MRATIBU wa mfuko wa maendeleo ya jamii (TASAF) wilayani karagwe mkoani Kagera
Edius Rwangoga amesema kuwa walengwa wa kaya maskini watakao tumia fedha
hizo kwa ajili ya kuoa au kuongeza mke mwingine wataondolewa katika mfuko huo.
Hayo yalisemwa jana na mratibu wa
Tasaf Rwangoga wakati akizungumza na walengwa wa mpango wa kunusuru kaya
maskini kwa nyakati tofauti katika vijiji vya Rugu,Nyakasimbi Ihembe
Bisheshe na Kituntu.
Rwangoga alisema kuwa katika dirisha la
saba (7) la uhawilishaji fedha linaloendelea wilayani humo watabaini na
kuwachukulia hatua baadhi ya walengwa wa kaya maskini wanaotumia fedha hizo kwa
ajili ya kuoa na kuongeza wake wengine ikiwemo pia ulevi wa kupindukia kinyume
cha malengo wa mpango huo.
Alisema kuwa kuna baadhi ya walengwa
ambao wamegeuza mpango wa Tasaf kama chombo cha starehe na kusahau kuwa malengo
ya mpango huo ni kunusuru kaya maskini,kuboresha Lishe,Elimu na Afya.
Rwangoga alisema kuwa Tasaf imeweka
mkakati mwingine utakao wezesha walengwa wa mpango wa kunusuru kaya maskini
kuongeza kipato kwa kushiriki katika kazi za mikono hususani katika kipindi cha
hari kwa kuibua miradi yenye manufaa kwa jamii ikiwemo hifadhi ya
mazingira,umwagiliaji na barabara.
Naye mwalimu mkuu wa shule ya msingi
Rulalo kata ya Chonyonyo John Bitakwate alisema kuwa utekelezaji wa mpango huo
umeongeza idadi ya wanafunzi wanao hudhuria masomo hususani katika shule za
msingi kwenye maeneo ya walengwa wa mpango huo.
Alisema kabla ya mpango huo
maudhurio katika shule yake yalikuwa ni asilimia 35 na kuwa kwa sasa mahudhurio
na taaluma imepanda kwa asilimia 85 kutokana na wanafunzi kuwa na vitendea kazi
na sare za shule.
Kwa upande wake Frank Gimali mhudumu wa
afya kituo cha chochonyo kata ya chochonyo alisema moja ya mashariti yaliyomo
kwenye mpango huo ni kahakikisha kuwa watoto wanahudhuria masomo na kupata
huduma za matibabu kwenye zahanati au vituo vya afya vilivyopo kwenye maeneo
yao .
“Tumeshuhudua mahudhurio ya akina mama
wajawazito na watoto kwenye vituo vya afya na hospitali kwenye maeneo ya
walengwa yameongeza pia”Alisema Gimali.
Hata hivyo amewataka waratibu
wa Tasaf na wawezeshaji ngazi ya rika kutoa elimu mara kwa mara kwa walengwa wa
mfuko huo ili kuepusha matumizi mabaya ya fedha za Tasaf yanayofanywa na baadhi
ya walengwa wa kaya maskini.
Post a Comment