SALAMU
KUTOKA SHIRIKA LA UNDER THE SAME SUN
SIKU
YA KIMATAIFA YA KUONGEZA UELEWA KUHUSU UALBINO
JUNE
13, 2016, VIWANJA VYA MNAZI MMOJA
Mheshimiwa
Mgeni Rasmi Naibu Waziri, Dkt. Abdallah Possi;
Mheshimiwa
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam
Mwenyekiti
wa Taifa wa Chama cha Watu wenye Ualbino;
Waheshimiwa
wanabalozi, viongozi wa serikali, asasi zisizo za kiserikali;
Wageni
waalikwa, Wawakilishi wa Vyombo vya Habari
Ndugu
zangu wenye ualbino;
Itifaki
imezingatiwa…
Asalaamu
Aleikhum! Amani iwe nanyi!
Shirika la Under The Same Sun, (UTSS) linayo
furaha kubwa na limefarijika sana kuwaona viongozi wa wetu katika maadhimisho
haya ya Siku ya Kimataifa ya Kuongeza Uelewa Kuhusu Ualbino.
Kwa niaba ya UTSS nachukua fursa hii kumpongeza na
kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa juhudi zake zote za kuiongoza nchi hii kwa
upendo, haki na uadilifu.
Mwaka
mmoja tu baada ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Kupitisha Azimio la kutenga Siku
ya Kimataifa ya Kuongeza Uelewa Kuhusu Ualbino, Mheshimiwa Rais alimteua Naibu
Waziri Mheshimiwa Dkt. Abdallah Possi kusimamia Masuala ya Watu wenye Ulemavu
katika Ofisi ya Waziri Mkuu. Hatua hii
imeweka historia kubwa katika nchi yetu.
Tunamshukuru Rais wetu. Ndoto ya
kuwaondoa watu wenye ulemavu kwenye Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii sasa
imekamilika. Huu ni mfano mzuri wa kuigwa na mataifa mengine kwa kuwa Tanzania imekuwa nchi ya kwanza Afrika Mashariki kutekeleza kwa vitendo ushauri wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon pale aliposema na ninakuu, "Ajenda ya 2030 ya Maendeleo Endelevu inaahidi kutomuacha mtu yeyote nyuma. Hii ni pamoja na watu wenye ualbino. Vitendo vya ukatili, ubaguzi na umaskini lazima vitokomezwe.”
Tuna imani kuwa serikali kwa kushirikiana na wadau
mbali mbali ndani na nje ya nchi inaweza kutatua changamoto zifuatazo ambazo
zinadumaza maendeleo ya watu wenye ualbino nchini.
Ulinzi
na Usalama:
Mheshimiwa Mgeni Rasmi, tunaiomba serikali yako iongeze juhudi katika
ulinzi na usalama wa watu wenye ualbino.
Baadhi yao wamekuwa wakikikimbilia kwenye vituo ambavyo vimegeuka kuwa
makambi yao. Japokuwa serikali
ilianzisha vituo hivyo kwa nia njema ya kuwalinda watu wenye ualbino, hali
kwenye makambi haya hairidhishi. Wazazi
washinikizwe kuwatembelea watoto wao kwenye vituo hivyo. Tunaunga mkono juhudi za Mheshimiwa Naibu
Waziri za kuzivunja kambi hizi na kuwapeleka wanafunzi katika shule zenye mfumo
wa elimu jumuishi. Juhudi zifanyike
kuwahamishia watu wenye ualbino kwenye maeneo salama kutoka katika maeneo
hatarishi. Sanjari na hayo kwa sasa
pawepo na Afisa Ustawi wa Jamii na daktari katika kila kituo ili kuwanasihi
walioathirika kisaikolojia na pia kuwaangalia afya zao.
Hivi juzi tu nilikuwa Tabora na Kagera ambako
matukio mawili tofauti yametokea katika mikoa miwili katika siku moja ya May
23, 2016.
Katika kijiji cha Kalitu, Wilaya ya Nzega watoto
Tausi na Kulwa walinusurika kutekwa nyara na kuuawa baada ya wahalifu kuvamia
nyumba yao kwa nia ya kuwadhuru, usiku wa Mei 23, 2016. Mmoja alikuwa hayupo nyumbani usiku huo na
mwingine alijificha na kujinusuru.
Katika Kitongoji cha Chankonko, Kijiji cha
Nyashimwe, Wilaya ya Kyerwa, mkoa wa Karagwe, kaburi la mtoto wa miezi mitatu,
Magufuli Begumisa, lilifukuliwa usiku wa Mei 23, 2016 na miwli wake kuchukuliwa
wote.
Japokuwa taarifa hizi hazijatangazwa, ukatili
dhidi ya watu wenye ualbino bado unaendelea.
Watoto wangu na wajukuu zangu, msirubuniwe na vitu
kama vile pipi na miwa na kuangukia kwa watu waovu. Kama mtu usiyemjua anakupa vitu kama hivyo
kwa madhumuni ya kuondoka naye, piga kelele na waite watu wazima wakusaidie.
Kuongeza
Uelewa kwa Umma kuhusu Ualbino: Kuwepo na mpango wa kitaifa wa Kuielimisha
Jamii kuhusu Ualbino kupitia vyombo vya habari, vipeperushi, filamu na warsha
kama inavyofanywa kuhusu Malaria, Kifua Kikuu, Afya ya Mama na Mwana, VVU na
UKIMWI na kadhalika na pia kwa kujumuisha Ualbino kama somo- kwenye mitalaa ya
shule na vyuo. Elimu hii pia itolewe kwa
vyombo vya ulinzi na usalama, polisi, mahakama wizara zote za serikali na
bungeni.
Elimu: Kuwajengea mazingira rafiki yatakayowawezesha
watu wenye ualbino kupata elimu bora katika ngazi zote. Kuchapisha na kusambaza nakala nyingi zaidi
za Mwongozo wa Walimu, Walezi na Wazazi wa Watoto wenye Ualbino. Kununua visaidizi vya uoni hafifu na vitabu
vya kiada vyenye maandishi makubwa kwa kila mwanafunzi katika ngazi zote za
elimu.
Afya: Serikali itenge vyumba maalumu vya watu wenye
ualbino kwenye hospitali zote za wilaya ili kuhakikisha kwamba wanahudumiwa kwa
wakati na kwa haraka ili kuokoa maisha yao:
Hii ni pamoja na uchunguzi wa dalili za awali za saratani ya ngozi, matibabu ya papo hapo kwa kutumia Liquid Nitrogen. Matibabu haya yote yatolewe bila malipo. Serikali inunue mitungi ya kuhifadhia Liquid
Nitrogen na pia vifaa vya kutibia kama vile Cryoguns na mafuta kinga. Vifaa hivi na mafuta kinga visitozwe ushuru. Serikali iongeze uwezo kwa RDTC wa
kutengeneza mafuta kinga mengi zaidi ya KiliSun ili kila Mtanzania mwenye
ualbino ayapate.
Kesi: Tunapongeza juhudi za serikali kupitia vyombo
vya kisheria kwa kuwakamata, kuwashitaki na kuwahukumu baadhi ya wahalifu
waliofanya vitendo vya ukatili dhidi ya watu wenye ualbino nchini. Tunaiomba serikali iongoze juhudi hizi na iharakishe
kesi za ukatili huu dhidi ya ndugu zetu ili haki itendeke kwa wote.
Mheshimiwa mgeni Rasmi, naomba niwakilishe salamu za
Mariamu Staford aliyekatwa mikono kule Ngara Oktoba 17, 2008. Ameniomba
nifikishe kwako ujumbe ufuatao, na ninanukuu, “Wakati Mheshimiwa Rais
unapoendelea na kasi ya kutumbua majipu ya watumishi hewa, wanafunzi hewa na
viongozi wasio waadilifu, tunaomba sasa utumbue na majipu ya wahalifu
wanaotuteka nyara, wanaotukata viungo na wanaotuua ili viungo vyetu vitumiwe
kuwaletea mafanikio mbali mbali na wale wanaonunua na kutumia viungo vyetu, na
pia wale wanaoficha au wanaopoteza ushahidi kwa kurubuniwa na rushwa.” mwisho
wa kunukuu.
Viungo
Bandia vinavyofanya kazi:
Serikali ihakikishe kuwa watu wenye ualbino waliokatwa viungo wanapatiwa
viungo bandia vinavyofanya kazi ili wasiwe tegemezi na pia kuwajengea uwezo wa
ama kuendelea na masomo au kuanzisha miradi ya kuwawezesha kujikimu
kimaisha. Kwa sasa hivi wanapatiwa
viungo hivyo nje ya nchi kwa msaada wa mashirika ya nje.
Sheria
na Sera ya Ualbino:
Kwa sababu kundi hili limekuwa likiwindwa kwa ajili ya viungo vyao hadi
kuwekewa kambi maalum za kuwalinda, tunakuomba serikali itunge sera na sheria
ya Ualbino ili kulinda uhai wao na masilahi yao. Tunaamini kuwa hivi vitasaidia kurahisisha
kazi za polisi, mawakili, waendesha mashtaka na mahakama katika kuhakikisha
kwamba haki inatendeka
kwa waliofikwa na madhila ya ukatili dhidi ya binadamu. Na vile vile itahakikisha kwamba walioathiriwa
na ukatili huo na familia zao na za wale waliouawa wanapata ushauri wa
kisaikolojia na wanalipwa fidia. Sheria
na Sera ya Watu wenye Ulemavu haviwajumuishi watu wenye ualbino.
Wachochezi
wa Mauaji:
Imefahamika wazi kuwa wachochezi wa mauaji haya na ukataji viungo vya
watu wenye ualbino ni waganga wa kienyeji.
Tunaamini kwamba serikali yako itaendelea kuwakamata na kuwachukulia
hatua waganga hawa na wapiga ramli, na kufunga
kabisa shughuli zao. Na hapa
hatuzungumzii wataalamu wa Tiba Asili na Tiba Mbadala watakaohakikiwa na
serikali.
Marekebisho
ya Sheria: Tunaiomba serikali irekebishe Sheria ya Uchawi ya
Desemba 28, mwaka 1928 na ile Sheria ya Tiba Asili na Tiba Mbadala ya Mwaka
2002. Sheria zote mbili zina mianya
inayotumiwa na waganga wa kienyeji ili kuhalalisha utumiaji wa viungo vya
binadamu chini ya kisingizio kuwa kisayansi / kibailojia binadamu ni jamii ya
wanyama.
Ushirikiano
na Mataifa Mengine:
Tunaiomba serikali yako iwe mstari wa mbele katika kukomesha kabisa
ukatili huu na kuwakutanisha viongozi wa Afrika Mashariki, Kusini mwa Afrika na
bara zima la Afrika katika kulijadili suala hili na kutafuta ufumbuzi wa pamoja
kwa lengo la kukomesha ukatili huu dhidi ya watu wenye ualbino.
Uovu huu umekuwa ukifanywa katika nchi za Afrika
kwa miaka mingi sana. Kila wiki sasa
tunapokea taarifa za mauaji, ufukuaji wa makaburi, ukataji viungo na utekaji
nyara kutoka kwa jirani zetu Malawi na Msumbiji. Taarifa za kipolisi nchini humo zinazungumzia
kuhusu biashara ya viungo vya watu wenye ualbino kuvuka mipaka.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi, Katika kila Watanzania 19
kuna Mmoja mwenye vinasaba vyenye ualbino! Naomba kumalizia kwa kutoa rai kwa ndugu zangu
Watanzania wenzangu kuwa na moyo wa kuwapenda, kuwathamini, kuwajali na
kuwalinda ndugu zetu wenye ualbino. Tutoe
taarifa za uhalifu mapema na tuzuie kwa haraka uwezekano wa kutokea kwa ukatili
huo! Sisi wote ni binadamu tuna haki ya kuishi nchini mwetu kwa
amani! Na hivyo basi tunapaswa kupigania haki za ndugu zetu.
Narejelea
kauli ya Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli ya Oktoba 2015 siku chache kabla
ya Uchaguzi Mkuu na ninanukuu:
“Tutalinda
masilahi ya watu wenye ulemavu wakiwemo watu wenye ualbino ili wasiuawe katika
nchi hii,” mwisho wa kunukuu.
Na sisi tuna
ndoto kwamba siku moja watu wenye ualbino nchini Tanzania na barani Afrika watachukua
nafasi yao stahiki katika kila ngazi ya jamii na kwamba siku za ubaguzi dhidi
ya watu wenye ualbino zitakuwa kumbukumbu iliyofifia!”
Haya yanawezekana
ikiwa kila mmoja wetu atatimiza wajibu wake!
Ahsante kwa
kunisikiliza.
Imeandikwa na kusoma na Vicky Ntetema,
Mkurugenzi Mtendaji wa Under The Same Sun – Tanzania kwa niaba ya shirika hilo.June 13, 2016
Post a Comment