JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
OFISI YA RAIS
TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA
Anwani
ya Simu: “REGCOM”
Simu
ya mdomo: (028) 2220215-18
E-mail:
ras.kagera@pmoralg.go.tz
Fax: (028) 2222341 / 2221356
|
|
OFISI YA MKUU WA MKOA,
S. L. P. 299,
BUKOBA - KAGERA.
TANZANIA.
|
TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
TAREHE 04 AGOSTI, 2O16
Ndugu
Waandishi wa Habari,
Katika
Mkoa wetu wa Kagera vimeibuka vitendo vya hujuma hasa wakati huu wa majira ya
kiangazi (hususani mwezi Juni na Julai 2016) ambapo wananchi wenye nia mbaya na
Taifa na Mkoa wetu wamekuwa wakichoma moto ovyo na kuteketeza misitu ya hifadhi
ya Serikali, mashamba ya miti ya watu binafsi na mashamba ya mazao ya chakula suala
ambalo halikubaliki na ni kinyume na sheria zilizowekwa na
nchi yetu.
Ndugu
Waandishi wa Habari,
Kwa taarifa nilizonazo za uchomaji moto katika Halmashauri za Wilaya tatu mkoani kwetu ni kama ifuatavyo; Kufikia
Agosti 3, 2016 katika Manispaa ya Bukoba
maeneo yaliyoripotiwa kuchomwa moto ni ekari tisa na nusu (9.5) zenye thamani
ya zaidi ya shilingi milioni ishirini (20,000,000)
Katika Halmashauri ya Wilaya ya Muleba zaidi
ya ekari 473 za misitu ya hifadhi ya kupandwa na mazao ya chakula imechomwa na
kusababisha hasara ya mamilioni ya fedha kwa wananchi.
Halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo taarifa
zilizonifikia ni kwamba tayari ekari 53 za misitu na mazao ya chakula
zimechomwa na kusababisha hasara ya mamilioni ya fedha pia kwa wananchi. Kwa
hizo Halmashauri chache za Mkoa wa Kagera unaweza kuona uharibifu mkubwa wa
uchomaji moto ulivyosababisha hasara kubwa.
Ndugu
Waandishi wa Habari,
Kutokana na uharibifu huo wa uchomaji moto katika Mkoa wetu wa Kagera na kwa
Mamlaka niliyopewa chini ya kifungu cha
sheria ya Tawala za Mikoa, sheria Na. 19 ya mwaka 1997 Kifungu cha 5
kifungu kidogo cha (1) na (2), Sheria hii inanipa Mamlaka na majukumu ya
kulinda Amani na Usalama na kuhakikisha uzingatiaji wa sheria katika Mkoa wa
Kagera unatimizwa.
Aidha, kwa kuzingatia sheria ya misitu Na. 14
ya mwaka 2002 vifungu vya 70 hadi 73 na Kifungu cha 91 vifungu kidogo (1) na
(2) vinavyozuia mtu yeyote kuchoma mashamba binafsi na misitu ya hifadhi.
Hivyo, ninawaagiza Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya wote Mkoani Kagera kuhakikisha
wanadhibiti uchomaji moto ovyo kwenye Wilaya zao kwa kutumia sheria zilizopo
ikiwa ni pamoja na sheria ndogo za Halmashauri za Wilaya za utunzaji wa
mazingira.
Ndugu
Waandishi wa Habari,
Aidha, naagiza kwa maeneo ambayo yatabainika kuchomwa moto, moto huo uzimwe
mara moja kwa ushirikiano wa wananchi na kumbaini mara moja mwananchi
aliyehusika kuchoma moto huo katika eneo husika.
Pia naagiza Viongozi wote kuanzia ngazi ya
Kitongoji,Kijiji,Kata,Tarafa na Wilaya wenye jukumu la kisheria kusimamia
misitu na mazingira wahakikishe waharifu wa uchomaji moto wanabainika na
kukamatwa na kuchukuliwa hatua kali za kisheria, Viongozi watakaoshindwa kufanya
hivyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Ndugu
Waandishi wa Habari,
Vile vile naagiza Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya kuhakikisha taarifa za kudhibiti
uchomaji moto na kubaini waharifu wa uchomaji moto ovyo zitumwe Ofisini kwangu kila siku. Pia Kamati za Mazingira
zilizoundwa kupitia sheria ya mazingira ya mwaka 2004 kwa ngazi zote zihakikishe zinatekeleza
kazi zake kisheria na kuwasilisha taarifa Mkoani kila Wiki.
Ndugu
Waandishi wa Habari,
Nawakumbusheni kuwa Misitu ni rasilimali muhimu kwa Taifa na kwa Mkoa wetu wa
Kagera kwani misitu ni uhai. Misitu huchangia kuwepo kwa hali nzuri ya hewa,
uwepo wa mvua za uhakika na uwepo wa vyanzo vya maji vya kutosha Mkoani kwetu
na Taifa kwa ujumla.
Sheria ya Misitu Na. 14 ya mwaka 2002
inaitambua misitu ya hifadhi ya asili na ile ya kupandwa na inaeleza wazi ni
jukumu la kila Mwananchi kuhakikisha misitu hii inalindwa na kutunzwa.
Nawakumbusheni wananchi kuhakikisha wanatunza mazingira na kuacha vitendo vya
uchomaji moto ovyo katika mkoa wetu wa Kagera badala yake wanatakiwa kuwa
walinzi mazingira katika maeneo yao.
Imetolewa na; Mhe. Meja Jenerali (Mst) Salum M. Kijuu
Mkuu
wa Mkoa
KAGERA
Post a Comment