BAADHI ya wafanyabiashara wa maduka katika jengo
linalomilikiwa na umoja wa wanawake Tanzania (UWT) wilayani Karagwe mkoani
Kagera wameulalamikia umoja huo kufunga vyumba vyao bila kufuata utaratibu wa kisheria
na kuuathiri uchumi wao.
Hayo yalibainishwa jana na baadhi ya
wafanyabiashara hao katika mji mdogo wa Kayanga wilayani humo wakati zoezi la
kufunga maduka yao likifanyika kwa kuendeshwa na umoja huo kwa kusimamiwa na
jeshi la polisi kwa madai kuwa ni kutokana na wafanyabiashara hao
kutolipa kodi ya pango kwa kipindi kirefu.
Mmoja wa wafanyabiashara hao Grace Mahumbuka
ambaye pia ni mwenyekiti wa umoja wa wanawake wajane wilayani humo alisema kuwa
taratibu za kufunga maduka yao hazikufanyika kisheria zaidi kwani wenye maduka
hawakushirikishwa, mali zao hazikuhesabiwa wala hakuna mwenyekiti wa mtaa
aliyeshirikishwa.
“zoezi hilo lilifanyika kwa jaziba zaidi na
lililenga kutuathiri kiuchumi na zaidi zaidi ilikuwa ni kuwakomoa wale ambao
hawakukiunga mkono chama cha mapinduzi (CCM) kwenye uchaguzi mkuu mwaka jana”
alisema Mahumbuka.
Alisema kuwa baadhi yao wameathirika na
zoezi hilo kutokana na wafanyabiashara walioingia mkataba na (UWT) kuwatoza
hela za kodi na kutowalipa (UWT) suala ambalo limepelekea wao kufungiwa maduka
bila taarifa.
Aliongeza kuwa kwa kuwa kitendo hicho
wamekichukulia kama cha udhalilishaji kwao, kilicholenga kuwaathiri kiuchumi na
kisaikololojia wanajipanga kufungua kesi mahakamani kudai haki yao.
Kwa upande wake mwenyekiti wa (UWT) wilaya ya
Karagwe Rehema Mtawala alisema kuwa katika zoezi hilo wafanyabiashara saba ndio
walaliolipa shilingi milioni tano na kuruhusiwa kuendelea na biashara zao kila
mmoja ambapo deni lililobaki kwa wafanyabiashara wengine ni shilingi milioni 8.
Hata hivyo aliongeza kuwa umoja huo unatarajia
kuwafikisha mahakamani wafanyabiashara wengine ambao bado wamegoma kulipa fedha
hiyo kwani tayari walishapata notisi ya kuhama iliyotolewa na dalali wa
mahakama wilayani humo (court brocker) na kuwataka kutolichukulia suala hilo
kama la kisiasa.
Post a Comment