Mbunge wa Jimbo la Kigamboni (CCM)
Dkt Faustine Ndugulile ameyataka Mataifa kushirikisha Mabunge katika
kufanikisha mpango wa Usalama wa Afya Duniani (Global Health Security Agenda).
Akizungumza kwenye mkutano wa
masuala ya Usalama wa Afya ulioandaliwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) na kufanyika
Jijini Bali, Indonesia, ulioanza Juni 27 na kuhitimishwa Juni 30 Dkt Ndugulile amesema, Mabunge yanaweza kutoa
mchango mkubwa sana kwenye utekelezaji wa Mpango wa Usalama wa Afya Duniani kwa
kusimamia Serikali na kuhakikisha hatua zote muhimu zinatekelezwa, kutunga
Sheria zitakazosimamia utekelezaji wa mpango huu pamoja na kuhakikisha mpango
huu unapata fedha za kutosha kutoka kwenye Bajeti ya Serikali.
Aidha Dkt Ndugulile amesema kuwa
muingiliano wa shughuli za kilimo, mifugo na shughuli nyingine za kibinadamu
zimesababisha baadhi ya magonjwa ya wanyama kuleta athari kwa binadamu na pia
usugu wa madawa ya aina ya antibiotiki na kuongeza kuwa kuna haja ya wadau wa sekta hizi kuwa na
ushirikiano wa karibu chini ya mpango wa “Afya Moja”
Amesema kuwa Ili mpango wa “Afya
Moja” ufanikiwe in lazima maboresho yafanyike kwenye uratibu wa sekta
mbalimbali ndani ya nchi na pia kuandaa mpango wa pamoja wa udhibiti na
kushughulikia majanga.
Dkt Ndugulile mbali ya kuwa Mbunge
wa Jimbo la Kigamboni, ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ushauri ya Mabunge Duniani
(Inter Parliamentary Union) kuhusiana na masuala ya UKIMWI, Afya ya Wanawake,
Vijana na Watoto.
Post a Comment