JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
OFISI YA RAIS
TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA
Anwani
ya Simu: “REGCOM”
Simu
ya mdomo: (028) 2220215-18
E-mail:
ras.kagera@pmoralg.go.tz
Fax: (028) 2222341 / 2221356
|
|
OFISI YA MKUU WA MKOA,
S. L. P. 299,
BUKOBA - KAGERA.
TANZANIA.
|
TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
TAREHE 04 AGOSTI, 2O16
Ndugu Waandishi wa Habari, Wiki
ya Agosti 1 hadi 7, Tanzania huungana na nchi nyingine ulimwenguni kuadhimisha
wiki ya unyonyeshaji maziwa ya mama Duniani. Maadhimisho hayo yamekuwa
yakifanyika tangu mwaka 1992 kufuatia Azimio la Innocent (nchini Italia) ambalo
linasisitiza umuhimu wa kulinda, kuendeleza na kusaidia unyonyeshaji na
ulishaji bora wa watoto. Wiki ya Unyonyeshaji
inatukumbusha kuwa unyonyeshaji wa maziwa ya mama pekee katika miezi sita ya
mwanzo ya maisha ya mtoto na kuendelea kunyonyeshwa mpaka umri wa miaka miwili
au zaidi. Aidha, Wiki ya unyonyeshaji, mwaka huu 2016 inaadhimishwa Kitaifa Mkoani
kwetu Kagera.
Ndugu Waandishi wa Habari, Kauli mbiu ya mwaka huu 2016, ni “UNYONYESHAJI WA MAZIWA YA MAMA: MSINGI KWA MAENDELEO
ENDELEVU.” Tunaelewa wazi kuwa pamoja na maendeleo
ambayo Mkoa wetu umekuwa ukiyapata katika maeneo mbalimbali, bado utapiamlo
umeendelea kuathiri jamii hususani katika nyanja za afya,elimu na uchumi; hivyo
kusababisha kasi ya kupungua kwa umaskini kutoridhisha. Lishe duni si tu
inaathiri maendeleo ya mtoto lakini pia inaathiri ukuaji wake kimwili na
kiakili hatimaye kuathiri mchango wake katika maendeleo ya Taifa katika kipindi
chote cha uhai wake.
Ndugu Waandishi wa Habari, Wiki
ya Unyonyeshaji Maziwa ya Mama ina umuhimu mkubwa sana kwa Mkoa wetu
ukizingatia kuwa takribani asilimia 52 ya watoto wenye umri chini ya miaka
mitano katika Mkoa wetu, wamedumaa. Udumavu huu unatokana na lishe duni
waliyoipata watoto hawa tangu wakiwa wadogo ikiwemo suala zima la unyonyeshaji.
Lazima tuungane wana Kagera kubadilisha hali hii; Mkoa wetu ni kati ya Mikoa
yenye chakula cha kutosha na fursa nyingi, hivyo ni lazima tuungane kuondoa huu
udumavu kwa watoto.
Sababu
kubwa ya utapiamlo huu kwa watoto ni ulishaji usio sahihi ambao huchangiwa na
majukumu mengi yanayomkabili mama na hivyo kukosa muda wa kutosha wa kumtunza
mtoto. Ni dhahiri kuwa mchango wa mwanamke katika familia, ajira na uzalishaji
kwa ujumla ni mkubwa hivyo ni muhimu kuwatia moyo na kuwasaidia wanawake ili
waweze kutimiza majukumu ya uzalishaji na utunzaji familia kwa ukamilifu.
Ndugu Waandishi wa Habari, Nasistiza
Sheria ya Ajira na Mahusiano kazini ya mwaka 2004 kuzingatiwa hasa katika mkoa
wetu ili kumruhusu mama mwajiriwa anayenyonyesha apewe ruhusa ya masaa mawili
kila siku ili akamnyonyeshe mtoto wake, pia mama aliyejifungua mtoto mmoja
kupewa likizo ya uzazi ya siku 84 kama amejifungua mtoto mmoja na siku 100 kwa
watoto zaidi ya mmoja. Pia baba kupewa likizo ya siku 3 ndani ya wiki moja
aliyojifungua mama ili kutoa huduma kwa mama.
Aidha
sheria hiyo inakataza mama aliye ajiriwa na ambaye ananyonyesha au mjamzito
kufanya kazi ngumu au za hatari kwa afya yake au ya mtoto wake. Kwasababu hii,
ninatoa wito kwa Taasisi zisizo za Kiserikali, Taasisi za Kijamii na za Kidini,
jamii na familia kwa ujumla kuwasaidia wanawake ambao hawapo kwenye ajira rasmi
ili waweze kuwanyonyesha watoto wao ipasavyo.
Ndugu Waandishi wa Habari, (Ushauri)
Mtoto anyonyeshwe ndani ya saa moja baada ya kuzaliwa. Pia mtoto anyonyeshwe
maziwa ya mama pekee katika miezi sita ya mwanzo. Uji, ugali, ndizi, maziwa ya
kopo au ng'ombe, havitakiwi kwa mtoto mwenye umri chini ya miezi sita; Mwili wa
mtoto wa umri huu hauna uwezo wa kuvitumia, hivyo mtoto akipewa vyakula hivi
hujaza tumbo tu na kumfanya mtoto kujisikia ameshiba na kumzuia kunyonya aidha,
mtoto anyonye mara kwa mara kadiri anavyohitaji.
Ndugu Waandishi wa Habari, (Umuhimu
wa Maziwa ya mama) Kunyonyesha maziwa ya mama pekee katika miezi sita
ya mwanzo ya maisha ya mtoto ndio njia bora na salama ya kumpatia virutubishi
vyote muhimu kwa ukuaji na maendeleo yake. Maziwa ya mama yana sifa ya kipekee
ya kuwa na kinga ambazo humkinga mtoto dhidi ya magonjwa hivyo kuchangia katika
kupunguza vifo vya watoto chini ya umri wa miaka mitano. Unyonyeshaji sahihi wa
maziwa ya mama katika miezi sita ya mwanzo pia huweza kutumika kama njia ya
uzazi wa mpango. Tendo la kunyonyesha pia linajenga mahusiano kati ya mama na
mtoto wake. Mtoto anapofikia umri miezi sita, anapaswa kuanzishiwa vyakula vya
nyongeza, lakini aendelee kunyonyeshwa maziwa ya mama mpaka atimize miaka
miwili au zaidi.
Ndugu Waandishi wa Habari, (Mikakati) ili
kufanikisha unonyeshaji jamii inashauriwa kutekeleza mikakati ifutayo;
Kuanzisha na kuendeleza vikundi vya kusaidia masuala ya unyonyeshaji ambavyo
vitawashirikisha baba au wanaume.
Kuhakikisha
kuwa vituo vya afya, maduka ya dawa na maduka ya bidhaa mbalimbali yanatekeleza
kanuni inayodhibiti uuzaji na usambazaji wa maziwa na vyakula vya watoto.
Kuwaunganisha
vijana wa kike na wa kiume ili waweze kubadilishana uzoefu na kupeana mbinu za
kuboresha unyonyeshaji wa maziwa ya mama.
Kuhakikisha
kuwa vituo vyote vinavyotoa huduma ya afya vinatekeleza vidokezo kumi vya
kufanikisha unyonyeshaji wa maziwa ya mama na hivyo kuwa Rafiki wa Mtoto.
Nawaombeni wananchi kabla hamjaondoka hakikisheni mnapitia kwenye mabanda yetu
hapa chini kuelekezwa juu ya vidokezo hivyo.
Ndugu Waandishi wa Habari, (Wito)
Serikali inatambua kuwa bado zipo changamoto nyingi katika kukabiliana na
utapiamlo hapa Mkoani mwetu. Pengine,
changamoto kubwa kuliko zote ni ile ya uelewa mdogo wa masuala ya lishe katika
jamii ikiwemo unyonyeshaji, kuanzia ngazi ya familia hadi kwa watendaji na
viongozi wa Serikali. Uelewa mdogo kuhusu masuala ya lishe umesababisha masuala
ya lishe kutopewa kipaumbele katika jamii ambako ndiko waliko watoto na
wanawake wengi wanaohitaji zaidi huduma bora za lishe.
Nipende
kutoa wito kwenu Wanahabari kutumia ujuzi wenu na vyombo vyenu vya Habari kwa
kushirikiana na wadau mbalimbali wa afya kuielimisha jamii hasa katika Mkoa
wetu wa Kagera juu ya kukabiliana na utapiamlo na umuhimu wa unyonyeshaji wa
maziwa ya mama kama inavyoshauriwa na wataalamu wetu wa lishe ili tuwe na
kizazi cha watoto wenye afya zilizoimarika.
Kagera: Kazi Amani na Maendeleo
Imetolewa na; Mhe. Meja Jenerali (Mst) Salum M. Kijuu
Mkuu
wa Mkoa
KAGERA
Post a Comment