Kunako majaliwa ninakusudia kuandika historia ya mageuzi
ya siasa za vyama vingi hapa nchini. Inasikitisha, pengine kwa kuwa mwitikio wa
wasomi kupigania mageuzi ya siasa za vyama vingi ulikuwa mdogo, historia ya
vyama vingi hapa nchini haijaandikwa vya kutosha na bila kupotoshwa.
Kwa sasa tunaweza kusoma vipande kadhaa vya taarifa
kuhusu harakati za siasa za mageuzi nchini ila si historia kamili na sahihi
ikianinsha na kubainisha kumbu kumbu sahihi za muda wa na matukio makuu, sababu
za matukio hayo, wahusika wakuu, michakato na minyukano, kupanda na kushuka kwa
mashujaa wa kweli na wanyemeleaji wa historia ya mageuzi ya kisiasa nchini
kuanzia 1989 hadi 2015.
Kwa kuanzia, nimeanza kwa kuweka kwa usahihi kumbukumbu
kadhaa.
1.
KONGAMANO LA KITAIFA LA MAGEUZI JUNI 1991
Juni 11-12/1991 kulifanyika Kongamano la kitaifa la
mageuzi katika ukumbi wa Diamond Jubilee Dar es salaam. Wahusika wakuu wa
kongamano hilo walikuwa [vijana wakati huo] Mabere Marando, Ringo Tenga,
Ndimara Tegambwage, Prince Bagenda, Mashaka Nindi Kimoto (apumzike kwa
amani) na Mch. Christopher Mtikila
(rip). Wazee [hawa wote ni marehemu kwa sasa na wapumzike kwa amani] walikuwa
akina Chief Abdallah Said Fundikira, Kasanga Tumbo na Kasela Bantu.
Hao walitafutwa
mahsusi na kupewa nafasi za kuoneka mbele ili kufuta hisia madai ya demokrasia
ya vyama vingi nchini yalikuwa ni matakwa ya vijana. Kwa Zanzibar walialikwa
washiriki 11, wafuasi na wawakilishi wa Maalim Seif Sharif Hamad, aliyekuwa
kizuizini wakati huo, wakiongozwa Mzee Shaaban Mloo (apumzike kwa amani) na
aliambatana na Awesu Dadi na wenzake.
Aidha kulikuwa na Watanzania walikokuwa wanajulikana kwa
misimamo yao ya kimageuzi tangu miaka ya 1960 ambao nao walialikwa pia, lakini
pia wakimwakilisha Oscar S Kambona. hao ni Mzee Dastan Lifa Chipaka, Mzee
Efraem Mwakitwange (apumzike kwa amani) - alikuwa mmiliki wa beach resort hotel
ikijulikana kwa jina la Rungwe Oceanic), Mzee Kichoweko, Bwn. James Mapalala na
wengineo. Chuo Kikuu walialikwa akina Prof. Mwesiga Baregu na wanafunzi akina
James Mbatia, Anthony ABC Komu, Idrissa Al Nuru (amekwisha tangulia mbele ya
haki, apumzike kwa amani) na wanafunzi wengineo.
2.
MAAZIMIO YA KONGAMANO LA KITAIFA
Mwishoni mwa kongamano kulitolewa maazimio kumi, mojawapo
likiwa ni Tanzania kuanzisha mfumo wa vyama vingi vya Siasa. Kisha iliundwa
Kamati ya Mabadiliko ya Katiba, kwa Kiingereza, ikijulikana kwa jina la
National Comiittee for Constitutional Reform (NCCR) ikiongozwa na Chief
Abdallah Said Fundikira, na Katibu wake Mkuu akiwa Mabere Marando.
Kamati hiyo kwa upande wa Zanzibar iliitwa Kamati ya
Uhuru wa Kisiasa (KAMAHURU) ikiongozwa na Mzee Shaaban Mloo lakini aliyekuwa
defacto leader ni Maalim Seif Sharif Hamad.
Maazimio ya Kongamano hili yaliandikwa na kusambazwa
katika kjitabu kilichojulikana kwa title ya TUNACHOTAKA SASA.
Katika Kongamano hilo la kitaifa hakuna kumbukumbu
zinazoonesha Mzee Mtei, Freeman Mbowe na waasisi wengine wa Chadema kuhudhuria
au pengine kufika tu hapo Diamond Jubilee. Kunako
3. KAMATI YA MAGEUZI NA UJIO WA CHAMA CHA NCCR -MAGEUZI
NA VYAMA VINGINE
Februari 15/1992 NCCR [Kamati] ilijibadilisha jina na
malengo na kisha kuwa Chama Cha Siasa kwa jina la National Convention for
Construction and Reform (NCCR)- Mageuzi. Kwa hiyo NCCR [Kamati] ceased to exist
right from 15/02/1992. Lengo lilikuwa ku-maintain jina (NCCR) na historia ya
harakati za mabadiliko ya kisiasa nchini (Mageuzi). Wakati huo, kwa sababu
mbali mbali, wakongwe akina Mzee Fundikira, Mzee Kasanga Tumbo, na mzee Kasela
Bantu walishaamua kuondoka na kuanzisha chama chao cha UMD kikiongozwa na Chief
Fundikira, James Mapalala akishirikana na Alec Chempnda (huyu sijui iwapo bado
anaishi) walianzisha Chama Cha Wananchi
(CCW), baadaye kiliungana na KAMAHURU na kujiita jina la CUF.
Mch. Christopher
Mtikila akishirikiana na Kaoneka, Mwinnjilist Kamara Kusupa Mwingandoshi
(apumzike kwa amani) na mtu mmoja aliitwaKabati walianzisha chama chao kikiitwa
Chama Cha Demokrasia (CCD) na kisha baada ya kugombana na Mtikila CCD ilibaki
na Mwenyekiti wake Kabati, Mch. Mtikila (mjanja) alibadirisha CCD kutoka jina la Kiswahili kuwa jina la
Kiingereza (Democratic Party /DP).
Kaoneka baadaye aliajiriwa Chadema kwa nafasi ya
usimamizi wa ofisi (office supervisor), Kisutu, dar es Salaam, na Mtikila
aliendelea na DP (CCD kwa Kimombo) yake, kwanza akiwa mshauri na baadaye
Mwenyekiti wa taifa hadi mauti yalipo mfika 2015.
Mzee Mwakitwange hakuelewana
na wafuasi wa Mzee Kambona wakiongozwa na Mzee Dustan Lifa Chipaka na hivyo
kuzaliwa vyama viwili, Popular National Party (PONA) kikiongozwa na Mwenykiti
wake Mzee Mwakitwange na Katibu Mkuu Peter Terry (sijui kama bado anaishi).
Kundi la wafuasi wa Mzee Kambona likiongozwa na Mzee Chipaka lilianzisha chama
cha Tanzania Democratic Alliance (TADEA).
Aidha kabla ya Julai 1992
vilianzishwa vyama vya Liberal Democratic Party (LDP) kilichoongozwa na Mzee
Hilal Mapunda, aliyekuwa mhadhiri wa Chuo cha Chama Kivukoni; National Reconstruction
Alliance (NRA/NAREA) kilichoongozwa na Mzee Abubakar Olotu na baadaye Profesa
Kigoma Ali Malima (muda mfupi sana-apumzike kwa amani); na chama cha National
League for Democracy (NLD) kilichoongozwa na Dr. Emmanuel Makaidi (apumzike kwa
amani) hadi alipofikwa na mauti mwaka 2015.
4.
UJIO WA CHADEMA NA MZEE EDWIN MTEI
Kunako April 1992, Prince Bagenda akiambatana na James
Mbatia alitumwa na viongozi wenzake kumfuata Mzee Mtei Nyumbani kwake,
Usa River, Arusha. Kabla ya hapo kulikuwa kumefanyika mazungumzo ya simu kati
ya Mzee Mtei na Mabere Marando, kumshawishi mzee Mtei ajiunge NCCR-Mageuzi. Mzee Mtei alishauri
apelekewe Katiba na andiko la Seraza
Chama cha NCCR- Mageuzi. Kwa hiyo, safari ya Bagenda ilikuwa kwenda kuongea
naye ana kwa ana lakini pia kumpatia nyaraka za chama alizokuwa amesahuri
azisome na kuzielewa kabla ya kufanya uamuzi wa kujiunga NCCR-Mageuzi.
Baada ya Mzee Mtei kupokea nyaraka hizo aliahidi kuja Dar es Salaam
kukutana na 'vijana' na kisha kuwapa msimamo wake. [sikumbuki tarehe, ila ni
mwezi huo huo wa Aprili /92] Marando, Bagenda na Chimoto walipopata taarifa
kuwa Mzee Mtei tayari alikuwa amerejea Dar es salaam walifanya miadi kwenda
kumwona na kisha kupata jibu lake, wakiwa na matumani kuwa angejiunga na chama
cha NCCR -Mageuzi.
Walipofika nyumbani kwake na kumkuta, Mzee Mtei
aliwakaribisha na kisha kuwaambia maneno haya, "kuna watu wenye means and
substance wamekuwa wakinishawishi kuanzisha chama.
Nimeamua kuanzisha
chama kwa hiyo ninyi vijana mwende mvuje chama chenu kisha mje kujiunga kwenye
chama change nitakachoanzisha". Kwa kauli hiyo vijana hao walipoa, ila
Marando alimjibu na hapa ninamnukuu, "Mzee Mtei tumetumia muda, akili,
nguvu, pesa na kunyeshewa na mvua nyingi wakati wa kuanzisha chama cha NCCR
-Mageuzi, tunakushauri uendelee na juhudi zako ila tunaamini huko tuendako mvua
itakunyeshea pia, na ikiwa hivyo, kisha ukitafuta mahali pa kujikinga
tutakukaribisha kujikinga pamoja".
Kesho yake tulipata taarifa kuwa saa 5 mchana juu ya alama
Mzee Mtei alikuwa aongee na waandishi wa
habari pale Motel Agip.
Mwandishi aliyekuwa ametumwa na NCCR-Mageuzi alirejesha
feedback kuwa Mzee Mtei akiwa na marafiki zake wa enzi zake - Bob Makani,
Edward Barongo na wengineo, alikuwa ametangaza kuanzisha chama mara baada ya
kuwepo kwa sheria ya kuruhusu Tanzania kuwa nchi ya vyama vingi vya Siasa.
Kwamba chama hicho kingeitwa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA); na
kwamba kwenye mkutano huo waasisi wote waliokuwepo walikuwa wamevaa sare -
walifunga tai, makoti yakiwa yamening’inizwa ukutani na suruali zao
zikining'nia kwenye suspenders.
Taarifa hiyo haikushangaza viongozi na wanachama wa NCCR
Mageuzi ila nyaraka walizopewa waandishi wa habari zilikuwa ni zile zile (copy
right) Prince Bagenda alizompelekea Mzee Edwin Mtei Nyumbani kwake Usa River -
Katiba na Sera za NCCR Mageuzi isipokuwa kubadilishwa (replace with) maneno
'NCCR-Mageuzi' kwa 'CHADEMA' basi.
Ukiangalia nembo ya NCCR -Mageuzi utaona kuwa hata maneno Demokrasia na
Maendeleo yalitolewa humo. Maneno ya Mzee Mtei na wenzake kwa jina CHADEMA ni
[CHA] tu, DEMA ilichomolewa kwenye nembo ya NCCR-Mageuzi.
Hii ni historia kwa kifupi sana ya kutafutana na kukutana
kwa waasisi wa mageuzi wakati wa harakati za awali za kuasisiwa [tena] kwa mfumo
wa siasa za vyama vingi hapa nchini Tanzania.
Imeandikwa na Bubelwa Kaiza
Post a Comment