Maonesho ya Wakulima ya
Nanenane ya mwaka huu 2016 Mkoani Kagera tayari yamezinduliwa rasmi na Mkuu
wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Mstaafu Salum Mustaph Kijuu katika uwanja wa kilimo wa Kyakairabwa
uliopo nje kidogo ya Manispaa ya Bukoba.
Akifungua Maenesho hayo Kijuu Agosti 3, 2016 alitembelea mabanda na
bustani mbalimbali za vibanda vilivyoandaliwa na wadau mbalimbali wa kilimo,
mifugo na uvuvi ambao ni kutoka katika Mkoa mzima wa Kagera zikiwemo
Halmashauri za Wilaya zote za Kagera.
Aidha Kijuu mara baada ya kutembelea shughuli za
wadau wa kilimo, Mifugo na Uvuvi aliongea na wananchi walihudhuria katika
maonesho hayo na kutoa wito kwa wananchi ambao hawajafika katika viwanja hivyo kufika
ili kujifunza shughuli mbalimbali za kilimo cha kisasa katika kujikomboa na
umasikini kwa kutumia eneo dogo na kulima kwa tija.
Kaulimbiu ya maonesho ya
Nane Nane kitaifa mwaka huu 2016 ni “Kilimo, Mifugo na Uvuvi ni Nguzo ya Maendeleo,
Vijana shiriki kikamilifu Hapa kazi tu.” Akisistizia Kauli mbiiu
hiyo Kijuu amewakumbusha vijana
kushiriki katika shughuli za kilimo, ufugaji wa kisasa na ufugaji wa samaki ili
kujiajili na kuacha kulalamika kuwa hakuna ajira.
Katika hatua nyingine Mkuu
wa Mkoa ametoa agizo kwa Wakuu wa
Wilaya wote wa Mkoa wa Kagera kuhakikisha wadhibiti vitendo vya uchomaji moto
ambapo vitendo hivyo vimekithiri mkoani hapa kwa kuchoma mashamba ya misitu ya
hifadhi, misitu ya kupandwa na mashamba ya wananchi hasa kwa kipindi cha miezi
miwili ya Juni na Julai 2016.
Wakuu wa Wilaya waliagizwa
pia kuhakikisha wanawasimamia viongozi katika ngazi zote na kuwabaini wananchi
wanaojihusisha na vitendo vya uchomaji moto na kuwachukulia hatua kali za
kisheria aidha, Kwa viongozi ambao hawatawajibika watachukuliwa hatua kali za
kisheria wao wenyewe.
Agizo
la pili la Mkuu wa Mkoa wa Kagera lilikuwa ni kuhusu Wanansiasa
kufanya mikutano katika maeneo yao na si viongozi wa kisiasa kutoka katika
maeneo mengine kwenda sehemu zisizo kuwa zao na kufanya mikutano ya kisiasa na
kuwasumbua wananchi katika shughuli zao za maendeleo ambapo Kijuu amesema hatakuwa tayari kuwavumilia
viongozi wa namna hiyo katika mkoa wake.
Pamoja na kufungua rasmi
maonesho ya Nane Nane Mkoani Kagera pia Mkuu huyo wa Mkoa amezindua wiki ya
Unyonyeshaji Kitaifa ambayo inaadhimishwa Mkoani Kagera ambapo maonesho yake,
Elimu na ushauri vinatolewa katika uwanja huo wa Kyakailabwa na kilele chake
kitakuwa ni Julai 7, 2016.
Post a Comment