Wakuu wa Wilaya wateule saba wa Wilaya za Mkoa wa Kagera
wameapishwa rasmi leo Julai 4, 2016 na Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. Meja
Jenerali Mstaafu Salum M. Kijuu katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa
Kagera.
Wakuu hao saba wa Wilaya
waliapa mbele ya Mkuu wa Mkoa Mhe. Kijuu kwa kula viapo vitatu ambavyo ni Kiapo cha Utii, Kiapo cha Utumishi na Kiapo
cha kutunza siri za Serikali. Aidha, tayari wamekula Kiapo cha Maadili
mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Magufuli tarehe
29/06/2016 ikiwa ni pamoja na kupokea maelekezo ya utekelezaji wa shughuli zao.
Mara baada ya kula viapo
vyao Mkuu wa Mkoa Mhe. Kijuu aliwapongeza kwa kuteuliwa kuwa Wakuu wa Wilaya
wapya wa wilaya za Mkoa wa Kagera pia akawaasa kufanya kazi zao kwa kuzingatia
Kauli mbiu ya Mhe. Rais Magufuli ya “Hapa
Kazi tu”
“Nawaasa kuwatumikia
wananchi kwa nguvu sana kwani hali za wananchi katika maeneo yenu mliopangiwa
si nzuri, lakini nawataka kufanya kazi kwa kutenda haki bila kuwaonea na mtende kazi bila woga.” Aliwaasa Mhe.
Kijuu
Aidha Mhe. Kijuu aliwapongeza
wliokuwa wa Wilaya za Mkoa wa Kagera ambao wamestaafu na kuwatakia maisha mema
huko waendako pia aliwashukuru kwa kazi kubwa waliyoifanya wakiwa Wakuu wa Wilaya kwani
walipigana kwa nguvu kusukuma maendeleo ya wananchi mbele.
Wakuu
wa Wilaya saba Walioapishwa rasmi leo Julai 4, 2016
Mhe. Deodatus Lucas
Kinawilo Mkuu wa Wilaya ya Bukoba wa 19 tangu Wilaya hiyo kuanzishwa mwaka
1961.
Mhe. Godfrey Ayub Mheluka Mkuu wa Wilaya ya Karagwe wa 20 tangu Wilaya
hiyo kuanzishwa mwaka 1961.
Mhe. Lt.Col. Denis Filangali Mwila Mkuu wa Wilaya
ya Missenyi wa 4 tangu Wilaya hiyo kuanzishwa mwaka 2007.
Wengine
ni Mhe. Col. Mstaafu Shaban Ilangu Lissu Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa wa 3 tangu
Wilaya hiyo kuanzishwa mwaka 2012
. Mhe. Saada Ibrahim Malunde Mkuu wa Wilaya ya
Biharamulo wa 22 tangu Wilaya hiyo kuanzishwa mwaka 1961.
Mhe. Lt.Col. Michael
Mangwela Mntenjele Mkuu wa Wilaya ya Ngara wa 19 tangu Wilaya hiyo kuanzishwa
mwaka 1962.
Wa
mwisho ni Mhe. Mhandisi Richard Henry Ruyango Mkuu wa Wilaya ya Muleba wa 15
tangu Wilaya hiyo ilipoanzishwa mwaka 1975.
Aidha mara baada ya hafla fupi ya
kuapishwa Wakuu hao wa Wilaya waliondoka na kuelekea katika vituo vyao vya kazi
kuanza kutekeleza majukumu yao ya kazi.
Post a Comment