Na: Sylvester Raphael
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa ameongoza mamia ya wananchi wa Mkoa
wa Kagera waliofurika uwanjani Kaitaba kuiaga miili ya wapendwa wao waliofariki
wakati mkoa huo ulipopatwa na janga la tetemeko la ardhi lililotokea Septemba
10, 2016 saa 9:00 alasiri na kusababisha vifo vya wananchi 16, kujeruhi 253 pia na kusababisha nyumba 840 kuanguka na
nyumba 1,264 kupata nyufa.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliwapa
pole wananchi wa Mkoa wa Kagera kwaniaba ya Serikali na kusema kuwa Serikali
inafanya juhudi zote za kutuma wataalam kuja Mkoani Kagera kuangalia kama
tetemeko la ardhi litarudia tena au dalili za lini linaweza kutokea tena ili
kutoa elimu kwa wananchi jinsi ya kujikinga na tetemeko hilo pindi linapotokea
tena.
Waziri Mkuu Kassimu Majaliwa
alisema tayari ofisi yake imetuma Wataalamu wa kitengo cha maafa ili kufika Mkoani
Kagera kufanya tathimini ya kina na ya haraka wakishirikiana na kamati ya maafa
ya mkoa ili kubaini ni sehemu gani zinazohitaji huduma au msaada wa haraka ambapo
janga la tetemeko limesababisha madhara makubwa.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. Kijuu akitoa taarifa jinsi
tetemeko hilo lilivyotokea na madhara yaliyosababishwa na tetemeko hilo
alimweleza Waziri Mkuu Kassim majaliwa kuwa tetemeko hilo lilitokea majira ya
saa 9:00 alasiri, aidha, tetemeko hilo lilikadiriwa kuwa na ukubwa 5.7 katika
vipimo vya Richter na lilisababisha madhara makubwa katika mkoa mzima.
Mhe. Kijuu alimweleza Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa kuwa tetemeko hilo lilisababisha vifo vya wananchi 16,
majeruhi waliolazwa katika Hospitali mbalimbali zilizoko kwenye mkoa wa Kagera
ni 170, Majeruhi waliotibiwa na kuruhiusiwa ni 83 na jumla ya majeruhi wote ni
253. Aidha nyumba za makazi zilizoanguka
ni 840, nyumba zilizopata nyufa ni 1,264 na majengo ya taasisi yaliyoripotiwa kuanguka ama
kupata nyufa ni 44.
Aidha, Mkuu wa Mkoa
alimweleza Mhe, Majaliwa kuwa mara baada ya tetemeko hilo kutokea uongozi wa mkoa
ulichukua hatua za haraka kwa kuokoa wananchi na kuwapeleka hospitali
mbalimbali kwa ajili ya matibabu. Pili, baadhi ya wananchi wenye nyumaba
zilizoathirika walipatiwa makazi ya muda na kuwahamasisha kusaidiana wao kwa
wao kupeana hifadhi. Mwisho Mkoa
unaendelea na tathimini ya athari na hasara zilizosababishwa na tetemeko hilo.
Agizo
la Waziri Mkuu, Mkoa chini ya Mwenyekiti wa kamati ya Maafa
ya mkoa ambaye ni Mkuu wa Mkoa pia na Maafisa kutoka kitengo cha Maafa Ofisi ya
Waziri Mkuu waendelee kufanya tathmini
ya kina ya kubaini athari na hasara za tetemeko hasa kwa kuanza na sehemu
zinazohitaji huduma ya haraka kama shule mbili za Sekondari za Ihungo na
Nyakato ili Serikali iweze kusaidia mara baada ya kupata tathimini ya hali halisi
ya maafa.
Katika hatua nyingine Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa mara baada ya kuwasiili Mkoani Kagera majira ya saa 7:00
mchana aliwatembelea majeruhi waliojeruhiwa wakati wa tetemeko hilo ambao bado
wamelazwa katika Haspitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera, pia alitembelea shule za
Sekondari za Nyakato na Ihungo ambako madhara yalitokea makubwa na kupelekea
wanafunzi kukosa sehemu za kulala baada ya mabweni yao kubomolewa na tetemeko.
Vile vile Mhe Majaliwa alishuhudia maiti 14 na kutoa heshima zake za
mwisho kwa marehemu katika uwanja wa Kaitaba ambapo marehemu hao waliombewa dua na sala kutoka kwa viongozi wa
dini Mkoani Kagera . Pia Mhe. Majaliwa aliwapa pole wafiwa na kuzungumza na
wananchi waliokusanyika uwanjani hapo kwa kuwapa salaam za Serikali.
Post a Comment