watekeleza majukumu
yao ipasavyo na kuacha mara moja tabia ya kutoa vibali hovyo vya watu kutoka
nchi jiarani na kuhamia katika Mkoa wa Kagera na kuingiza mifugo pamoja na
kuhozi ardhi ya wazawa.
Vilevile Waziri Mkuu Mhe.
Kassim Majaliwa alisistiza juu ya ukusanyaji wa kodi ili Serikali iweze
kuwaletea wananchi maendeleo yao. Alihoji juu ya utoroshwaji wa Madini ya bati
Wilayani Kyerwa wakati viongozi wakiwepo bila kuchukua hatua. Waziri Mkuu Mhe.
Majaliwa alisema hali hiyo inatakiwa kukoma mara moja kutorosha madini hayo
kwenda nchi jirani bila serikali kupata mapato yake.
Uzinduzin wa Miradi
Katika
hatua nyingine Waziri Mkuu Mhe. Majaliwa alitembelea na kuzindua mradi wa maji
Bunena ambao ujengwa katika Maispaa ya
Bukoba kwa ufadhili wa Serikali ya Ufaransa na umekamilika kwa asilimia 98% na gharama
ya mradi huo ni zaidi ya shilingi bilioni 31na unatarajiwa kukabidhiwa mwezi
Aprili 2016 mara baada ya kuwa umekamilika kwa asilimia mia moja.
Pia Waziri Mkuu Mhe. Kassim
Majaliwa alizindua kiwanda cha Maji cha Bunena Spring Water ambacho kinazalisha
maji ya kunywa na kimejengwa na Kanisa Katoliki likishirikiana na wawekezaji
wawili wazawa. Kiwanda hicho kina uwezo wa kuzalisha maji safi na salaama ya
kunywa chupa za Mililita 600 milioni tatu kwa siku.
Mkutano na Watumishi wa
Serikali
Waziri
Mkuu Mhe. Majaliwa pia aliongea na
watumishi wa Serikali Mkoani Kagera kwa kuwa kumbusha maadili ya kazi zao kwa
kusema kuwa wajibu wa mtumishi wa Serikali ni kumpokea mwananchi, kumsikiliza,
na kumhudumia au kumwelekeza mahali pa kupata huduma stahili bila kinyongo au
kukasirika.
“Najua kuwa watumishi wa
kada mbalimbali mnaidai Serikali stahiki zenu, Serikali ya awamu ya tano
imejipanga kuhakikisha inalipa madeni ya watumishi na kwasababu hiyo nawaombeni
watumishi msitumie kigezo hicho cha
kuidai serikali kufanya fujo au kukataa kuwahudumia wananchi. Alisistiza Waziri
Mkuu Mhe. Majaliwa
Mkutano wa Hadhara
Akiongea
na wananchi wa Manispaa ya Bukoba katika uwanja wa Uhuru pamoja na kero
mbalimbali walizoziwasilisha kwake ikiwa mojawapo ni kero ya wananchi
waliopimiwa viwanja 800 na hawakugawiwa viwanja hivyo, Mhe. Majaliwa alitoa
muda wa mwezi mmoja kwa Mkurugenzi na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Bukoba kuwa
wawe wametafuta utatuzi wa mgogoro huo
pia aliagiza Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa
fedha za serikali kuja kufanya ukaguzi kuhusu viwanja hivyo.
Post a Comment