Waziri wa Ofisi ya Rais
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Angella Kairuki akiwa Mkoani
Kagera aliawaagiza viongozi wa Mkoa kuhakikisha wanaondoa data chafu za Watumishi
katika mfumo wa utumishi ili kuondokana tatizo la watumishi hewa.
Mhe. Kairuki alitoa agizo
hilo alipokuwa akiongea na Mkuu wa Mkoa
Meja Jenarali Mstaafu Salum M. Kijuu ofisini kwake mara baada ya
kuwasili Mkoani hapa kwaajili ya kikao kazi cha kuongea na Watumishi wa Serikali
kutoka katika Taasisi na Idara mbalimbali za Serikali Mkoani Kagera.
“Mhe. Mkuu wa Mkoa katika
Mkoa wako kuna data chafu kama ifuatavyo, katika Sekretarieti ya Mkoa zipo data
chafu 21, Bukoba Manispaa 70, Biharamulo 296, Halmashauri ya Wilaya Bukoba 429, Karagwe 211, Muleba 51, Ngara 454,
Missenyi 1,608 na Kyerwa 234.” Mhe. Kairuki alitoa takwimu hizo mbele ya Mkuu
wa Mkoa wa Kagera na kusistiza data hizo
kuondolewa katika mfumo mara moja.
Aidha Mhe. Kairuki alifafanua
kuwa data hizo chafu zilibainika wakati Wizara yake ikifanya uhakiki wa Watumishi
kujiridhisha na takwimu zilizotolewa kuhusu watumishi hewa na kubaini kuwa kuna
data chafu ambazo zinasababishwa na baadhi ya Watumishi kutokuwa na akaunti za
benki za kupitishia mishahra yao.
Pia baadhi ya nyaraka za Watumishi
kutofautiana majina na majina halisi
wanayoyatumia kazini na yaliyopo katika mfumo wa Taarifa za kiutumishi na
mishahara (HCMIS). Vilevile baadhi ya Watumishi kuonekana kuwa tayari wamezidi
umri wa miaka 60 ya kustaafu kwa lazima lakini bado wanaonekana kuwa bado wapo kazini
na wanalipwa mishara ya Serikali.
Katika hatua nyingine Mkuu
wa Mkoa wa Kagera Mhe. Kijuu akitoa taarifa ya Mkoa kwa Mhe. Kairuki alisema
kuwa Mkoa wa Kagera una Watumishi 19, 982 aidha, katika zoezi la kuhakiki
Watumishi hewa Mkoa ulibaini watumishi hewa 274 waliolipwa kiasi cha shilingi
bilioni 1,153,690,895.63 na fedha zilizorejeshwa ni shilingi Milioni 103,
725,731.23 sawa na asilimia 8.8%
Vile vile Mhe. Kijuu alimweleza
Waziri Kairuki kuwa Mkoa unakabiliwa na tatizo la baadhi ya nafasi za watendaji kukaimiwa ambapo nafasi hizo ni
59. Jambo ambalo linasababisha baadhi ya maamuzi katika ngazi mbalimbali
kutotolewa kwa wakati na kwa usahihi kutokana na Makaimu hao kutokuwa na madara
kamili.
Akitoa ufafanuzi Mhe.
Kairuki alisema kuwa uhakiki ni zoezi endelevu na kazi hiyo itafanyika kwa
kuangalia alama za vidole ili kubaini wale wanaotumia vyeti vya watu wengine na
kusisitiza hakuna Mtumishi atakayeonewa katika zoezi hilo.
Alisema pamoja na hilo
uhakiki utafanyika kwa kuangalia taarifa mbalimbali za kiutumishi, ikiwamo
waliobadili majina endapo kama taratibu za kisheria zilifuatwa ili kubaini
waliofanya hivyo kwa nia ovu.
Waziri Kairuki aliainisha
kuwa Watumishi wanaokaimu nafasi mbalimbali waangaliwe kama wana sifa
zinazostahili ili kubaini wale waliopo na wenye sifa lakini hawajapewa.
Aliwaelekeza Maafisa
Utumishi kujielimisha kuhusu Kanuni za Kudumu katika Utumishi wa Umma ili
kuepuka malalamiko miongoni mwa Watumishi na kusema ofisi yake inaandaa mfumo ambao
Watumishi wa Umma nchini watawasilisha malalamiko yao kwake pale ambapo
hawataridhika na huduma wanazopewa kwa waajiri wao.
Mwisho Mhe. Kairuki alitumia
muda mwingi katika kikao kazi na Watumishi kusikiliza kero mbalimbali na
masuala mbalimbali yahusuyo watumishi na kuyatafutia ufumbuzi hapo kwa papo.
Post a Comment