Umoja
wa Mataifa kupitia Mkurugenzi wake Mkazi nchini Tanzania Bw. Alvaro Rodriguez
umetembelea, kukagua na kuridhishwa na utekelezaji
wa miradi inayofadhiliwa na umoja huo Mkoani Kagera ambapo zaidi ya Dola za
Kimarekani (618,000 USD) zimetolewa ili kufadhili na kutekeleza miradi
mbalimbali ya maendeleo kama Elimu na Afya pia na miradi ya kijamii.
Bw.
Alvaro Rodriguez ambaye ni Mwakilishi Mkazi wa Mashirika matatu ya Umoja wa
Maifa nchini Tanzania (IOM, UNICEF na UNDP) aliwasili Mkoani Kagera Machi 13,
2017 na ujumbe wake ili kutembelea na kukagua miradi ya Maendeleo na Kijamii
inayofadhiliwa na Umoja huo katika maeneo mbalimbali mkoani hapa.
Miradi
aliyoitembelea Bw. Rodriguez ni pamoja na mradi wa ujenzi wa vyoo, madarasa, mabweni na jengo la utawala katika shule ya
Msingi Mgeza Mseto Manispaa ya Bukoba ambapo mara baada ya kukamilika mradi utagharimu
Dola za Kimarekani (318,000 USD) ambapo ujenzi wa vyoo umekamilika, madarasa mabweni
na jengo la Utawala ujenzi upo katika hatua ya msingi.
Bw.
Rodriguez akiongea na wanafunzi, walimu na wananchi waliofika kumpokea katika
shule hiyo alisema kuwa amefurahishwa kufika katika shule hiyo na kujionea hali
halisi ya watoto wenye ulemavu wa albinizimu na walemavu wengine aidha, alisema
kuwa Umoja wa Mataifa uliamua kutoa fedha hizo ili kurejesha miundombinu ya shule
hiyo baada ya kuharibiwa na Tetemeko la Ardhi lilitokea Septemba 10, 2016.
“Nilipokuwa
Dar es Salaam niliambiwa na Waziri Profesa Joyce Ndalichako kuwa nikifika
Kagera nitembelee Shule ya Msingi Mugeza Mseto pia nilipofika Kagera Mkuu wa
Mkoa ameniambia nitembelee shule hii sasa nimejionea na kujua ni kwanini
walinisistiza, shule inahitaji msaada mkubwa. Aidha, Umoja wa Mataifa unapenda
kusaidia lakini Tanzania shule za namna
hii zipo nyingi na ndiyo maana tunasaidia kidogo kidogo ili kuongeza mahitaji
muhimu.” Alisistiza Bw. Rodriguez
Pai Bw.
Rodriguez alisema kuwa mara baada ya kujionea hali halisi ya shule hiyo
ataendelea kushawishi wafadhili mbalimbali ili kuhakikisha shule hiyo yenye
mahitaji maalum inapewa kipaumbele katika ufadhili. Vilevile aliiomba jamii
kutowanyanyapaa watoto wenye ulemavu kwani ulemavu hauna ukabila, utaifa wala
rangi ambapo alisema kuwa hata yeye watoto wake ni walemavu jambo ambalo
alisema ulemavu hauna mzungu wala mweusi.
Umoja
wa Maifa pia umetoa ufadhili dola za Kimarekani (250,000 USD) kwenye shule za
Msingi 16 Katika Halmashauri ya Manispaa na Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba ili
kujenga vyoo na kuimarisha mifumo ya maji kwa ajili ya uboreshaji wa usafi na
mazingira. Pia kukarabati miundombinu yote iliyoharibiwa na Tetemeko la Ardhi
lililotokea mwaka jana 2016.
Aidha,
Umoja wa mataifa kupitia Shirika lake la (UNICEF) ulitoa ufadhili wa kujenga
majiko sanifu katika jamii kwaajili ya kutunza mazingira kwa wananchi wa hali
ya chini kwa kutumia nishati ya kuni kidogo. Pia kupitia shirika la (IOM)
wananchi na kaya masikini waliokumbwa na Tetemeko la Ardhi mwaka 2016 waligawiwa vifaa
mbalimbali kama ndoo, magodoro, blanketi,
bati, vyandarua na vifaa vya kujengea makazi ya muda katika Halmashauri za
Bukoba Manispaa, Bukoba na Missenyi.
Katika
Hatua nyingine Bw. Rodriguez alikagua mradi uliofadhiliwa na Umoja wa Mataifa
wa kufunga umeme wa jua katika Zahanati ya Bushasha Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba
na Shule ya St. Mary Rubya Seminari Wilayani Muleba. Katika Shule ya Rubya
Seminari ufungaji wa umeme wa jua uligharimu Dola za Kimarekani (50,000 USD)
hadi kukamilika.
Akitoa
maelezo ya Mradi huo Padre Malianus Rutagwerela ambaye ndiye Mkuu wa Seminari
hiyo alisema kuwa mradi huo umeongeza nguvu ya mwanga katika shule hiyo na kuwa
na umeme wa uhakika ikiwa ni pamoja na umeme wa TANESCO. Aidha aliushukuru
umoja wa Mataifa kwa niaba ya uongozi wa Jimbo Katoliki la Bukoba kuwa mradi
huo utaboresha zaidi elimu katika Seminari hiyo.
Naye
Mkurugenzi Mkazi Bw. Rodriguez alifurahishwa sana na mradi huo ambao
alishuhudia ukifanya kazi vizuri. “ Nimefurahishwa na mradi huu pia sisi kama Umoja
wa Mataifa tutaendelea kuona jinsi ya kusaidia shule kama hizi ili Mapadre na
Viongozi wa dini waendelee kuzalishwa katika shule kama hizi ili wasaidie
kueneza neno la Mungu kuhusu upendo na kuondoa chuki kati ya Wanadamu. Alieleza
Bw. Rodriguez
Mwisho,
Bw. Rodriguez alisema kuwa amefurahishwa na utekelezaji wa miradi ambayo ipo
chini ya Mashirika ya Umoja wa Maifa ambayo imetolewa ufadhili wa fedha na Umoja
huo na kutekelezwa au inaendelea kutekelezwa Mkoani Kagera. Aidha, alihaidi kuendelea kuushawishi Umoja huo na
wafahili mbalimbali ili waendelee kuuangalia na kuufadhili Mkoa wa Kagera
katika miradi mbalimbali ya maendeleao na Kijamii.
Post a Comment