Mkuu wa Mkoa Meja Jenerali
Mstaafu Salum M. Kijuu afanya ziara ya kukagua huduma za afya Mkoani Kagera na
kuzindua unyunyiziaji wa dawa ya kuua viluilui katika mazalia ya mbu ili
kupunguza tatizo la malaria mkoani hapa.
Ziara hiyo iliyoanza tarehe
12 Septemba, 2017 katika Halmashauri ya
Wilaya ya Bukoba Mhe. Kijuu alizindua ugawaji
wa vitambulisho vya kupata huduma ya afya kwa wazee ili watibiwe katika vituo
vya afya bure bila malipo yoyote.
Katika ziara hiyo Mkuu wa
Mkoa alilenga kukagua na kujihakikishia uwepo wa dawa katika vituo mbalimbali
vya afya kwa ajili ya kutoa huduma kwa wananchi. Pili alilenga kuhamasisha
wananchi kujikinga na kuchukua hatua za kupambana na ugonjwa wa Malaria ili
kupunguza maambukizi ya ugonjwa huo katika Mkoa wa Kagera.
Aidha, Mkuu wa Mkoa alilenga
kuhamasisha vituo vyote vya afya kutumia mfumo wa ukusanyaji mapato kwa njia ya
kielekitroniki ili kuongeza mapato yatayoboresha huduma kwa wananchi. Katika
ziara hiyo Mhe. Kijuu alijihakikishia kuwa dawa zipo za kutosha kwenye vituo na
kutoa rai kwa wananchi kufika katika vituo hivyo pindi wanapohisi wanaumwa ili
kupatiwa huduma za matibabu.
Katika ziara hiyo Mhe. Kijuu
aliwasistiza watendaji wa Halmashaui za Wilaya kuhakikisha wazee wanapatiwa
vitambulisho na kusema kuwa wazee hao wakati wa ujana wao walizalisha na
kulitumikia taifa kwa nguvu zao zote na sasa ni wakati wao kuhudumiwa hasa
kupatiwa huduma za afya bure bila kutozwa fedha zozote.
Aidha, Mhe. Kijuu
alimpongeza Rais John Pombe Magufuli ambaye naiongoza Serikali ya Awamu ya Tano
kwa kuwakumbuka wazee na kuwapatia vitambulisho ambavyo vitawaruhusu wazee wa
Tanzania kupatiwa huduma za afya bure bila malipo.
Katika Halmashauri ya
Manispaa ya Bukoba tayari wazee 900 wametambuliwa na kupewa vitambulisho,
Halmashauri ya Wilaya ya Missenyi tayari wazee 1500 wametambuliwa na
wanatarajiwa kupatiwa vitambulisho na Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba Zaidi ya
Wazee 200 tayari wamepatiwa vitambulisho vya kupatiwa huduma ya afya bure.
Agizo ni kuwa Halmashauri
zote zinatakiwa kuwatambua wazee na kuwapatia vitambulisho hivyo. Aidha Mhe.
Kijuu aliziagiza Halmashauri zote kuhakikisha zinanyunyizia dawa ya kuua
viluilui katika madimbwi, kandokando ya mito ili kuharibu mazalia ya mbu, pia
kuhakikisha Halmashauri zote zenye shehena ya dawa katika maghara ya dawa, dawa
hizo zisambazwe vituoni ili kutoa huduma
kwa wananchi.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa
Kagera Dk. Thomas Rutachunzibwa katika ziara hizo alitoa rai kwa watendaji wa Halmashauri kuona umuhimu wa kufunga mfumo
wa ukusanyaji mapato kwa njia ya kielekitroniki ili kuongeza mapato katika vituo
hivyo jambo ambalo litaboresha utoaji wa huduma za afya kwa wananchi na kuacha
utegemezi na vituo kujiendesha vyenyewe kwa makusanyo yao wenyewe.
Mkuu wa Mkoa Mhe. Kijuu
alitembelea vituo vya afya Rubale Wilayani Bukoba, Buyango na Bunazi Wilayani
Missenyi, pia na Kituo cha Afya Zamzam Manispaa ya Bukoba. Vilevile alitembelea
maeneo dawa ya kuua viluilui inakonyunyiziwa hasa katika madimbwi na maji
yaliyotuhama.
Post a Comment