Bila kujali itikadi za vyama vyao, wabunge wameukosoa mwongozo wa kuandaa mpango wa Bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha wa 2016/17, wakihoji suala la ujenzi wa reli ya kati kwa viwango vya kimataifa pamoja na mambo mbalimbali.
Pia,
wamepinga mpango wa Serikali wa kutaka mapato yote ya halmashauri,
taasisi na mashirika ya umma kuwekwa kwenye mfuko mkuu wa Serikali na
kuitaka itafute vyanzo vipya vya mapato.
Katika
kuonyesha msimamo wa pamoja, wabunge wote wanaotokea mikoa ambayo Reli
ya Kati inapita wameunda umoja kuhakikisha Serikali katika mpango wake
wa bajeti ya 2016/17, inakuja na mwelekeo wa ujenzi wa reli ili nchi
ipate maendeleo ya kweli, si ya kwenye makabrasha.
Umoja
huo uko chini ya uenyekiti wa Ezekiel Maige, mbunge wa Msalala (CCM),
wakati Zitto Kabwe, ambaye ni mbunge wa Kigoma Mjini (ACT Wazalendo),
anakuwa katibu wa wabunge hao walio katika mikoa inayoanzia Dar es
Salaam kupitia Tabora hadi Mwanza na kutokea Tabora hadi Kigoma.
Mikoa mingine inayounganishwa na reli hiyo kongwe ni Shinyanga, Morogoro na Dodoma.
Akichangia mjadala kuhusu mwongozo huo, Zitto alitahadharisha dhidi ya siasa za kikanda.
“Tunapaswa
kuwa makini sana kwenye siasa za kikanda. Tusikubali maslahi ya nchi
nyingine yafunike maslahi ya nchi yetu. Ni lazima tuhakikishe mtandao wa
reli ambao utaisaidia nchi yetu,” alisema kiongozi huyo wa chama cha ACT-Wazalendo.
“Juzi
nilisikia kwamba tuna tatizo la fedha. Mwaka jana Bunge lilipitisha
sheria ya Kodi ya Maendeleo ya Reli ambayo inataka kila mzigo unaoingia
nchini, utozwe asilimia 1.5 kwa ajili ya reli. Tunacho chanzo cha
uhakika cha fedha na tunachopaswa kufanya ni kuhakikisha kwamba chanzo
hiki kinatumika kwa madhumuni yaliyokusudiwa.
“Tupewe
tafsiri ya Reli ya Kati. Kwetu sisi Reli ya Kati ni ile inayotoka Dar
es Salaam, Tabora, Uvinza (kwenda msongati Burundi). Kutoka Kaliua
kwenda Mpanda mpaka Kalema kwa ajili ya ujenzi wa Bandari ya Kalema.
Kutoka Isaka kwenda Keza Ngara kwa ajili ya madini ya Nikel
yaliyogundulika huko ili kusafirishwa kwenda Dar es Salaam.”
Mvutano
kuhusu reli ulianza tangu wiki iliyopita katika mjadala wa hotuba ya
Rais John Magufuli wakati mbunge wa Nzega Mjini (CCM), Hussein Bashe
aliposema atawashawishi wenzake kuigomea bajeti ya 2016/17, iwapo
Serikali haitatoa mwelekeo wa ujenzi wa reli hiyo ya kati.
Kuhusu
Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), Zitto alisema badala ya Serikali
kukimbilia kununua ndege mbili, inapaswa kulifanyia shirika hilo
marekebisho kwa kuzifanya taasisi za utalii kuwa na hisa ATCL.
“Kutokana
na wingi wa watalii wanaoingia nchini, Tanapa na Ngorongoro wanapata
mapato. Turuhusu wawe na hisa ATCL ili shirika hili lijiendeshe
kibiashara,” alisema Zitto.
Mbunge
wa Kigoma Kaskazini (CCM), Peter Serukamba aliungana na Zitto kumtaka
Waziri wa Fedha, Dk Philip Mpango aeleze Reli ya Kati itajengwa kuanzia
wapi kwenda wapi wakati atakapokuwa akiwasilisha mpango huo.
Alisema bila kuwa na reli ya uhakika ni ndoto nchi kupata maendeleo inayoyatarajia.
Serukamba
alisema kuna taasisi zilizoanzishwa kwa sheria hivyo kuzitaka zianze
kupeleka fedha katika mfuko mkuu wa Serikali, italazimika sheria
kubadilishwa.
Mbunge huyo alihusisha suala hilo na uvivu wa watendaji wa hazina kutopenda kufikiria vyanzo vipya vya mapato.
“Mtazifanya
halmashauri zishindwe kujiendesha jamani mbona hamfikirii suala hili.
Waziri hii kitu si sawa kabisa iondoeni,” alisema.
“Viwango
vya kodi mnavyoviweka ni vikubwa sana. Hivi (Mamlaka ya Mapato) TRA
haijifunzi kwa nchi kama Mauritius ambayo viwango vyake vya kodi ni
vidogo lakini inakusanya fedha nyingi?” alihoji.
Naye mbunge wa Kigamboni (CCM), Dk Faustine Ndugulile alisisitiza umuhimu wa kuwa na reli.
“Tukitaka kupaisha uchumi, lazima tuwe na Reli ya Kati ya kiwango cha kisasa. Ni lazima serikali mje na mpango wa kueleweka,” alisema akizungumzia reli hiyo ambayo ujenzi wake ulianza mwaka 1905 wakati nchi ikiwa chini ya wakoloni wa Kijerumani.
Mbunge
wa viti maalum (CCM), Mwanne Nchemba alisema suala la reli ya kati si
la mzaha kwa maelezo kuwa wapigakura wengi wanaitegemea reli hiyo, pia
ni njia nzuri ya kusafirisha mizigo, hivyo lazima Serikali ihakikishe
inaijenga kwa kiwango cha kisasa.
Kwa
upande wake mbunge wa Kasulu Mjini (CCM), Daniel Nsanzugwako alisema
sera ya uchumi wa viwanda ya Serikali ya Awamu ya Tano haiwezi
kufanikiwa vyema bila nchi kuwa na reli ya uhakika.
“Mizigo
lazima ipite katika reli ili kuokoa barabara zetu. Msipokuja na mkakati
hatutawaelewa katika bunge hili. Haiwezekani miaka 20 sasa
tunazungumzie reli tu,” alisema huku akisisitiza kuwa uwepo wa reli utaongeza kasi ya mapato bandarini.
Mbunge
wa Babati Mjini (Chadema), Pauline Gekul naye aliungana na Serukamba
kuhoji uamuzi huo wa Serikali kuweka fedha zote za mapato kwenye mfuko
wa Serikali, akisema utaua halmashauri.
“Tukumbuke
historia ya ugatuaji wa madaraka, kumbukeni jinsi Mwalimu
(Julius)Nyerere alivyourudisha baada ya kuona faida zake. Serikali za
mitaa zina mamlaka ya kukusanya mapato na kutumia, sasa hayo mamlaka
mnayaondoa mnategemea nini,” alisema.
“Mkipitisha
suala hili, haya mapato hayatakusanywa ipasavyo na pia mtatengeneza
mianya mingine ya ajabu ajabu.Tumekuwa tukiona jinsi ambavyo Serikali
inashindwa kutoa fedha za maendeleo, sasa mnapotaka fedha zote zipelekwe
katika mfuko mkuu wa Serikali, je zitatoka zote wakati
zitakapohitajika?” alihoji.
Gekul alisema kama tatizo ni sheria za halmashauri na taasisi, ni vyema zinakabadilishwa ila si kuziondolea mapato.
Mbunge
wa Nsimbo (CCM), Richard Mbogo alizungumzia Shirika la Ndege (ATCL)
akitaka lipunguze wafanyakazi wake ili kuweza kujiendesha kibiashara.
Alisema kwa sasa shirika hilo linasuasua kutokana na kutokuwa na mapato ya kutosha.
Post a Comment