Na: Sylvester Raphael
Ujenzi
wa Chuo cha kisasa cha Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) Kagera wakaribia kuanza
katika eneo la Burugo Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba nje kidogo ya Manispaa ya
Bukoba ili kutoa Elimu au Mafunzo ya Ufundi Stadi kwa vijana wengi wanaohitimu
elimu ya Msingi na Sekondari kutoka ndani na nje ya mkoa.
Chuo cha Mafunzo ya Ufundi
Stadi (VETA) Kagera kinatarajiwa kujengwa kwa ufadhili wa Serikali ya China,
aidha, Serikali hiyo imetuma wataalam wa
sekta mbalimbali za ujenzi na tayari wamewasili mkoani Kagera kuanzia Septemba 7, 2016 ili kufanya upembuzi
yakinifu wa gharama za ujenzi wa chuo katika eneo kitakapojengwa.
Wataalamu hao wanane kutoka
nchini China waliwasili mapema asubuhi katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa kumsalimia
na kujitambulisha ambapo kati yao kuna Mhandisi wa masuala ya Maji, Ujenzi, na
Umeme ambao kwa mujibu wa kiongozi wao watafanya upembuzi yakinifu wa gharama
za ujenzi, katika eneo husika, mfano kuona eneo kama linafaa, upatikanaji wa
vifaa, gharama za vifaa na masuala yote yanayohusu ujenzi.
Mara baada yakuwapokea
ofisini kwake Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Mstaafu Salum M. Kijuu aliwaeleza
kuwa Serikali ya Mkoa ipo tayari kutoa ushirikiano kwao ili ujenzi wa chuo
hicho uanze mara moja . Pia liwakaribisha mkoani Kagera pamoja na kuja kufanya
upembuzi yakinifu lakini watembelee mkoa na kuona Kagera ilivyobarikiwa katika fursa
mbalimali za utalii na kiuchumi.
Chuo cha Kisasa cha Mafunzo
ya ufundi stadi (VETA) Kagera kinatarajiwa kujengwa na kuwa chuo cha mfano wa
vyuo vya ufundi nchini ambapo kitadahili wanafunzi wengi na kitakuwa na fani
mbalimbali za ufundi stadi ambazo zitakuwa zinaendana na hali halisi ya sasa ya
Sayansi na Technolojia .
Mkoa wa Kagera tangu
mwaka1987 hadi sasa hauna chuo cha (Vocational Educational and Training
Authority, VETA) cha ufundi isipokuwa kuna
Kituo cha mafunzo ya ufundi (Vocational Training Center) VTC Rwamishenye
ambacho ni kimojawapo kati ya vituo 27 vinavyomilikiwa na VETA chini ya Wizara
ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi nchini.
Kutokana na VTC kagera
kutokuwa na uwezo wa kudahili wanafunzi wengi aidha, kuwa kituo cha mafunzo
kisichokuwa na wanafunzi wa kulala (bweni) na kupelekea wanafunzi ambao ni wa nje
ya Manispaa ya Bukoba kukosa elimu ya ufundi na kuishia mitaani baada ya
kumaliza elimu ya msingi na sekondari ndiyo sababu Serikali ya Tanzania iliamua
kujenga chuo cha kisasa Kagera ili kupunguza tatizo hilo.
Ni baada ya Serikali ya
Awamu ya Nne chini ya aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Kikwete kuamua kujenga Chuo cha Kisasa
cha Ufundi, Rais Kikwete aliiomba nchi
rafiki ya China kujenga chuo hicho na kupendekeza kijengwa mkoani Kagera.
Aidha Rais Kikwete alitangza uamuzi wa Serikali ya
China kukubali kujenga chuo hicho cha Ufundi Stadi Mkoani Kagera Wakati
akiongea na wazee wa Mkoa wa Dodoma katika Ukumbi wa Kilimani tarehe 04/11/2014
na kuipongeza Serikali ya China kwa kukubali ombi lake kwa dhati.
Wananchi wa Mkoa wa Kagera hatuna budi kuupokea mradi wa
ujenzi wa chuo hicho kikubwa cha kisasa na kitakachotoa elimu ya ufundi wa
kisasa unaoendana na sayansi na teknolojia , pia na kutoa ajira kwa wananchi wa
mkoa wetu wakati wa ujenzi na mara baada ya kumalizika kujengwa kwa chuo hicho.
Post a Comment