Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe.
Meja Jenerali Mstaafu Salum M. Kijuu
azindua Mpango Mkakati wa Kulinda Raslimali za Uvuvi Mkoani Kagera ili kuondokana na uvuvi haramu
na madhara yake yanayosababisha kupungua kwa samaki katika Ziwa Victoria na kupelekea kudhoofisha uchumi wa Mkoa na Mwananchi
mmoja mmoja wanaojishughulisha na shghuli za uvuvi.
Mpango Mkakati huo
umezinduliwa leo Agosti 24, 2016 na Mkuu wa Mkoa katika Mwalo wa Malehe Kituo
cha Kanyigo Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba ambapo aliteketeza nyavu haramu
zilizokamatwa katika doria mbalimbali kupitia kituo hicho zenye thamani ya
shilingi milioni 205, 510,000/-
Kabla ya kuzindua Mpango Mkakati huo Mhe. Kijuu alikitembelea
Kiwanda cha kuchakata minofu ya samaki cha Vicfish ili kujionea uzalishaji wa
kiwanda hicho ambapo Meneja wa Kiwanda Bw.Nurdin Salum Juma alitoa taarifa kuwa uwezo wa kiwanda hicho ni
kuzalisha tani 60 kwa siku lakini kutokana na madhara ya uvuvi haramu kiwanda
hicho kinazalisha tani 6 hadi 8 kwa siku sababu ukosefu wa samaki.
Naye Kaimu Afisa Mfawidhi
Ofisi ya Usimamizi Raslimali za Uvuvi Mkoa wa Kagera Bw. Gabriel Mageni
alimweleza Mkuu wa Mkoa kuwa kuanzia
kipindi cha mwaka 2012 hadi sasa Agosti 2016 ofisi yake imefanikiwa kufanya
doria na kukamata zana za uvuvi haramu katika Vituo vya Kanyigo, Bukoba na
Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba kama ifuatavyo:
Makokoro ya Sangara 192
yenye thamani ya shilingi milioni 96,000,000/-, Timba 3,319 zenye thamani ya
shilingi milioni 232, 330,000/-, Nyavu za Makila 2,410 zenye thamani ya
shilingi milioni 24, 100,000/-, Nyavu za
dagaa chini ya (milimita 88) 25 zenye thamani yashilingi milioni 17,500,000/-
na Kokoro ndogo za vyambo 16 zenye thamani ya shilingi milioni 3,200,000/-,
Jumla kuu ni shilingi milioni 373,130,000/-.
Aidha, Bw. Mageni alimweleza
Mkuu wa Mkoa kuwa changamoto kubwa wanayoipata katika ofisi yake ni kuachiwa
suala la uvuvi haramu wao peke yao kama Maafisa Uvuvi badala ya Taasisi zote za
Serikali na binafsi na Wananchi
kupambana na uvuvi haramu, Pili ni kutopata ushirikiano kutoka kwa viongozi wa
Vitongoji, Vijiji na Kata hasa watendaji na Wenyeviti wanaozunguka katika Ziwa
Victoria.
Akiwahutubia wananchi na wavuvi
katika Mwalo wa Malehe Mhe. Kijuu aliwaeleza kuwa Mkakati aliouzindua utakuwa
shirikishi hasa viongozi na wanachi ili kukomesha uvuvi haramu katika Ziwa Victoria,
aidha, alitoa rai kuwa kiongozi au Mtendaji yeyote atakayegundulika kuhusika au
kukutotoa ushirikiano katika suala la uvuvi haramu atashghulikiwa ipasavyo
kisheria.
Aidha, aliwataka wananchi
wote wanaojihusisha na uvuvi haramu kuacha mara moja ili kuruhusu samaki
kuzaliana na kuvuliwa kwa utaratibu ulio mzuri. Katika hatua nyingine aliwahamasisha
wavuvi kujihusisha na miradi ya ufugaji samaki katika mabwawa kuliko kutegemea
Ziwa la Victoria peke yake.
Mpango Mkakati wa Kulinda
Raslimali za Uvuvi Mkoani Kagera unalenga
kuzuia uvuvi haramu katika Maziwa yanayopatikana katika Mkoa kwa kuendesha
doria za mara kwa mara na endelevu, kuhamasisha wavuvi kukopa na kuwekeza
katika uvuvi wa kisasa, na kutunza mazingira na mazalia ya samaki ili kuongeza
wingi na upatikanaji wa samaki hasa katika Ziwa Victoiria.
Mpango huo utawahusisha wadau
mbalimbali vikiwemo vyombo vya Ulinzi na Usalama, Wananchi, Wavuv,i Wenye
Viwanda na Viongozi katika ngazi mbalimbali za Serikali hasa kuanzia katika ngazi
ya Kitongoji, Kijiji na Kata ili kuhakikisha uvuvi haramu unakomeshwa mara moja
katika Mkoa wa Kagera.
Post a Comment