Aliyekuwa
Waziri wa Fedha katika Serikali ya awamu ya tatu, Basil Mramba,
ameishauri Serikali kuhakikisha inawatumia wafungwa kutumikia jamii
badala ya kuwarundika magerezani.
Amesema pamoja na hayo, maisha ya gerezani si salama na si njia pekee ya kumrekebisha mhalifu aliyehukumiwa na mahakama.
Kutokana
na hali hiyo, alisema kuna haja kwa Serikali kuanza kutumia sheria
namba 6 ya huduma kwa jamii kuwaangalia wafungwa wenye taaluma kutumika
adhabu zao katika fani au taasisi za umma ili kupunguza gharama
kuwahudumia watu ambao wanaweza kuisaidia jamii.
Mramba
alitoa kauli hiyo jana, wakati yeye na mwenzake aliyekuwa Waziri wa
Nishati na Madini, Daniel Yona, walipomaliza kufanya usafi katika
Hospitali ya Sinza Palestina, Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya
kutumikia adhabu ya kifungo chao cha nje baada ya wiki iliyopita
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuridhia kuwa wanastahili kutumikia
jamii kwa kipindi cha miezi sita hadi Novemba 5.
Alisema
imekuwa ni kawaida jamii kuwa na mtazamo kwamba mtu yeyote anayekutwa
na hatia lazima atapelekwa jela ajirekebishe na kuacha tabia aliyonayo
jambo ambalo si sahihi.
“Jamii
inaamini jela ni sehemu salama na mtu akishikwa na hatia kwa kosa
lolote, mahala sahihi ni jela tu, kule anakutana na watu wa kila aina,
wenye makosa tofauti, hali ambayo inamfanya ajifunze mambo mengine
mapya.
“Unakuta
mtu amefanya uhalifu wa kuiba kitu, anafungwa na kupelekwa gerezani,
anakutana na majambazi sugu wanaompa mbinu zaidi, sasa akitoka jela
anakuja akiwa ameiva, anarudia kwenye matukio akiwa amekamilika,” alisema Mramba.
Alisema kuwapeleka wafungwa katika huduma za kijamii kutasaidia kupunguza gharama kwa Serikali na msongamano ndani ya magereza.
Akizungumzia
suala la kuwatumia wafungwa ambao ni wanataaluma, Mramba alisema sheria
hiyo ikitumika vizuri italisaidia taifa kwani wapo baadhi ya wafungwa
wana taaluma ya udaktari, ualimu, ufundi na uhasibu, ambao wanaweza
kutumika katika fani zao kwenye taasisi za umma.
“Kuna
maeneo mengine yana uhaba wa wataalamu ambao wengine wapo magerezani
wanahudumiwa na Serikali kuanzia chakula, malazi na hata afya zao, hivyo
wakiwatumia hao itakuwa faida kwa taifa kwa kuwa watafanya kazi bila
malipo,” alisema Mramba.
Alisema
suala la kuwatumia wafungwa katika huduma za kijamii si geni kwa nchi
zilizoendelea ambako kwa kiasi kikubwa wamesaidia kuinua uchumi wa nchi
zao.
Kwa
siku ya jana, Mramba na Yona walianza kufanya usafi saa 2 asubuhi kwa
kufagia nyuma ya jengo la wazazi katika hospitali hiyo.
Naye
Ofisa Huduma za Jamii Mkoa wa Dar es Salaam, Deogratius Shirima,
alisema gharama zinazotumika kuwahudumia wafungwa magerezani ni kubwa,
hivyo ni vyema wale wanaoguswa na sheria ya huduma za jamii namba 6 ya
mwaka 2002 kutumikia kifungo cha nje.
“Sheria
hii ni vyema ikatumika kwa wale inaowagusa kwani itapunguza gharama za
kuwahudumia magerezani, na pia adhabu wanayopata wafungwa wa nje ni wazi
jamii ambayo ndiyo iliyokosewa inaona utekelezaji wake kwa uwazi,” alisema Shirima.
Alisema
mataifa mengine ikiwamo nchi ya Kenya wanatumia sheria hiyo ambapo nusu
ya wafungwa nchini humo wapo katika huduma za jamii.
Februari
6, mwaka huu mawaziri hao walibadilishiwa adhabu ya jela na kupewa
adhabu ya kutumikia kifungo cha nje mwishoni mwa wiki iliyopita na
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, baada ya kukamilika kwa mchakato wa
kufikia hatua hiyo.
Hakimu
Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Cyprian Mkeha, alisema sheria ya huduma kwa
jamii namba 6 kifungu namba 3(1) ya mwaka 2002 inasema mtu yeyote
anayetiwa hatiani kwa kosa ambalo adhabu yake ni miaka mitatu kushuka
chini mahakama inaweza kumpa adhabu ya kutumikia jamii.
Mramba
na Yona, ambao baada ya rufaa walibakiwa na adhabu ya miaka miwili,
walitiwa hatiani kwa kutumia madaraka vibaya ambapo walitakiwa kumaliza
kifungo Novemba mwaka huu.
Hata
hivyo, hakimu huyo alisema magereza walifikisha barua mahakamani hapo
Desemba 5, mwaka jana yenye kumbukumbu namba 151/DAR/3/11/223,
wakipendekeza kifungo cha nje kwa mawaziri hao.
Hakimu
Mkeha alisema baada ya kupokea barua hiyo, mahakama iliamuru watu wa
huduma za jamii kuchunguza kama wanastahili kupewa adhabu hiyo na kwamba
walifanya hivyo na kurudisha ripoti kwamba wanastahili.
Alivitaja vigezo vya kupewa adhabu hiyo kuwa ni umri ambapo Mramba na Yona wana miaka 75.
Post a Comment