Chama
cha wakulima wa miwa mkoani Kagera kimepongeza uamuzi wa Rais John Magufuli wa
kusitisha uingizaji wa sukari kutoka nje ili kulinda viwanda vya ndani.
Akizungumza na waandishi wa habari
wanaotembelea kiwanda cha sukari cha Kagera Sugar kilichopo wilayani Misenyi
mkoani Kagera , Mwenyekiti wa chama hicho mkoani Kagera, Dk. Frank Muganyizi
amesema uamuzi huo ni wa manufaa.
Dk. Muganyizi amesema uamuzi huo ni
wa manufaa sana katika kulinda viwanda vya sukari na pia kipato cha wakulima
ambao wametiwa moyo wa kuendelea kulima nchini.
Katika kulinda kipato cha wakulima,
mwenyekiti huyo alisema kuwa, viwanda vya ndani vimetoa ajira kwa wingi kwa
Watanzania na hivyo kuwezesha watu kuendesha maisha yao na familia zao kwa
urahisi zaidi.
Zuio hilo la kuingiza sukari
litawezesha wakulima wa miwa kupanua mashamba yao kwa kuwa watakuwa na uhakika
wa kuuza miwa yao kiwandani, alisema mwenyekiti huyo.
Aidha, amesema, zuio pia litakipa
kiwanda cha Kagera Sugar uwezo wa kuzalisha sukari kwa wingi na kuweza kuondoa
umasikini katika jamii.
Kiwanda cha sukari cha Kagera kimetoa
ajira kwa wananchi zaidi ya 6,000.
Akizungumzia kuongezeka kwa wakulima
wa miwa, mwenyekiti huyo amesema kuwa watu wengi waliokuwa wanalima kahawa
wameamua kulima miwa na kukiuzia kiwanda cha sukari cha Kagera.
Chama hicho kina wanachama 386 na
kina heka 4,189.
Kilimo cha miwa kimekuwa na
changamoto nyingi ikiwemo mabenki kushindwa kukopesha wakulima kiasi kikubwa
cha fedha
Aidha, Dk. Muganyizi amesema hata
wale wanaokopeshwa hupata fedha kidogo kutokana na riba kubwa ambayo ni
asilimia 18 kwa muda mfupi wa miaka miwili kurejesha mkopo huo.
Mwenyekiti huyo amesema kuwa heka
moja ya miwa ili kuianza kulima hugharimu kiasi cha shilingi milioni 2 kwa
kutoa visiki shambani na pia hadi kuvuna huchukua muda wa mwaka mmoja na miezi
saba.
Post a Comment