Baraza la Madiwani katika
Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba Mkoani
Kagera limewasimamisha kazi Watendaji sita wa Halmashauri kupisha uchunguzi wa
upotevu na ubadhirifu wa milioni 851 za mfuko wa barabara, Mfuko wa Afya, na
Mfuko wa Jimbo zilizotumika bila kufuata utaratibu na kanuni za wa fedha.
Watendaji hao sita
waliosimamishwa katika kikao cha Baraza la Madiwani cha tarehe 28.01.2016
walihusika na ubadhilifu wa fedha hizo kwa kuzitumia bila kufuata kanuni,
taratibu na sheria za kuomba idhini ya kuhamisha vifungu vya fedha au
kubadilisha matumizi yake kutoka fungu moja kwenda fungu lingine.
Hayo yalibainishwa na Kamati
ya Wataalamu sita iliyoundwa na Mkuu wa Mkoa Mhe. Mongella katika kikao cha Bodi ya Barabara
kilichofanyika tarehe 21.01.2016 Mkoani Kagera na kuiagiza Kamati hiyo
kuchunguza upotevu wa fedha hizo mara baada ya Mhandisi wa Halmashauri hiyo
kuwasilisha taarifa ya matengenezo ya barabara na madaraja kwa mwaka wa fedha
2014/2015.
Kamati hiyo ya wajumbe sita
iliyoongozwa na Katibu Tawala Msaidizi Miundombinu Sekretarieti ya Mkoa wa
Kagera Bw. Sabora Wambura na ilipewa siku tano iwe imekamilisha taarifa yake.
Aidha, taarifa ya Kamati hiyo iliwasilishwa mbele ya Mkuu wa Mkoa, Baraza la
Madiwani, Watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba, Kamati ya Ulinzi na
Usalaama ya Mkoa na Wilaya tarehe 27.01.2016.
Katika kikao hicho cha
kupokea taarifa ya ubadhirifu wa shilingi milioni 851, Watendaji waliohusika
walihojiwa mara baada ya taarifa kuwasilishwa na kuonekana walitumia fedha hizo
kinyume na utaratibu wa fedha, katika mahojiano hayo walikiri kuwa utaratibu wa
fedha haukufuatwa na kukiri makosa yao.
Mkuu wa Mkoa Mhe. Mongella mara
baada ya kuwahoji alikubaliana na Baraza la Madiwani kuwa watendaji hao
wanatakiwa kuwajibishwa na kuliagiza Baraza hilo kukaa kikao na kuamua hatua ya
kuchukua kwa wahusika wote kwani mamlaka ya kuwawajibisha Wakuu wa Idara wa halmashauri
ipo kwa Madiwani wenyewe.
Aidha, alimwagiza Katibu Tawala
Mkoa kumwadikia barua Katibu Mkuu
TAMISEMI ili aweze kumchukulia hatua Mkurugenzi Mtendaji Bi Gradis Dyamvunye
aliyekuwepo wakati huo na kuomba aliyekuwa Mhandisi wa Ujenzi wa Halmashauri
hiyo Robert Massoro kurudishwa kujibu tuhuma za matumizi mabaya ya fedha za
mfuko wa barabara pia kuomba ufanyike ukaguzi maalum mara moaja.
Kikao cha Baraza la Madiwani
kilichofanyika tarehe 28.01.2016 kikiongozwa na Mwenyekiti wake Mustapha Ngeze
kiliamua kwa kauli moja kuwasimamisha kazi kupisha uchunguzi wa upotevu wa
milioni 851 watendaji wafuatao;
Idara ya fedha ni Bw.
Jonathan Katunzi (Mweka Hazina), Selialisi Mutalemwa, Idara ya Ujenzi, Bw. Deus
Bizibu, Elimu Sekondari ni Bw. Lucas Mzungu, Mifugo ni Dk. Kisanga Makigo na
Bw.Mustapha Sabuni Afisa Mipango.
Mchanganuo wa fedha
zilizotumika blia kufuata utaratibu na kanuni za fedha ni Shilingi milioni 200 za mfuko maalum wa
barabara zilizokuwa zimeletwa kwa ajili ya kujenga daraja la Kyamabale, Milioni
176 za mfuko wa barabara kwa ajili ya kutengeneza na kukarabati barabara, Milioni
168 za mfuko wa Jimbo, na Milioni 307 za mfuko wa Afya (Busket Fund)
Post a Comment