Waziri wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi awapangusa machozi wananchi wa Mkoa wa
Kagera waliokuwa wamedhurumiwa ardhi zao na walio kuwa na kero za ardhi za siku nyingi ambapo alisikiliza
kero hizo kwa umakini na kuzipatia ufumbuzi wa papo kwa hapo na kutoa haki kwa
waliostahili.
Akiwa Mkoani Kagera katika
ziara yake ya siku mbili Mhe. Lukuvi aliitumia siku yake ya kwanza ya tarehe 19/8/2016
kusikiliza, kupokea na kutatua kero mbalimbali za muda mrefu na zilizoshindikana kwa wananchi kuhusu ardhi ambapo kero nyingi alizisuluhisha
na kuzipatia ufumbuzi.
Aidha kwa wananchi
waliokuwawamejipatia ardhi kwa njia ya udanganyifu au kwa kuwatapeli wananchi
wenzao waliamuliwa kurejesha ardhi hizo kwa wamiliki halali wenye hati
zinazoonyesha mmiliki halali ni nani pia Halmashauri ya Manispaa iliamuliwa
kuwapatia viwanja wananchi ambao walichukuliwa viwanja vyao na kuhaidiwa kupatiwa
viwanja vingine ifikapo mwishoni mwa mwezi huu wa Agosti 2016.
Katika kutoa haki kwa wananchi
Mhe. Waziri Lukuvi alifuta umiliki wa ardhi ya Bw. George Rogers ambye alikuwa
Mtanzania lakini aliamua kuchukua uraia wa
nchi ya Uingereza ambaye alikuwa na mgogoro na wananchi wa kata ya Nyanga
katika Manispaa ya Bukoba.
Bw. Rogers raia wa Uingereza
alifutiwa umiliki wa ardhi aliyokuwa anaimiliki katika eneo la Kata ya Nyanga Manispaa
ya Bukoba kitalu namba 1(b) kilicho kuwa na ekari zaidi ya 1800, pia alifutiwa
umiliki wa eneo la Kibuye katika Manispaa ya Bukoba lenye vitalu 9 na kufutiwa
pia umiliki wa ekari 60 alizokuwa anazimiliki katika eneo la Bugolora Wilayani
Missenyi.
Akitangaza kufuta umiliki wa
maeneo yote hayo Mhe. Lukuvi Alisema kuwa Bw. Rogers na Kampuni yake ya Rockshild
Quality Food Products Ltd hawakufuata utaratibu wa umilikaji wa ardhi
bali yeye na Kampuni yake walijipatia ardhi hiyo kwa njia za udanganyifu kutoka
kwa wananchi.
Aidha Mhe. Lukuvi alisema
kuwa raia wa nchi za Kigeni hawaruhusiwi kuingia mitaani na kuanza kujinunulia
ardhi kwa wananchi bali wanatakiwa kupitia katika kituo cha uwekezaji (Tanzania
Ivestment Center) ambao wanayo dhamana ya kuwapatia wawekezaji au raia wa nchi
za nje sehemu au ardhi za kuwekeza mahala popote nchini.
Mbali na kutatua migogoro ya
mwananchi mmoja mmoja Mhe. Lukuvi alisema kuwa migogoro mikubwa kama ya
wafugaji na wakulima, mgogoro wa
wananchi wa Kakunyu Wilayani Missenyi na Ranchi za Taifa tayari unashughulikiwa
na Wizara nne ambazo ni Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,
TAMISEMI, Wizara ya Maliasili na Utalii na Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.
Katika hatua nyingine Mhe.
Lukuvi alisema kuwa ameamua kugawa majukumu ya wizara yake katika kanda ambapo
masuala yote yanayohusu ardhi hayaendi tena Dar es Saalam bali yanamaliziwa
katika kanda hizo na Mkoa wa Kagera upo katika Kanda ya Ziwa ambayo ipo jijini
Mwanza.
Mhe. Lukuvi kwenye ziara
yake Mkoani Kagera alifuatana na Kamishna Msaidizi wa Ardhi Kanda ya Ziwa Bw.
Joseph Shewiyo, Msajili Msaidizi wa Hati Kanda ya Ziwa Bi Magrgeareth Mziray,
na Msajili Msaidizi wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya Kanda ya Ziwa Bi
Dorothy Philip ambapo Wataalam hao wakishirikiana na Maafisa Ardhi wa Halmashauri
za Wilaya walimsaidia Mhe. Waziri Lukuvi kupata ufafanuzi wa kero mbalimbali na
kupata ufumbuzi wa keo hizo katika Mkutano na wananchi uliofanyika katika
viwanja vya Halmashauri ya Bukoba.
Post a Comment