Karagwe forum Karagwe forum Author
Title: HOTUBA YA MHESHIMIWA UMMY MWALIMU (MB) WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO, WAKATI WA MAKABIDHIANO NA UZINDUZI WA WODI YA WAZAZI KATIKA HOSPITALI YA RUFAA YA MKOA WA KAGERA - BUKOBA TAREHE 15/07/2016
Author: Karagwe forum
Rating 5 of 5 Des:
Mhe. Major Jenerali Mstaafu Salum Mustafa Kijuu, Mkuu wa Mkoa,        Katibu Tawala wa Mkoa, Armantus Msole,        Wajum...





Mhe. Major Jenerali Mstaafu Salum Mustafa Kijuu, Mkuu wa Mkoa,
       Katibu Tawala wa Mkoa, Armantus Msole,
       Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama,
       Mhe. Mkuu wa  Wilaya ya Bukoba Mjini, Deodatus Lucas Kinawilo,
       Mganga Mkuu wa Mkoa, Dkt. Thomas Rutachunzibwa,
       Mstahiki Meya Manispaa ya Bukoba - Chifu Karumuna,
       Mkurugenzi - Manispaa ya Bukoba,
       Mkurugenzi wa Shirika la Jhpiego - Tanzania, Jeremie Zoungrana,
       Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Marekani (USAID) - Tanzania,
       Wajumbe wa Bodi ya Ushauri ya Hospitali,
       Viongozi wa Dini,
       Watumishi wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Kagera,
       Wandishi wa Habari,
       Wageni Waalikwa,
       Mabibi na Mabwana.



Awali ya yote, napenda kuchukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kunijalia fursa ya kuja kujumuika nanyi katika shughuli hii muhimu ya leo. Pili, ninakushukuru wewe binafsi Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa kwa kunialika ili nijumuike nanyi katika tukio hili. Vile vile, nitumie fursa hii kukupongeza sana kwa kuaminiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa John Pombe Magufuli, kwa kukuteua kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera. Hongera sana.

Wageni Waalikwa,
Suala la kuongeza usawa katika utoaji huduma za afya, ili kupunguza vifo vya wanawake wajawazito pamoja na watoto wachanga na wale walio chini ya umri wa miaka mitano, ni mojawapo ya vipaumbele vya Serikali ya awamu ya tano. Wote tumeshuhudia msisitizo wa Mheshimiwa Rais katika kuhakikisha kuwa huduma za afya zinaboreshwa hapa nchini. Ninawapongeza na kuwashukuru wote wanaounga mkono juhudi za Serikali.



Wageni Waalikwa,
Serikali kwa kushirikiana na wananchi na wadau mbalimbali, imefanikiwa kupunguza vifo vya watoto wenye umri chini ya miaka mitano kutoka vifo 166 kwa kila vizazi hai 1,000 mwaka 1990, hadi vifo 54 kwa kila vizazi hai 1,000 mwaka 2012, na hivyo kufikia lengo namba tatu la Maendeleo ya Milenia. Kiwango cha vifo vya wanawake wajawazito kilipungua kwa takriban nusu, kutoka vifo 870 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 1990 hadi vifo 432 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2012 na kushindwa kufikia lengo namba tano la maendeleo ya Milenia ambalo lililenga vifo 193 kwa kila vizazi hai 100,000.
Kwa Mkoa wa Kagera wastani wa wanawake wajawazito 70 hupoteza maisha kila mwaka. Aidha, watoto wenye umri chini ya mwezi mmoja wapatao 280 - 300 hupoteza maisha kila mwaka, na wastani wa watoto 980 wenye umri chini ya miaka mitano hufariki kila mwaka. Hii ni kulingana na taarifa kupitia mfumo wa huduma za afya,  upo uwezekano kuwapo kwa vifo visivyojulikana katika ngazi ya jamii. Idadi hii ya vifo ni kubwa mno, hivyo ni jukumu letu sote kuhakikisha tunaungana ili tuokoe maisha ya makundi haya muhimu.

Wageni Waalikwa,
Mkakati wa Wizara yangu katika kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi, vifo vya watoto wachanga na watoto chini ya miaka mitano unazingatia mambo ya msingi yafuatayo:
       Kuboresha na kuongezea hadhi vituo vya afya ambavyo vipo karibu na wananchi, ili viweze kutoa huduma za upasuaji wa kutoa mtoto na damu salama.
       Kuongeza upatikanaji wa damu salama.
       Kuhamasisha wanawake wajawazito kujifungulia katika vituo vya kutolea huduma ya afya. Ili kuvutia wanawake wajawazito kujifungulia katika vituo vya kutolea huduma ya afya, Vituo hivi vimeagizwa kuwa na wodi za kujifungulia zinazokidhi viwango na ubora unaokubalika, vifaa tiba na vitendea kazi vya kutosha.  Aidha, serikali inatoa kifurushi cha vifaa muhimu vinavyotumika wakati wa kujifungua, vifaa hivi hutolewa wakati mama anahudhuria kliniki, ili kumuondolea adha ya kuagizwa kununua vifaa wakati anapokwenda kujifungua na kama kivutio cha kujifungulia katika vituo vya kutolea huduma ya afya. Kwa sasa huduma hii inatolewa katika mikoa sita ya Kagera, Mara, Geita, Mwanza, Simiyu na Shinyanga kanda ya ziwa, na lengo ni kuifikia mikoa yote.











       Kuhakikisha kuwa wanawake wajawazito wanahudhuria kliniki ya wajawazito angalau mara nne, ili waweze kuchunguzwa afya zao kwa minajiri ya kutambua viashiria vya hatari, na magonjwa ili kuanza tiba kama itakavyohitajika. Pia, wajawazito hupewa dawa za kuzuia malaria, chanjo ya kuzuia pepopunda, pamoja na kupewa ushauri nasha na kupima magonjwa ya kuambukiza kama UKIMWI, Kaswende, na kwa wale watakaogundulika kuwa wameathirika hupewa huduma hapo hapo.



       Kuhakikisha kuwa jamii inatumia njia za kisasa za uzazi wa mpango, ili kuepuka mimba zisizotarajiwa  kwa lengo la kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na vifo vya watoto wachanga.


       Kuhamasisha na kushirikisha jamii katika kupanga na kutekeleza mambo yanayohusu afya ya mama na mtoto.
       Kushirikisha wadau mbalimbali yakiwemo mashirika ya umoja wa mataifa, mashirika ya dini, mashirika yasiyo ya kiserikali na watu binafsi katika masuala yanayohusu afya ya mama na motto.




Wageni Waalikwa,
Kwa niaba ya Serikali napenda kutoa shukrani za dhati kwa wadau wetu wote, wanaounga mkono juhudi za serikali kuhakikisha kuwa haya yote yanatekelezwa kama ilivyopangwa. Nimepata taarifa ya kazi kubwa ya wadau wa afya katika Mkoa wa Kagera, wakiwemo:
       "Management and Development for Health" (MDH), kwa upanuzi wa Zahanati huko Muleba na katika Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba.


        Ninatambua kazi nzuri ya ujenzi wa kituo cha benki ya damu salama cha Mkoa wa Kagera, pamoja na ghala la kuhifadhia vifaa vya chanjo linayoendelea ndani ya Hospitali hii ya mkoa, chini ya ufadhili wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya watu - UNFPA.


        Nimepata taarifa kuwa ICAP imefanya kazi kubwa katika eneo la kudhibiti UKIMWI katika Mkoa huu kwa zaidi ya miaka kumi sasa, ninawapongeza sana kwani takwimu zinaonyesha kuwa kiwango cha maambukizi kinashuka katika Mkoa wa Kagera. Pia, Shirika la ICAP limefanya upanuzi wa miundombinu katika baadhi ya vituo vikiwemo Hospitali hii ya Mkoa, Kituo cha Afya Kaigara (Muleba), na Nyakahura
        Ninatambua mchango wa kila mdau: Abott Associates, Amref, TCDC, Red Cross, Marie Stopes na Engender Health.

Wageni Waalikwa,
Kwa tukio hili maalum la leo, kipekee napenda kuwapongeza shirika la Jhpiego, ambalo pamoja na kushiriki katika  maeneo mengine ya afya hapa nchini, ndilo limefadhili kazi ya upanuzi na ukarabati wa wodi hii ya wazazi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera.  Kukamilika kwa ukarabati huu, kumeifanya wodi hii kuwa ya kisasa inayomuwezesha mama mjamzito kujifungua katika mazingira safi na salama. Nimetaarifiwa kuwa kabla ya upanuzi huu, wazazi walikuwa wanalala chini tena kwa kubanana hali inayopelekea kuambukizana  magonjwa. Ukarabati huu ni matunda ya ziara ya Rais wa Jhpiego Dkt. Leslie Mancuso, aliyoifanya hapa mwezi wa Aprili, 2016 na kuguswa na msongamano wa wajawazito katika wodi ya wazazi. Naambiwa kazi kama hii imefanyika katika Hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Mara. Juhudi hizi zinanipa faraja kuwa huduma zetu zitawafikia wanawake wajawazito wengi zaidi.




Nimetaarifiwa kuwa, wodi hii imeanza kutumika japo kuna upungufu wa vitanda, tunaomba tuzidi kushirikiana ili vitanda vipatikane.

Wageni Waalikwa,
Upanuzi huu uliofanyika ni sehemu katika kuboresha utoaji wa huduma kwa wazazi. Lengo la Serikali ni kupanua wodi ya kujifungulia ambazo ni ndogo, kujenga vyumba vya upasuaji kwa ajili ya wajawazito pekee, pamoja na kujenga wodi maalum ya watoto wachanga. Kazi hii ni kubwa, hivyo tunahitaji nguvu ya pamoja na ushirikiano wa wadau wote mliopo hapa leo. Nimeambiwa upo mkakati wa kufanya harambee ya kuchangia miradi hii pamoja na ujenzi wa nyumba za watumishi. Ninaomba kila mmoja wetu achangie chochote katika kutekeleza mradi huu.










Tukishirikiana na tukajitolea tutaweza kubadilisha huduma za afya zilizopo sasa.

Wageni Waalikwa,
Ninatambua kazi kubwa inayotekelezwa chini ya mradi wa Maternal and Child Survival Programe (MCSP) ikiwa ni pamoja na; kutoa mafunzo ya uzazi salama kwa wataalam wa Afya, huduma ya uzazi wa mpango, mafunzo kwa Wahudumu wa Afya ngazi ya Jamii, kuboresha wa upatikanaji na matumizi ya takwimu za afya kwa ajili ya mipango ya afya. Mambo yote haya yanasaidia kuboresha huduma za mama na mtoto kwa lengo la kuzuia vifo na ulemavu.



Kutokana na kazi hii nzuri, ninapenda kurudia kulishukuru Shirika la Jhpiego kwa kuamua kuja Mkoa wa Kagera kushirikiana na Mkoa huu kuboresha huduma za afya ya  mama na mtoto.

Wageni Waalikwa,
Serikali kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya afya itaendelea kuwajengea uwezo watoa huduma kuweza kutoa huduma za dharura kwa wanawake wajawazito, kuhimiza Halmashauri zote kuweka kipaumbele kwenye uzazi salama na kushirikisha wananchi na jamii kwa ujumla juu ya kutokomeza vifo vya wanawake vitokanavyo na uzazi. Tuige mfano wa wananchi wa kijiji cha Utulo, katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya. Wananchi wa kijiji hicho wameweka mikakati ya kudhibiti vifo vya watoto wachanga katika jamii yao ambapo toka mwaka 1998 hakuna vifo vitokanavyo na uzazi vilivyoripotiwa katika Zahanati ya kijiji hicho.



Mwisho:
Wizara imeanza kutoa taarifa kila baada ya robo mwaka ya vifo vitokanavyo na uzazi. Nasisitiza kwamba kila wilaya iwasilishe Wizarani taarifa ya vifo vitokanavyo na uzazi kila wiki pamoja na taarifa ya (Infections Disease Week Ending  - IDWE), Kwani ni mojawapo ya chanzo cha takwimu zinazotumika kuandaa taarifa ya robo mwaka.





Baada ya kusema hayo machache, sasa niko tayari kuzindua wodi ya wazazi, iliyokarabatiwa na Shirika la Jhpiego

ASANTENI KWA KUNISIKILIZA.

About Author

Advertisement

Post a Comment

 

This Template Is Designed By Jacksay | call 0764 031 242 for this service

Top