Waziri wa Sheria na Katiba,
Dkt Harrison Mwakyembe aliyasema hayo wakati akiongea na wadau mbalimbali
waliopo chini ya Wizara yake, Watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Waandishi
wa Habari, Wabunge, Wakuu wa Wilaya na
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. Salum M.
Kijuu katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa kagera alipowasili Mkoani Kagera leo tarehe
14/07/2016 na kuanza ziara yake ya kazi ya siku tatu.
Waziri Mwakyembe
aliyeongozana na Mkurugenzi wa Mashitaka nchini Bw. Biswalo Mganga na Kaimu
Mtendaji Mkuu wa RITA Bi Emmy K. Hadson alisema katika kikao hicho kuwa ziara
yake mkoani Kagera inalenga mambo makuu
matatu kama ifuatavyo;
Kwanza
ni
kufuatilia na kuhimiza utekelezaji wa
sheria iliyonzishwa mwaka 2011ambayo ilianzisha Tume ya Utumishi wa
Mahakama ambayo ndani yake ilianzisha Kamati za Maadili ya Mahakimu wa Mahakama
za mwanzo katika ngazi ya Wilaya na Kamati za Maadili ya Mahakimu Wakazi na
Mahakimu wa Wilaya katika ngazi ya Mkoa.
Katika kuhimiza utekelezaji
wa sheria hiyo Waziri Mwakyembe aliwaagiza Wakuu wa Wilaya kuunda Kamati hizo
ili kutatua kero za wananchi wanazopata kutoka Makimu wa Mahakama za Mwanzo
ambao wanajifanya miungu watu na kuwanyanyasa wananchi kwa kuwaomba rushwa na
kupindisha haki. Aidha alimwagiza Mkuu wa Mkoa naye kuunda kamati hiyo ya mkoa
ili kutatua kero za malalamiko kwa Mahakimu Wakazi na Makimu wa Wilaya.
Kamati hizo za Maadili
katika ngazi ya Wilaya wajumbe wake ni Mkuu wa Wilaya ambaye ni mwenyekiti wa
Kamati hiyo, Katibu Tawala wa Wilaya ni katibu wa kamati hiyo, Mkuu wa Wilaya
pia atateua kiongozi mmoja katika Wilaya husika na Mwananchi mmoja anayeheshimika
katika jamii nao watakuwa wajumbe wa kamati hiyo pamoja na Hakimu Mfawidhi wa
Wilaya naye ni Mjumbe.
Pili, Waziri
Mwakyembe alisema katika ziara yake Mkoani Kagera ni kuhimiza juu ya uchukuaji
na utunzaji wa takwimu za vizazi na vifo hasa kwa watoto wadogo. Waziri Mwakymbe alisema kwa nchi nzima ya
Tanzania uandikishaji wa takwimu za vizazi na vifo bado ni tatizo kubwa kwani katika
Tanzania watoto na watu wazima takwimu zinaonyesha kuwa wenye vyeti vya
kuzaliwa nia asilimia 11% tu.
“Tatizo lilionekana kuwa
kubwa baada ya Serikali kuamua kutoa elimu bure hapo ndipo ilionekana kuwa
mfumo wetu wa takwimu una matatizo makubwa kwani watoto walifumuka sana kiasi ambacho hapo
awali takwimu zilikuwa hazioneshi kuwa wtotot hao wapo katika jamii.”
Alisistiza Mhe. Mwakyembe.
Aidha Waziri Mwakyembe
aliushukuru uongozi wa Mkoa wa Kagera kwa kuvuka asilimia ya kitaifa kwa
uandikishaji wa vizazi na vifo kwani kwa
Mkoa ni asilimia 12% ambapo kitaifa ni asilimia 11% na Wilaya ya Bukoba
inaongoza kwa asilimia 45%, Wilaya ya mwisho ni Kyerwa ambayo kwasasa imeandikisha
asilimia 9.4%
Angalizo,
Waziri Mwakyembe pamoja na kuushukuru uongozi wa Mkoa na kumuomba Mkuu wa Mkoa na Wakuu wa Wilaya kuongeza
juhudi za uhamasishaji wa wananchi kuona umuhimu wa kuandikisha watoto wao
lakini alitoa angalizo kuwa Mkoa lazima kuwa makini sana katika uandikishaji
huo ili kudhibiti wahamiaji toka nje ya nchi kuandikishwa .
Tatu, Waziri
Mwakyembe alisema amekuja Mkoani Kagera kuona tatizo la mlundikano wa Wafungwa
na mahabusu Magerezani ambapo alisema
kuwa amekuwa akitembelea Magereza kila Mkoa alipofanya ziara ili kuona ukubwa wa
tatizo ni kiasi gani na kuona jinsi ya kutatua changamoto hiyo Wizara yake
ikishirikiana na Wizara ya Mambo ya Ndani.
Waziri Mwakyembe alisema
kuwa badala ya kuongea na raia juu ya tatizo la mlundikano wa wafungwa yeye
akishirikiana na Waziri wa Mambo ya Ndani waliamua waongee na wafungwa ili
kujua tatizo kwa undani na katika kuongea na wafungwa hao katika Magereza
mbalimbali nchini waligundua yafuatayo:
Ucheleweshwaji wa nakala za
hukumu za kesi, jamabo ambalo tayari Mahakama
tayari zimeanza kulishughulikia kwa kasi
kubwa, pili Kesi za watuhumiwa kukaa
muda mrefu bila kusikilizwa, nalo pia mahakama imeanza kulishughulikia, na Tatu
Watuhumiwa kubambikiziwa kesi tofauti na kesi zilizowapeleka Magereza. Waziri
Mwakembe alisema matatzo yote hayo sasa yanashughulikiwa kwa kasi kubwa sana na
Mahakama.
Aidha, katika hatua nyingine
Mhe. Mwakyembe alitembelea Ofisi ya Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini
(RITA) katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Bukoba na kumuagiza Kaimu Mtendaji
Mkuu kuhaikikisha anaiwezesha ofisi hiyo vifaa vya kisasa kama (Kompyuta) ili
kurahisisha utendaji kazi kwani Wilaya hiyo imepiga hatua kubwa katika
uandikishaji, vile vile aligawa vyeti vya kuzaliwa kwa wanaume watano na
wanawake watano.
Waziri Mwakyembe atakuwepo Mkoani
Kagera kwa siku tatu tarehe 14-16/07/2016 na anatarajia kutembelea Mahakama
kuu, Gereza la Mkoa Bukoba, Ofisi ya Mwanasheria
Mkuu wa Serikali, Gereza la Wilaya ya Muleba na Gereza la Wilaya ya Biharamulo
na kuhitimisha ziara yake Wilayani humo.
Post a Comment