Karagwe forum Karagwe forum Author
Title: CHIMBUKO LA KARAGWE NA WATU WAKE.
Author: Karagwe forum
Rating 5 of 5 Des:
Chimbuko la Karagwe na watu wake. J ina "Karagwe"kutokana na simulizi za wazee wetu mbali mbali na watafiti wa Historia ka...

Chimbuko la Karagwe na watu wake.

Jina "Karagwe"kutokana na simulizi za wazee wetu mbali mbali na watafiti wa Historia kama(professor Katoke 1975,162) inaelezwa na kuthibitisha kwamba jina hili linatokana na kilima kinachopatikana kusini magharibi ya Karagwe,katika kijiji cha Kandegesho,kata ya Nyakakika ambacho mtawala (Omukama ) wa kwanza alipofanyia kafara yake ya kwanza ambapo wenyeji na wazee wetu wanaamini alikuwa Nono Malija kutoka ukoo wa Basiita.

Na kwamba kumbukumbu hii ya "Karagwe Ka Nono" inatokana na ukweli kuwa Nono alikuwa mtawala wa mwisho wa wenyeji asilia kabla ya kuondolewa madarakani na Omukama Ruhinda mtoto wa Wamara kwa ujanja.Na hii ndiyo kumbukumbu yake ya chimbuko na historia ya jina Karagwe.


Cory(1949;18) anaeleza"Ruhinda alipofika Karagwe kutoka kusini alimkuta mtawala mwenyeji aliyekuwa akiitwa Nono Malija wa ukoo wa Basiita.Nono hakushindwa katika vita bali alidanganywa na ujanja wa Ruhinda".Tafiti hii inashabihiana na simulizi nyingi za wazee wa Karagwe na nchi jirani kuwa Wasiita kutokana na njaa kali iliyokuwepo wakati huo waliuza ngoma ya utawala Wahinda/Ruhinda na kupewa ulezi kwa ajili ya chakula na kuanzia wakati huo wakawa chini ya utawala wa Abahinda/Ruhinda. Ruhinda alijenga boma lake katika eneo la Bwehange nchi iliyo kusini ya ziwa lililoitwa "Wndemere" na baadaye kuhamia Bweranyange,mahali palipo karibu na uwanda wa juu penye mteremko wa vilima vinavyozunguka ziwa.Hapa ndipo watawala wote walipotawalishwa hadi walipofika Wadachi.


Taarifa za utafiti huu unashabihiana sana kwa karibu sana na bwana Halley katika kitabu chake cha "An African survey" ukurasa wa 23/24"kaskazini magharibi ya ziwa Victoria" watu wa makabila ya Waganda,wanyankole,watoro,wanyoro,na makabila manane ya wilaya ya Bukoba katika Tanganyika na Ruanda (Nchi ya udhamini wa Ubeligiji) ni mchanganyiko wa makabila ya wenyeji wakulima wabantu na makabila ya wafugaji waKihima toka kaskazini ambayo yanasadikiwa yalizishambulia nchi hizo zama za miaka mia tatu iliyopita na kuwashinda wenyeji wake.Katika falme hizi wafugaji wa ng'ombe waitwao Wahima mpaka sasa ni jamaa wa watawala"


Lakini pamoja na kuondolewa kwa utawala huu mwishoni mwa karne ya 15 na mwanzoni mwa karne ya 16 bado itakumbukwa kwa jinsi utawala huu wa Nono Son of malija ulivyokuwa umefanikiwa kuwa na utaratibu mzuri wa kuchagua kiongozi wa Karagwe nzima, kuanzisha wazo la utawala wa kitemi (Kingship).Nchi nzima ya karagwe walimtegemea Omukama kwa ushauri na ulinzi.Alitoa maelekezo katika masuala yote muhimu kuhusu nchi yake.


kuanzishwa kwa umoja wa Karagwe na utawala (Kingship) uliwezekana kwa wakati huo kutokana na mambo mawili makuu ambayo ni:(1) Kuongezeka kwa idadi ya watu kutokana na mapinduzi ya kilimo na (2)Ongezeko la wahamiaji kutoka Bumyoro ambapo walikuwa wanalazimika kukimbia mapigano na uvamizi wa watu kutoka kaskazini.


Kutokana na ukweli kwamba wanyambo asilia walikuwa na utawala wao(Kingship) uliokuwa unaendelea karagwe an nchi jirani zake,hatuwezi kusema kuwa Buhinda ndiyo waliowajibika kuleta taasisi hii kama Cory na watafiti wengine wanavyoeleza.


Kuwepo kwa mchanganyiko wa  makabila mbali mbali katika karagwe unaanzia katika karne ya 18 ambapo Stanley (1876) anaripoti kuwa "In Karagwe there were Wanyambo,Wanyarwanda, Wasuwi,wanyamwezi,Arabs,and Swahili at the court of Rumanyika.


Taarifa hii inatuonyesha kuwa aragwe toka zamani hadi leo ilikuwa na mwingiliano wa makabila mbali mbali ambazo ziliingia Karagwe kutokana na sababu mbali mbali kama ukame,njaa,matatizo ya kiuchumi na kisiasa,na wakati mwingine mapigano ya koo za kikabila yamesababisha watu wengi kuhamia Karagwe.Hivyo,Karagwe kwa sasa pamoja na wenyeji (Wanyambo) wanaishi watu toka kabila mbali mbali ndani ya nchi na wengine toka nchi jirani za Rwanda,Burundi,Uganda,n.k.


Leo hii ukitembelea kijiji cha Kafulo katika kata ya Nyabiyonza utaona mwembe mkubwa uliopandwa na kuachwa na Waarabu walifika katika karne ya 18 kwa ajili ya biashara.

About Author

Advertisement

Post a Comment

 

This Template Is Designed By Jacksay | call 0764 031 242 for this service

Top