Karagwe forum Karagwe forum Author
Title: WAZIRI MWAKYEMBE AAGIZA KAMATI ZA MAADILI YA MAHAKIMU KUANZISHWA MARA MOJA MKOANI KAGERA ILI KUTATUA KERO ZA WANANCHI
Author: Karagwe forum
Rating 5 of 5 Des:
Waziri wa Sheria na Katiba, Dkt Harrison Mwakyembe aliyasema hayo wakati akiongea na wadau mbalimbali waliopo chini ya Wizara...






Waziri wa Sheria na Katiba, Dkt Harrison Mwakyembe aliyasema hayo wakati akiongea na wadau mbalimbali waliopo chini ya Wizara yake, Watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Waandishi wa  Habari, Wabunge, Wakuu wa Wilaya na Mkuu wa Mkoa wa Kagera  Mhe. Salum M. Kijuu katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa kagera  alipowasili Mkoani Kagera leo tarehe 14/07/2016 na kuanza ziara yake ya kazi ya siku tatu.



 

Waziri Mwakyembe aliyeongozana na Mkurugenzi wa Mashitaka nchini Bw. Biswalo Mganga na Kaimu Mtendaji Mkuu wa RITA Bi Emmy K. Hadson alisema katika kikao hicho kuwa ziara yake mkoani Kagera  inalenga mambo makuu matatu  kama ifuatavyo;





Kwanza ni kufuatilia na kuhimiza utekelezaji wa  sheria iliyonzishwa mwaka 2011ambayo ilianzisha Tume ya Utumishi wa Mahakama ambayo ndani yake ilianzisha Kamati za Maadili ya Mahakimu wa Mahakama za mwanzo katika ngazi ya Wilaya na Kamati za Maadili ya Mahakimu Wakazi na Mahakimu wa Wilaya  katika ngazi ya Mkoa.


Katika kuhimiza utekelezaji wa sheria hiyo Waziri Mwakyembe aliwaagiza Wakuu wa Wilaya kuunda Kamati hizo ili kutatua kero za wananchi wanazopata kutoka Makimu wa Mahakama za Mwanzo ambao wanajifanya miungu watu na kuwanyanyasa wananchi kwa kuwaomba rushwa na kupindisha haki. Aidha alimwagiza Mkuu wa Mkoa naye kuunda kamati hiyo ya mkoa ili kutatua kero za malalamiko kwa Mahakimu Wakazi na Makimu wa Wilaya.






Kamati hizo za Maadili katika ngazi ya Wilaya wajumbe wake ni Mkuu wa Wilaya ambaye ni mwenyekiti wa Kamati hiyo, Katibu Tawala wa Wilaya ni katibu wa kamati hiyo, Mkuu wa Wilaya pia atateua kiongozi mmoja katika Wilaya husika na Mwananchi mmoja anayeheshimika katika jamii nao watakuwa wajumbe wa kamati hiyo pamoja na Hakimu Mfawidhi wa Wilaya naye ni Mjumbe.




Pili, Waziri Mwakyembe alisema katika ziara yake Mkoani Kagera ni kuhimiza juu ya  uchukuaji  na utunzaji wa takwimu za vizazi na vifo hasa kwa watoto wadogo.  Waziri Mwakymbe alisema kwa nchi nzima ya Tanzania uandikishaji wa takwimu za vizazi na vifo bado ni tatizo kubwa kwani katika Tanzania watoto na watu wazima takwimu zinaonyesha kuwa wenye vyeti vya kuzaliwa nia asilimia 11% tu.





“Tatizo lilionekana kuwa kubwa baada ya Serikali kuamua kutoa elimu bure hapo ndipo ilionekana kuwa mfumo wetu wa takwimu una matatizo makubwa kwani  watoto walifumuka sana kiasi ambacho hapo awali takwimu zilikuwa hazioneshi kuwa wtotot hao wapo katika jamii.” Alisistiza Mhe. Mwakyembe.


Aidha Waziri Mwakyembe aliushukuru uongozi wa Mkoa wa Kagera kwa kuvuka asilimia ya kitaifa kwa uandikishaji wa vizazi na vifo kwani  kwa Mkoa ni asilimia 12% ambapo kitaifa ni asilimia 11% na Wilaya ya Bukoba inaongoza kwa asilimia 45%, Wilaya ya mwisho ni Kyerwa ambayo kwasasa imeandikisha  asilimia 9.4%



Angalizo, Waziri Mwakyembe pamoja na kuushukuru uongozi wa Mkoa na kumuomba  Mkuu wa Mkoa na Wakuu wa Wilaya kuongeza juhudi za uhamasishaji wa wananchi kuona umuhimu wa kuandikisha watoto wao lakini alitoa angalizo kuwa Mkoa lazima kuwa makini sana katika uandikishaji huo ili kudhibiti wahamiaji toka nje ya nchi kuandikishwa .



Tatu, Waziri Mwakyembe alisema amekuja Mkoani Kagera kuona tatizo la mlundikano wa Wafungwa na mahabusu  Magerezani ambapo alisema kuwa amekuwa akitembelea Magereza kila Mkoa alipofanya ziara ili kuona ukubwa wa tatizo ni kiasi gani na kuona jinsi ya kutatua changamoto hiyo Wizara yake ikishirikiana na Wizara ya Mambo ya Ndani.


Waziri Mwakyembe alisema kuwa badala ya kuongea na raia juu ya tatizo la mlundikano wa wafungwa yeye akishirikiana na Waziri wa Mambo ya Ndani waliamua waongee na wafungwa ili kujua tatizo kwa undani na katika kuongea na wafungwa hao katika Magereza mbalimbali nchini waligundua yafuatayo:








Ucheleweshwaji wa nakala za hukumu za kesi,  jamabo ambalo tayari Mahakama  tayari zimeanza kulishughulikia kwa kasi kubwa, pili Kesi za watuhumiwa kukaa muda mrefu bila kusikilizwa, nalo pia mahakama imeanza kulishughulikia, na Tatu Watuhumiwa kubambikiziwa kesi tofauti na kesi zilizowapeleka Magereza. Waziri Mwakembe alisema matatzo yote hayo sasa yanashughulikiwa kwa kasi kubwa sana na Mahakama.


Aidha, katika hatua nyingine Mhe. Mwakyembe alitembelea Ofisi ya Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Bukoba na kumuagiza Kaimu Mtendaji Mkuu kuhaikikisha anaiwezesha ofisi hiyo vifaa vya kisasa kama (Kompyuta) ili kurahisisha utendaji kazi kwani Wilaya hiyo imepiga hatua kubwa katika uandikishaji, vile vile aligawa vyeti vya kuzaliwa kwa wanaume watano na wanawake watano.









Waziri Mwakyembe atakuwepo Mkoani Kagera kwa siku tatu tarehe 14-16/07/2016 na anatarajia kutembelea Mahakama kuu, Gereza la Mkoa  Bukoba, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Gereza la Wilaya ya Muleba na Gereza la Wilaya ya Biharamulo na kuhitimisha  ziara yake Wilayani humo.



About Author

Advertisement

Post a Comment

 

This Template Is Designed By Jacksay | call 0764 031 242 for this service

Top