Mkazi wa jijini Dar es Salaam,
Robert Massawe (51), ambaye polisi wanadai ni mtuhumiwa wa uporaji na mauaji,
ameuawa kwa kupigwa risasi na watu wanaodaiwa kuwa ni wahalifu wenzake.
Kabla ya kuuawa katika majibizano ya
risasi, mtuhumiwa huyo anadaiwa alikamatwa akiwa na SMG yenye risasi 24, simu
19 zilizoporwa maeneo mbalimbali na laini za simu 58.
Taarifa iliyotolewa jana Jumanne na
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Hamisi Issah imesema mtuhumiwa aliuawa
na wenzake saa tisa usiku wa kuamkia jana wilayani Rombo.
Alisema mtuhumiwa pamoja na mkewe
walikamatwa jijini Dar es Salaam na baada ya kuhojiwa na polisi inadaiwa
alieleza matukio ya ujambazi aliyoshiriki na alikubali kuwaonyesha mahali
alipoficha bunduki.
Polisi imesema simu tatu kati ya 19
wamegundua ziliporwa Moshi na moja alikuwa akiitumia mkewe ambaye anashikiliwa
Dar es Salaam.
Kamanda Issah alisema aliwaeleza
polisi kuhusu mpango wa kufanya tukio la ujambazi katika Kijiji cha Chilio,
Kata ya Holili wilayani Rombo jana alfajiri.
Alisema askari walifuatana naye
chini ya ulinzi hadi Moshi kwenye dampo lililopo jirani na kiwanda cha ngozi
ambako bunduki ilifukiwa ardhini ikiwa na risasi 24.
“Chini ya ulinzi wa askari kanzu,
alipowaona wenzake alipiga kelele kuwajulisha polisi walikuwepo eneo hilo,”
alisema.
Kamanda Issah alisema kelele
ziliwafanya watuhumiwa hao kukimbia huku wakifyatua risasi hovyo na baadhi
zilimpiga Massawe mkono wa kushoto, mgongoni na mguuni hivyo kusababisha kifo
chake.
Polisi imesema mtuhumiwa alishiriki
matukio manane ya uporaji wa fedha na mauaji kwa kutumia silaha na amewahi
kufungwa kwa ujambazi lakini aliachiwa baada ya kukata rufaa.
Post a Comment