Karagwe forum Karagwe forum Author
Title: Hotuba Ya Waziri Wa Fedha Na Mipango, Dkt. Philip Mpango , Akiwasilisha Bungeni Mapendekezo Ya Mpango Wa Maendeleo Wa Taifa Kwa Mwaka 2018/19
Author: Karagwe forum
Rating 5 of 5 Des:
UTANGULIZI 1.    Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba, Bunge lako Tukufu likae kama Kamati ya Mipango ili kupokea na kujadili M...
UTANGULIZI
1.    Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba, Bunge lako Tukufu likae kama Kamati ya Mipango ili kupokea na kujadili Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka 2018/19 na Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti kwa Mwaka 2018/19.


2.    Mheshimiwa Spika, awali ya yote, naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uzima na afya. Aidha, tunamshukuru sana kwa kuendelea kulijalia Taifa letu amani na utulivu na kutuwezesha kukutana katika mkutano huu wa tisa wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kujadili namna ya kuharakisha maendeleo ya nchi yetu.

3.    Mheshimiwa Spika, kipekee napenda kumshukuru Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuniamini kuongoza Wizara ya Fedha na Mipango kufuatia mabadiliko aliyoyafanya hivi karibuni katika Baraza lake la Mawaziri na safu ya uongozi wa Mikoa. Aidha, ninawapongeza Waheshimiwa Mawaziri, Naibu Mawaziri na Wakuu wa Mikoa waliobakia katika nafsi zao na wale waliobadilishwa vituo vya kazi. Vile vile, ninawapongeza kwa dhati wote walioteuliwa kuwa Mawaziri, Naibu Mawaziri na Wakuu wa Mikoa wapya.

4.    Mheshimiwa Spika, naomba pia nitumie fursa hii adhimu kutambua na kumpongeza Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa uongozi wake mahiri na makini katika kusimamia rasilimali za Taifa, kupambana na rushwa, kuimarisha nidhamu na uwajibikaji katika utumishi wa umma na zaidi ya yote, kwa moyo wake adili katika kupatia majibu kero za wanyonge. Hakika uongozi wake umezidi kuijengea heshima kubwa nchi yetu.

5.    Mheshimiwa Spika, naomba nitumie fursa hii kumpongeza Mhe. Janeth Masaburi (Mb) aliyeteuliwa na Mheshimiwa Rais kuwa Mbunge katika Bunge lako Tukufu hivi karibuni kutoka Chama Tawala cha CCM. Aidha, nawapongeza kwa pamoja Waheshimiwa Alfredina Apolinary Kahigi, Kiza Hussein Mayeye, Nuru Awadh Bafadhili, Rukia Ahmed Kassim, Shamsia Aziz Mtamba, Sonia Jumaa Magogo, Rehema Juma Migilla na Zainab Mndolwa Amir walioteuliwa na Chama cha Wananchi - CUF kuwa Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ninapenda kuwakaribisha na kuwashauri watumie jukwaa hili kikamilifu katika kuishauri Serikali na kuwatumikia wananchi. Napenda pia kumpongeza Bw. Stephen Kagaigai kwa kuteuliwa na Mheshimiwa Rais kuwa Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

6.    Mheshimiwa Spika, ninawiwa pia kutoa shukrani za dhati kwa Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mheshimiwa Dkt. Ashatu Kachwamba Kijaji (Mb) na watendaji wote wa Wizara ya Fedha na Mipango wakiongozwa na Katibu Mkuu, Bw. Doto Mgosha James kwa ushirikiano walionipa katika maandalizi ya hotuba hii na vitabu vya Mapendekezo ya Mpango na Mwongozo. Aidha, ninawashukuru sana Wizara, Taasisi, Idara za Serikali, Sekta Binafsi na wadau mbalimbali waliotoa maoni na michango yao katika kukamilisha Mapendekezo ya Mpango na Mwongozo.

7.    Mheshimiwa Spika, hoja ninayoiwasilisha hapa imetayarishwa kwa kuzingatia dhana ya ushirikishwaji mpana wa jamii. Kwa ujumla tumepata maoni na ushauri kutoka katika makundi mbalimbali ya jamii na Taasisi za Serikali. Siwezi kuwataja mmoja mmoja wale wote waliochangia hoja hii hadi kufikia hapa. Hata hivyo, kwa namna ya kipekee, napenda kuishukuru na kutambua mchango wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti chini ya Mwenyekiti wake Mheshimiwa Hawa Abdulrahman Ghasia, Mbunge wa Mtwara Vijijini katika kuboresha rasimu za Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti kwa Mwaka 2018/19 na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka 2018/19. Maoni na ushauri mahsusi wa Kamati ulijikita katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na yafuatayo:
(i)    Kujumuisha matumizi ya gesi asilia kwa ajili ya uzalishaji wa umeme na kama malighafi katika viwanda ikiwemo viwanda vya mbolea;
(ii)    Kuzingatia maeneo yanayogusa wananchi walio wengi kwa ajili ya kukuza kipato na kupunguza umaskini hususan kilimo, uvuvi, upatikanaji wa pembejeo na mitaji;
(iii)    Kuweka msukumo mkubwa katika kuboresha mazingira kwa ajili ya ushiriki wa Sekta Binafsi katika kugharamia na kutekeleza miradi ya maendeleo inayolenga kutimiza azma ya Serikali ya kujenga uchumi wa viwanda na maendeleo ya watu;
(iv)    Kuendelea kuboresha mikakati ya kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya Serikali ikiwa ni pamoja na kuibua vyanzo vipya;
(v)    Kuendelea kulipa madeni yaliyohakikiwa na kuzuia uzalishaji wa madeni mapya; na
(vi)    Kufanya tathmini ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2016/17 – 2020/21) kwa kipindi cha miaka miwili ya awali.

8.    Mheshimiwa Spika, hoja ninayowasilisha leo mbele ya Bunge lako Tukufu ni hatua ya awali katika mchakato wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2018/19. Madhumuni ya wasilisho hili ni kuomba maoni na ushauri wa Waheshimiwa Wabunge wakiwa ndiyo wawakilishi wa sauti za wananchi kuhusu masuala yanayostahili kupewa kipaumbele na msisitizo katika Mpango na Bajeti kwa mwaka ujao. Hivyo, napenda kuahidi kuwa maoni na ushauri uliotolewa na Kamati ya Bunge ya Bajeti na yote yatakayotokana na Bunge lako Tukufu linapokaa sasa kama Kamati ya Mipango tutayazingatia kwa dhati wakati wa kuandaa Mpango wa Maendeleo wa Taifa na Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2018/19.

9.    Mheshimiwa Spika, Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Mwaka 2018/19 na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2018/19 yamezingatia Ilani ya Uchaguzi ya Chama Tawala ya mwaka 2015; Sera na mikakati mbalimbali ya maendeleo ya kisekta, kikanda na kimataifa; na Maelekezo mengine ya Serikali. Aidha, vyote vimezingatia hali halisi ya mwenendo wa uchumi katika kipindi cha mwaka 2016  na nusu ya kwanza ya mwaka 2017. Pia, vimezingatia mahitaji ya msingi katika kuimarisha kasi ya utekelezaji wa Mpango na kujenga mazingira yatakayowezesha kufikiwa kwa azma ya Taifa ya kujenga uchumi wa viwanda kama ilivyobainishwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025.

10.    Mheshimiwa Spika, hoja ninayoiwasilisha ina vitabu viwili. Kitabu cha kwanza kinahusu Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti kwa Mwaka 2018/19. Kitabu cha pili kinawasilisha Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka 2018/19. Vitabu vyote viwili vinapaswa kusomwa kwa pamoja.

MWONGOZO WA MAANDALIZI YA MPANGO NA BAJETI YA MWAKA 2018/19

11.    Mheshimiwa Spika, naomba sasa kuwasilisha Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti kwa Mwaka 2018/19. Mwongozo huu unaainisha maelekezo mahsusi yanayopaswa kuzingatiwa na Wizara, Idara Zinazojitegemea, Taasisi na Wakala wa Serikali, Mashirika ya Umma, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa katika kuandaa, kutekeleza, kufuatilia, kutathmini na kutoa taarifa za utekelezaji wa Mpango na Bajeti kwa mwaka 2018/19.

12.    Mheshimiwa Spika, lengo la Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti kwa Mwaka 2018/19 ni kuwaelekeza Maafisa Masuuli kuhusu maeneo ya kipaumbele na masuala mahsusi yanayopaswa kupewa msukumo wa kipekee katika  uandaaji wa mipango na bajeti za mafungu husika. Maelekezo haya yanatokana na Sheria ya Bajeti Na. 11 ya mwaka 2015 na Kanuni zake; maboresho yaliyofanyika katika mifumo ya kibajeti, ukusanyaji wa mapato, usimamizi na udhibiti wa matumizi; usimamizi wa mashirika na taasisi za umma; na usimamizi wa madeni ya Serikali. Mwongozo pia umeainisha mfumo wa bajeti ya mwaka 2018/19, ikiwa ni pamoja na mapendekezo ya awali ya mfumo wa mapato na matumizi ya Serikali kwa mwaka 2018/19 na mfumo wa ufuatiliaji, tathmini na utoaji taarifa za utekelezaji.

Mapitio ya Viashiria vya Uchumi kwa Nusu ya Kwanza ya Mwaka 2017
13.    Mheshimiwa Spika, kabla ya kuwasilisha vipengele muhimu vya Mwongozo, naomba nianze kueleza kwa kifupi mapitio ya viashiria vya uchumi kwa kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka 2017 na utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2016/17.

14.    Mheshimiwa Spika, viashiria vya mwenendo wa uchumi kwa ujumla wake vinaonesha kuwa uchumi wa Taifa ni imara. Katika kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka 2017, Uchumi wa Taifa ulikua kwa asilimia 6.8, ukichangiwa zaidi na kuimarika kwa sekta za mawasiliano, usafirishaji na ujenzi. Ukuaji wa sekta ya kilimo uliongezeka kutoka wastani wa asilimia 2.7 nusu ya kwanza ya mwaka 2016 hadi kufikia asilimia 3.1 nusu ya kwanza ya mwaka 2017 kutokana na hali nzuri ya hewa.

15.    Mheshimiwa Spika, Mfumuko wa Bei bado umeendelea kubakia katika wigo wa tarakimu moja kutokana na kuongezeka kwa ugavi wa chakula katika masoko ya ndani na ya nchi jirani; kutoyumba kwa bei za mafuta ya petroli katika soko la dunia; na utekelezaji wa sera za bajeti za kupunguza matumizi yasiyo na tija. Mfumuko wa bei mwezi Julai ulikuwa asilimia 5.2, Agosti asilimia 5.0 na Septemba asilimia 5.3 ikilinganishwa na lengo la asilimia 5 hadi 8 kwa kipindi husika. Mwenendo wa Thamani ya Shilingi ya Tanzania dhidi ya dola ya Marekani uliendelea kuwa imara katika kipindi chote cha mwaka 2016/17 narobo ya kwanza ya 2017/18. Thamani ya shilingi ya Tanzania imebadilika kutoka shilingi 2,177.26 kwa dola moja ya Marekani mwezi Januari 2016, hadi shilingi 2,221.96 mwezi Januari 2017. Kasi ya shilingi kupungua thamani iliongezeka na kudumu kwa muda mfupi mwezi Januari 2017 hali iliyosababishwa na Benki Kuu ya Marekani kupandisha riba yake na hivyo kuongeza mahitaji ya dola ya Marekani duniani kwa ajili ya kuwekeza. Aidha, baada ya mwezi Januari 2017, thamani ya shilingi iliendelea kuwa tulivu na kufikia shilingi 2,237.78 mwezi Oktoba 2017.

16.    Mheshimiwa Spika, Deni la Taifa liliongezeka kufikia dola za Marekani milioni 26,115.2 mwezi Juni 2017, ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 17.0, ikilinganishwa na dola za Marekani milioni 22,320.76 katika kipindi kama hicho mwaka 2016. Ongezeko hilo lilichangiwa na mikopo mipya iliyochukuliwa ili kugharamia miradi ya maendeleo kama vile: Standard Gauge Railway; Strategic Cities; mradi wa usafirishaji Dar es Salaam (DART) na kupanua upatikanaji wa maji safi Dar es Salaam. Deni hili la Taifa linajumuisha deni la Serikali lililofikia dola za Marekani milioni 22,443.70 na deni la sekta binafsi la dola za Marekani milioni 3,671.50. Pamoja na ongezeko hili, viashiria vyote bado vinaonesha kuwa deni la Taifa ni himilivu kwa kipindi cha muda mfupi, wa kati na mrefu. Uwiano kati ya deni na Pato la Taifa umefikia asilimia 31.2 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 56.
 
Mapitio ya Utekelezaji wa Bajeti 2016/17
17.    Mheshimiwa Spika, Serikali ilitekeleza bajeti kulingana na upatikanaji wa mapato. Mapato yaliyopatikana kutoka vyanzo vyote kwa mwaka 2016/17 yalikuwa Shilingi bilioni 23,634.55, ikilinganishwa na  makadirio ya Shilingi bilioni 29,539.60. Mapato ya ndani yalikuwa Shilingi bilioni 16,639.97, sawa na asilimia 90.2 ya makadirio lakini yakiwa na ongezeko la asilimia 17.7 ikilinganishwa na makusanyo ya mwaka 2015/16. Aidha, misaada na mikopo nafuu kutoka kwa Washirika wa Maendeleo ilifikia Shilingi bilioni 2,474 sawa na asilimia 68.7 ya ahadi. Mikopo ya ndani ilikuwa Shilingi bilioni 4,504.8 sawa na asilimia 83.8 ya lengo la kukopa Shilingi bilioni 5,374.3. Kwa upande wa mikopo ya nje ya kibiashara, Shilingi bilioni 1,226.8 zilipatikana, ikiwa ni asilimia 58.4 ya malengo. Kiasi cha Shilingi bilioni 1,211.0 kati ya mikopo yenye masharti ya kibiashara hakikuweza kutumika kwa mwaka 2016/17 kwa kuwa kilipokelewa mwishoni mwa mwaka. Kiasi hiki cha fedha kitatumika kugharamia miradi ya maendeleo iliyokusudiwa katika mwaka 2017/18.

18.    Mheshimiwa Spika, jumla ya Shilingi bilioni 23,634.55 zilitolewa, ikiwa ni asilimia 80.0 ya makadirio ya mwaka 2016/17. Kiasi hiki kilikuwa ni zaidi ya matumizi halisi ya mwaka 2015/16 ya Shilingi bilioni 22,099.1 kwa asilimia 6.5. Kati ya kiasi hicho, Shilingi bilioni 17,136.2 zilitumika kwa matumizi ya kawaida, sawa na asilimia 96.7 ya lengo na Shilingi bilioni 6,498.3, kwa matumizi ya maendeleo, sawa na asilimia 55.0 ya lengo la mwaka.

19.    Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Serikali napenda kuwapongeza Watanzania walioitikia wito wa Serikali wa kulipa kodi kwa hiari hususan ongezeko la mwitikio wa kutumia mashine za kieletroniki (EFD). Mwaka 2016/17 tulishuhudia pia mwitikio na hamasa ya kipekee kwa wananchi kulipa kodi ya majengo. Haya kwa ujumla wake yanaonesha uelewa wa Watanzania kuhusu wajibu wa kulipa kodi ili kuchangia maendeleo yao. Nawaomba Watanzania waendelee na moyo huo wa kizalendo na kuwahimiza wale ambao hawajapata mwamko kuanza kulipa kodi kwa hiari. Ni kwa njia hii pekee ndipo tutaweza kujenga msingi endelevu wa uchumi na ustawi wa jamii na kulinda heshima ya uhuru wetu.

Mapitio ya Utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo kwa Mwaka 2016/17
20.    Mheshimiwa Spika, mafanikio yaliyofikiwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa mwaka 2016/17 ni pamoja na:- kugharamia ujenzi wa awamu ya kwanza wa reli ya kati kwa kiwango cha Standard Gauge kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro (Shilingi bilioni 1,000.0); ujenzi na ukarabati wa barabara kwa kutumia fedha za mfuko wa barabara (Shilingi bilioni 807.4); mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu (Shilingi bilioni 495.4); elimumsingi bila malipo (Shilingi bilioni 206.9); upanuzi wa miundombinu ya umeme vijijini (Shilingi bilioni 361.5); uboreshaji wa usafiri wa anga kwa ununuzi wa ndege mpya mbili (Shilingi bilioni 103.4) na malipo ya awali ya ndege mpya nne (Shilingi bilioni 320.1); uwekezaji kwenye miundombinu ya umeme (Shilingi bilioni 176.5); ununuzi wa dawa na vifaa tiba (Shilingi bilioni 165); uwekezaji katika miundombinu ya usambazaji maji mijini na vijijini (Shilingi bilioni 137.4); na upatikanaji wa pembejeo za kilimo (Shilingi bilioni 21).

21.    Mheshimiwa Spika, mafanikio mengine yaliyopatikana ni pamoja na: kupata mradi mkubwa wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima-Uganda hadi Chongoleani-Tanga (dola za Marekani bilioni 3.5) ambapo kupitia mradi huu Taifa litanufaika na ajira, utaalamu na fursa za kibiashara. Miradi mingine ni pamoja na:- upanuzi wa bandari ya Dar es Salaam (dola za Marekani milioni 345); ununuzi wa asilimia 35 ya hisa za ZANTEL katika Shirika la Simu Tanzania (TTCL) na hivyo kuiwezesha Serikali kumiliki TTCL kwa asilimia 100 (Shilingi bilioni 14.9); kuimarisha ulinzi na usalama wa raia na rasilimali za Taifa.

22.    Mheshimiwa Spika, hatua za utekelezaji wa baadhi ya miradi inayotekelezwa na Serikali na Sekta Binafsi ni kama ifutavyo:
(i)    Miradi ya sekta binafsi, hususan, ya viwanda imekuwa na mwenendo mzuri, ambapo viwanda mbalimbali vilianza uzalishaji, ikiwa ni pamoja na viwanda vya kuzalisha vifungashio vya Global Packaging (T) Ltd na Madoweka Co. Ltd; viwanda vya kuzalisha bidhaa za ujenzi vya Goodwil Ceramics Ltd na Waja General Co. Ltd; viwanda vya kuzalisha vinywaji baridi vya Saini Food Products Co. Ltd; Sayona Drinks Ltd na kiwanda cha kusindika nyama cha  Mitoboto Farmers Co. Ltd. viwanda vyote nilivyotaja vipo mkoa wa Pwani. Aidha, kuna kiwanda cha kusindika nyama cha Paul Kisivani – Arusha; na viwanda vya kuzalisha mafuta ya kula vya Jielong Mills Ltd kilichopo Shinyanga, Mkongori Oil Mills na Nkupa Oil Mills - vilivyopo Singida, Super Cooking Oil - kilichopo Mwanza na Mount Meru Millers - kilichopo Mara;
(ii)    Miradi mipya 1,160 ya maji katika vijiji 1,206 katika Halmashauri 148; uchimbaji visima 11 mkoani Tabora; upanuzi wa huduma ya maji safi katika manispaa ya Dodoma na Singida;
(iii)    Hospitali ya Taifa Muhimbili: kukamilika kwa ukarabati na upanuzi wa vyumba 7 vya upasuaji na kuongeza idadi ya vyumba kufikia 20 katika jengo kuu la upasuaji; kukamilika kwa ukarabati wa vyumba vinne (4) vya upasuaji katika jengo la watoto pamoja na kuweka mfumo wa hewa medical gas piping; kununuliwa kwa mashine 1 ya kisasa ya CT-Scan, mashine 14 za upasuaji (diathermy machines), mashine 2 kubwa za usafishaji vifaa (auto clave machines), vifaa vya usikivu (cochlear implants), mashine za kutolea huduma ya kupandikiza vifaa vya usikivu (audiometer and ABR machine) na lifti 2 kwa ajili ya majengo ya Kibasila na Sewahaji;
(iv)    Huduma ya Afya ya Uzazi na Mtoto: kukamilika kwa ukarabati mkubwa na ujenzi wa vituo vya afya 8 vilivyopo Kanda ya Ziwa ambapo hadi sasa vituo 171 vinatoa huduma ya upasuaji wa matatizo yatokanayo na uzazi pingamizi pamoja na upatikanaji wa damu salama; na ununuzi wa magari 67 ya kubebea wagonjwa;
(v)    Utunzaji na Uhifadhi wa Vyanzo vya Maji ambapo mipaka ya vyanzo vya maji kumi (10) imewekwa katika mabonde ya Rufiji; Ruvuma na Pwani ya Kusini; Ziwa Rukwa na Wami/Ruvu;
(vi)    Ujenzi wa Bwawa la Kidunda: hatua iliyofikiwa ni kukamilika kwa usanifu wa bwawa na barabara ya Ngerengere – Kidunda (km 76) pamoja na sehemu ya malipo ya fidia kwa wananchi 2,603 waliohamishwa kupisha ujenzi wa bwawa na barabara;
(vii)    Mradi wa Uchimbaji wa Visima Virefu Kimbiji na Mpera ambapo visima 15 kati ya 20 vilivyokuwa vimepangwa vimekamilika; na
(viii)    Mtandao wa Majisafi Jijini Dar es Salaam ambapo shughuli za ujenzi wa matanki saba (7), ulazaji wa mabomba makubwa yenye urefu wa kilometa 69 na madogo ya usambazaji maji kwa urefu wa kilomita 361 umekamilika na kuanza kuunganishiwa maji kwa wateja katika maeneo ya Mbezi, Kiluvya, Tegeta na Bagamoyo.

Utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo katika Robo ya Kwanza ya Mwaka 2017/18

23.    Mheshimiwa Spika, hatua za utekelezaji zilizofikiwa kwa baadhi ya miradi ya maendeleo katika robo ya kwanza ya mwaka 2017/18 ni pamoja na:
(i)    Ujenzi wa bwawa na mitambo ya kuzalisha umeme -Stiegler’s Gorge: zabuni ilitangazwa ili kumpata mkandarasi wa mradi;
(ii)    Ujenzi wa Reli ya Kati: ujenzi wa kipande cha Dar - Morogoro uliendelea, ambapo ujenzi wa kambi za Ilala, Soga na Ngerengere unaendelea; na mkandarasi wa ujenzi wa reli hiyo kwa kipande cha Morogoro – Makutupora amepatikana, ambapo mkataba ulisainiwa Septemba, 2017;
(iii)    Shamba la Miwa na Kiwanda cha Sukari cha Mkulazi: Ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilomita 7 kwa kiwango cha changarawe kutoka barabara kuu ya Dodoma – Morogoro inayoingia katika kiwanda cha kuzalisha sukari cha Mbigiri; kununuliwa kwa matrekta 3; na kukamilika kwa usafishaji wa shamba kubwa (ekari 1000) ambapo ekari 320 zimepandwa miwa. Aidha, ujenzi wa majengo ya kiwanda cha sukari unaendelea;
(iv)    Kuzinduliwa kwa meli mbili (2) za mizigo katika ziwa Nyasa na ujenzi wa kivuko kikubwa kati ya Kigongo na Busisi unaendelea;
(v)    Ujenzi wa barabara zikiwemo flyovers unaendelea na barabara ya KIA – Mererani (km 26) imekamilika na kuzinduliwa;
(vi)    Hifadhi ya Mazingira na Vyanzo vya Maji: kuvitambua, kuviwekea mipaka na kuvitangaza vyanzo vya maji 78 kuwa maeneo tengefu;
(vii)    Huduma ya Maji Vijijini: kukamilika kwa ujenzi wa miradi 90 ya maji vijijini na hivyo kufanya jumla ya miradi iliyokamilika kufikia 1,423; ujenzi wa jumla ya vituo vya maji 117,190;
(viii)    Mradi wa Maji wa Same – Mwanga – Korogwe: kukamilika kwa asilimia 26.3 ya mradi ikiwemo ujenzi wa chanzo; mtambo wa kusafisha maji; na tanki la kuhifadhi maji;
(ix)    Mradi wa Maji kwa Vijiji 100 Vinavyopitiwa na Bomba Kuu kutoka Ziwa Victoria, ambapo miradi ya vijiji 14 na upimaji na usanifu wa miradi ya vijiji 32 umekamilika; na
(x)    Ukarabati na Upanuzi wa Mfumo wa Kusambaza Majisafi Dar es Salaam: ulazaji wa mabomba yenye urefu wa kilomita 77 umekamilika katika maeneo ya Mbezi na Kiluvya.

Uwekezaji wa Sekta Binafsi
24.    Mheshimiwa Spika, ninaomba kutambua mchango wa Sekta Binafsi kwa kuiunga mkono Serikali katika juhudi za kuendeleza viwanda na hivyo kuinua maisha ya watanzania. Katika Mwaka 2016, Kituo cha Taifa cha Uwekezaji kilisajili miradi 345 na kati ya hiyo, miradi 103 ni ya wawekezaji wa ndani, 137 ya wageni na 105 ya Ubia kati ya wawekezaji wa ndani na wageni. Thamani ya miradi iliyosajiliwa mwaka 2016 ilikuwa ni dola za Marekani bilioni 5.92.  Mgawanyiko wa miradi kisekta unaonesha kuwa sekta ya nishati ilisajili miradi yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 2.46 majengo na biashara bilioni 1.13; uzalishaji viwandani bilioni 0.62; kilimo bilioni 0.5; usafirishaji mizigo bilioni 0.38; mawasiliano bilioni 0.28; maliasili bilioni 0.26; na bilioni 0.29 katika sekta zingine. Aidha, sekta ya uzalishaji viwandani iliongoza kwa kuvutia wawekezaji wengi ambapo mwaka 2016 ilisajili miradi 178 ikifuatiwa na majengo ya biashara iliyosajili miradi 48; utalii miradi 33 na kilimo miradi 24.

Changamoto za Utekelezaji wa Mpango na Bajeti na Hatua za kukabiliana Nazo
25.    Mheshimiwa Spika, changamoto zilizojitokeza ni pamoja na: uvujaji wa mapato; mwamko mdogo wa kulipa kodi kwa hiari; udhaifu katika ukusanyaji wa mapato kwa Wizara, Idara Zinazojitegemea, Wakala, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka ya Serikali za Mitaa, Taasisi na Mashirika ya Umma; kutopatikana kwa wakati kwa mikopo yenye masharti nafuu na ya kibiashara kutoka nje; kuongezeka kwa ulimbikizaji wa madai; Wafadhili kupendelea zaidi kufadhili miradi moja kwa moja badala ya utaratibu wa kupitia bajeti ya Serikali unaoiwezesha Serikali kupanga matumizi kulingana na vipaumbele vyake: maandalizi ya miradi mingi kutokuwa kamili kuruhusu hatua za utekelezaji kuanza katika muda uliopangwa; na mwenendo wa kupungua kwa misaada na mikopo nafuu.
 
26.    Mheshimiwa Spika, ili kukabiliana na changamoto hizo, Serikali  inaendelea kuchukua hatua zifuatazo: kuimarisha mifumo na taasisi za ukusanyaji wa mapato; kuimarisha mifumo na taasisi za udhibiti wa mapato na ulinzi wa rasilimali za Taifa; kuendelea kusimamia utekelezaji wa Sheria za Kodi; kuendelea na zoezi la utambuzi na usajili wa walipa kodi kwenye kanzidata ya walipa kodi; kuhuisha mifumo ya kielektroniki ya kumtambua mlipa kodi; kuendelea kuboresha makusanyo ya mapato yasiyo ya kodi hasa yale yanayotokana na michango ya mashirika na wakala za Serikali; kuzitaka Wizara, Idara Zinazojitegemea, Wakala, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka ya Serikali za Mitaa, Taasisi na Mashirika ya Umma kutumia mifumo ya kielektroniki katika kukusanya maduhuli; na kutekeleza makubaliano kati Serikali na Washirika wa Maendeleo juu ya mfumo ulioboreshwa wa ushirikiano utakaoanza kutumika mwaka 2018/19. Hatua nyingine ni pamoja na: kuimarisha benki za maendeleo ili zichangie katika upatikanaji wa rasilimali fedha, hususan mikopo ya kibiashara ya muda mrefu; kuboresha mazingira ya uendeshaji biashara kwa ajili ya kuchochea ushiriki wa Sekta Binafsi; kutoa mafunzo kwa wataalam wa Wizara, Idara Zinazojitegemea na Taasisi za Serikali juu ya uandaaji wa miradi ya maendeleo; kupitia Sheria ya uwekezaji kwa ubia (PPP); na uandaaji wa Mkakati wa Utekelezaji, Ufuatiliaji na Tathmini ya Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano.

SHABAHA NA MALENGO YA UCHUMI JUMLA 2018/19 – 2020/21

27.    Mheshimiwa Spika, shabaha na malengo ya uchumi jumla katika kipindi cha muda wa kati (2018/19 – 2020/21) ni kama ifuatavyo:-
i.    Ukuaji wa Pato Halisi la Taifa kufikia asilimia 7.1 mwaka 2018 ikilinganishwa na matarajio ya asilimia 7.0 mwaka 2017;
ii.    Kudhibiti kasi ya mfumuko wa bei kutoka wastani wa asilimia 5.3 Juni 2017 hadi  asilimia 5.0 ifikapo Juni 2018;
iii.    Mapato ya kodi kuwa asilimia 14.2 ya Pato la Taifa mwaka 2018/19 sawa na ilivyokuwa mwaka 2017/18;
iv.    Matumizi ya Serikali yanatarajiwa kuwa asilimia 24.5 ya Pato la Taifa mwaka 2018/19 ikilinganishwa na asilimia 26.2 mwaka 2017/18;
v.    Kupunguza nakisi ya bajeti (ikijumuisha misaada) kutoka asilimia 3.8 mwaka 2017/18 hadi asilimia 2.5 mwaka 2018/19; na
vi.    Kuwa na akiba ya fedha za kigeni kwa kiwango cha kukidhi mahitaji ya uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje kwa kipindi kisichopungua miezi minne.

MISINGI YA MPANGO NA BAJETI (ASSUMPTIONS)

28.    Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha muda wa kati (2018/19 – 2020/21), misingi ya mpango na bajeti ni pamoja na:
i.    Kuendelea kuimarishwa na kudumishwa kwa amani, usalama, utulivu na umoja nchini  na nchi jirani;
ii.    Kuimarika kwa viashiria vya uchumi jumla na maendeleo ya kiuchumi na kijamii kama vile Pato la Taifa, ukusanyaji wa mapato ya ndani na mfumuko wa bei;
iii.    Kuendelea kuimarika na kutengemaa kwa uchumi wa dunia;
iv.    Kuendela kuwa na utulivu wa bei za mafuta katika soko la dunia; na
v.    Kuwa na hali ya hewa nzuri ndani ya nchi na katika nchi jirani.

MAOTEO YA AWALI YA UKOMO WA BAJETI 2018/19

29.    Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia sera za uchumi jumla pamoja na misingi na sera za bajeti kwa mwaka 2018/19, maoteo ya awali yanaonesha kuwa jumla ya Shilingi bilioni 32,476 zinatarajiwa kukusanywa na kutumika katika kipindi hicho. Maoteo haya yatathibitishwa baada ya kufanya uchambuzi wa mwenendo wa utekelezaji wa bajeti katika kipindi cha nusu  ya kwanza ya mwaka 2017/18. Mapato ya ndani yanatarajiwa kuwa Shilingi bilioni 22,088.2, sawa na asilimia 68 ya mahitaji yote. Kati ya hayo, maoteo ya mapato ya kodi yatakuwa Shilingi bilioni 18,817.0 sawa na asilimia 85.2 ya mapato ya ndani. Vile vile, mapato yasiyo ya kodi yatakuwa Shilingi bilioni 2,423.5 na mapato kutoka vyanzo vya Halmashauri yatakuwa Shilingi bilioni 847.7. Serikali inategemea kukopa kiasi cha dola za Marekani milioni 600 sawa na Shilingi bilioni 1,374.0 kutoka vyanzo vya nje vyenye masharti ya kibiashara na Shilingi bilioni 4,028.6 ni mikopo ya ndani kwa ajili ya kulipia hatifungani na dhamana za Serikali zinazoiva. Aidha, Shilingi bilioni 1,327 sawa na asilimia 1 ya Pato la Taifa, itakuwa ni mikopo mipya ya ndani kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo.

30.    Mheshimiwa Spika, katika maoteo hayo, Washirika wa maendeleo wanatarajiwa kuchangia Shilingi bilioni 3,658.2 ambapo Shilingi bilioni 946.0 ni misaada na mikopo nafuu ya kibajeti, Shilingi bilioni 2,153.3 ni misaada na mikopo kwa ajili ya miradi ya maendeleo na Shilingi bilioni 558.9 ni misaada na mikopo nafuu ya mifuko ya pamoja ya kisekta.

31.    Mheshimiwa Spika, kwa upande wa matumizi, Serikali itatumia jumla ya Shilingi bilioni 32,476.0 ambapo matumizi ya kawaida ni Shilingi bilioni 20,227.6  na maendeleo  ni Shilingi bilioni 12,248.3. Kati ya fedha za  matumizi ya kawaida, Shilingi bilioni 7,627.7 ni kwa ajili ya mishahara ya watumishi wa Serikali na Taasisi za Umma na Shilingi bilioni 9,705.2 kwa ajili ya Deni la Taifa. Aidha, kwa upande wa matumizi ya maendeleo kiasi cha Shilingi bilioni 9,536.2 au asilimia 76.6 ni fedha za ndani.

MAPENDEKEZO YA MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA WA MWAKA 2018/19

32.    Mheshimiwa Spika, Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka 2018/19 ni mwongozo katika uandaaji wa miradi na programu za maendeleo itakayojumuishwa katika Mpango wa Maendeleo wa Taifa mwaka 2018/19 na kitabu cha bajeti ya Maendeleo 2018/19 nitakavyowasilisha mwezi Juni hapa Bungeni. Hivyo, ni matarajio ya Serikali kuwa Waheshimiwa Wabunge watatumia fursa hii kutoa maoni yao yatakayojumuishwa katika Mpango wa Maendeleo wa Taifa mwaka 2018/19.

33.    Mheshimiwa Spika, Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2018/19 utakuwa wa tatu katika mwendelezo wa kutekeleza Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano. Mapendekezo haya yamezingatia malengo ya Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano, 2016/17 – 2020/21, hususan:- (a) Kuendeleza kasi ya ukuaji wa uchumi; (b) Kuimarisha kasi ya utekelezaji wa Mpango, hasa kwa kutanzua changamoto za upatikanaji wa fedha na mitaji, upatikanaji wa ardhi na maeneo ya uwekezaji, na kuimarisha mipango miji na maendeleo ya makazi; (c) Kuongeza uzalishaji wa bidhaa za viwandani; (d) Kuongeza uwezo wa kupambana na umaskini; (e) Kuimarisha ustawi na maendeleo ya jamii kwa kutoa huduma bora za afya, elimu, maji na kinga kwa jamii; (f) Kuongeza matumizi ya teknolojia, ubunifu, ujuzi na utoshelevu wa mahitaji ya rasilimali watu yenye weledi unaohitajika kwa ustawi wa uchumi wa viwanda; na (g) kuhakikisha usalama wa chakula na mahitaji ya lishe bora nchini.

Vipaumbele vya Mpango na Miradi Itakayopewa Msukumo wa Kipekee Mwaka 2018/19

34.    Mheshimiwa Spika, vipaumbele vya Mpango wa Maendeleo kwa mwaka 2018/19 vitazingatia maeneo manne ya kipaumbele ya Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano. Aidha, maeneo hayo yamejumuisha miradi ya kielelezo ambayo utekelezaji wake utapewa msukumo wa kipekee:-
(i)    Viwanda vya kukuza uchumi na ujenzi wa msingi wa uchumi wa viwanda:
Lengo ni kuendelea kujenga viwanda vinavyotumia malighafi zinazopatikana nchini, hususan za kilimo, madini na gesi asilia. Katika eneo hili, miradi itakayopewa msukumo wa kipekee ni pamoja na: Mradi wa Makaa ya Mawe Mchuchuma; Kiwanda cha Kufua Chuma cha Liganga; Shamba la Miwa na Kiwanda cha Sukari Mkulazi; Ujenzi wa mtambo wa kusindika Gesi Kimiminika; uanzishwaji wa Kanda Maalum za Kiuchumi; na  Kituo cha Viwanda Kurasini. Aidha, Serikali itaendelea kupanua na kuimarisha shughuli za Shirika la Viwanda Vidogo – SIDO ili kulifanya kuwa chombo cha kuleta mageuzi ya viwanda nchini.

(ii)    Kufungamanisha Uchumi na Maendeleo Watu:
Eneo hili linalenga kuendeleza mafanikio ya ustawi wa maisha ya watanzania hasa wa vijijini. Msukumo utakuwa katika kuboresha upatikanaji wa huduma za afya hususan huduma za kibingwa, elimu na ujuzi, huduma za ustawi wa jamii; upatikanaji wa uhakika wa chakula na lishe bora; kuendelea kuimarisha upatikanaji wa huduma za maji safi na salama vijijini na mijini; kusimamia rasilimali za maji nchini; na kuimarisha usimamizi wa mazingira na mabadiliko ya tabia ya nchi. Aidha, Serikali itaendelea kuimarisha usimamizi wa utawala bora ikiwa pamoja na kukamilisha azma ya kuhamishia shughuli za Serikali Kuu Dodoma.

(iii)    Ujenzi wa mazingira wezeshi kwa uendeshaji biashara na uwekezaji:
Eneo hili linalenga kuendeleza ujenzi na ukarabati wa miundombinu, ikijumuisha miundombinu ya nishati, usafirishaji (reli, barabara, madaraja na bandari), usafiri wa anga (viwanja vya ndege) na usafiri wa majini (meli na vivuko). Miradi itakayopewa msukumo wa kipekee katika eneo hili ni pamoja na: ujenzi wa bwawa na mitambo ya kufua umeme wa Stiegler’s Gorge; ujenzi wa Reli ya Kati; na kuboresha Shirika la Ndege Tanzania. Vile vile, Serikali inaendelea kuboresha mfumo wa ugawaji na usimamizi wa ardhi; kuboresha mazingira ya kibiashara ili kuvutia uwekezaji na kupanua masoko; na kuendeleza ushirikiano wa kikanda na kimataifa hususan kwa njia ya diplomasia ya kiuchumi.
(iv)    Kuimarisha usimamizi na utekelezaji wa Mpango: hatua zinazopendekezwa zinalenga  kuboresha ufuatiliaji, tathmini na utoaji taarifa za utekelezaji wa Mpango, ikiwa ni pamoja na: kuimarisha mifumo na taasisi za utekelezaji wa Mpango; kuweka mfumo utakaowezesha upatikanaji wa uhakika wa rasilimali fedha kwa maandalizi na utekelezaji wa miradi; na kuweka vigezo vya upimaji wa mafanikio ya utekelezaji.

Miradi ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi
35.    Mheshimiwa Spika, Mpango umebainisha miradi mikubwa ya maendeleo inayotarajiwa kutekelezwa kwa njia ya ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi. Miongoni mwa miradi hiyo ni pamoja na mradi wa mabasi yaendayo haraka Dar es Salaam; kiwanda cha kuzalisha madawa muhimu na vifaa tiba; na mradi wa Dar es Salaam – Chalinze Toll Road. Msukumo utawekwa kuongeza idadi ya miradi itakayotekelezwa kwa mfumo wa PPP.

Mikakati ya Kushirikisha Sekta Binafsi kwa mwaka 2018/19
36.    Mheshimiwa Spika, Sekta Binafsi ndio mtekelezaji mkuu wa Mpango kadri ya dhana ya kujenga uchumi wa viwanda. Serikali imeweka mikakati inayolenga kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi katika utekelezaji wa mpango, ikiwa ni pamoja na kuimarisha mikakati ya kubainisha maeneo yatakayowezesha kuvutia uwekezaji wa sekta binafsi na kuainisha vivutio kwa wawekezaji katika maeneo ya kipaumbele; kuboresha zaidi mfumo rekebu na jukwaa la majadiliano kati ya Serikali na sekta binafsi kuhusu uwekezaji (investors round-table); kufanya mapitio ya sheria ya uwekezaji wa ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi; kuendeleza maboresho ya kimifumo na kitaasisi kuhusiana na ufumbuzi wa mahitaji ya sekta binafsi. Aidha, Serikali itaendelea kuziimarisha benki za ndani za maendeleo ili ziweze kukidhi ongezeko la mahitaji ya mikopo na udhamini kwa sekta binafsi.

MAELEKEZO MAHSUSI KATIKA UANDAAJI WA MIPANGO NA BAJETI KWA MWAKA 2018/19

37.     Mheshimiwa Spika, Maafisa Masuuli wanatakiwa kuzingatia Sheria ya Bajeti Na. 11 ya mwaka 2015 na Kanuni zake ikiwa ni pamoja na kuunda Kamati za Mipango na Bajeti na kuhakikisha Kamati hizo zinatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Kifungu cha 17(3) cha Kanuni za Bajeti za mwaka 2015. Masuala muhimu ambayo Maafisa Masuuli wote wanapaswa kuzingatia wakati wa uandaaji na utekelezaji wa bajeti kama ifuatavyo:

Ukusanyaji wa Mapato ya Ndani
38.    Mheshimiwa Spika, Maafisa masuuli wanaelekezwa: kuhakikisha kuwa makusanyo yote yanawekwa kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali; kuendelea kuboresha mifumo ya ukusanyaji wa mapato; kuhakikisha zabuni za watoa huduma na makandarasi zinatolewa kwa wanaotumia mashine za kielektroniki; kukusanya mapato kutoka vyanzo bunifu vilivyoainishwa katika Mkakati wa Ugharamiaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano pamoja na vyanzo vingine; kutoingia mikataba yenye vifungu vya sheria vinavyohusiana na misamaha ya kodi bila kupata ridhaa ya Waziri wa Fedha na Mipango; na kuhakikisha kuwa kampuni zote ambazo Serikali ina hisa zinaendeshwa kwa ufanisi na hivyo kutoa gawio stahiki kwa Serikali.

Kudhibiti Matumizi na Kupunguza Gharama
39.    Mheshimiwa Spika, ili kuhakikisha Serikali inadhibiti na kupunguza gharama za uendeshaji, Wizara, Idara Zinazojitegema, Wakala, Taasisi za Umma, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa zinaelekezwa: kuendelea kufanya uhakiki wa watumishi ili kuhakikisha kuwa mishahara inalipwa kwa watumishi wanaostahili; kuendelea kupunguza matumizi ya Serikali kwa kutumia Taasisi za Serikali zenye gharama nafuu na huduma bora; kuhakikisha kuwa mikataba yote inayoingiwa na Serikali na Taasisi zake inakuwa katika Shilingi ya Tanzania isipokuwa kwa mikataba inayohusisha biashara za kimataifa; kufanya tathmini ya gharama za uendeshaji wa Taasisi za Serikali ili kuchukua hatua stahiki; na kuhakikisha kuwa Taasisi za Serikali zinazojiendesha kibiashara zinapata faida na kuacha kutegemea ruzuku kutoka Serikali Kuu.

Kulipa na Kuzuia Ongezeko la Madeni ya Serikali
40.    Mheshimiwa Spika, katika kulipa na kudhibiti ongezeko la madeni ya Serikali, Maafisa Masuuli wanaagizwa: kuhakikisha madai yote yamehakikiwa na Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali na kuingizwa kwenye hesabu za Fungu husika (Financial Statement); kutenga fedha za kulipa madeni yaliyohakikiwa; kutekeleza maagizo mbalimbali yaliyotolewa na Serikali kuhusu ununuzi wa bidhaa na huduma; kutoingia mikataba ya miradi mipya bila kuwa na uhakika wa upatikanaji fedha; na kuzingatia matumizi ya Hati ya ununuzi (LPO) zinazotolewa kwenye Mfumo wa Malipo (IFMS) ili kudhibiti ulimbikizaji wa madai.

Maelekezo Mengine
41.    Mheshimiwa Spika, pamoja na maelekezo hayo mahsusi, Maafisa Masuuli pia wanaelekezwa: kutoa taarifa za utekelezaji kwa kuzingatia muundo wa utoaji taarifa uliobainishwa katika Mwongozo; kuhakikisha mipango na bajeti inawekewa viashiria, vigezo na shabaha bayana ambavyo usimamizi wa utekelezaji utavizingatia; na kutekeleza Sera ya Ugatuaji wa Madaraka kwa kuhakikisha kuwa fedha zinatengwa kwenye Halmashauri husika badala ya kutengwa kwenye bajeti za Wizara.

HITIMISHO
42.    Mheshimiwa Spika, Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti kwa Mwaka 2018/19 na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka 2018/19 yaliyowasilishwa mbele ya Bunge lako Tukufu yanalenga  kujenga uelewa wa pamoja juu ya: hali ya uchumi na utekelezaji wa bajeti na miradi ya maendeleo kwa mwaka wa fedha uliopita; maeneo ya kiupaumbele na bajeti yanayopendekezwa kwa mwaka 2018/19 katika kukuza uchumi na kupunguza umaskini; hatua mbalimbali zitakazochukuliwa na Serikali katika kuvutia uwekezaji wa sekta binafsi hususan katika sekta ya viwanda; na kwamba juhudi za makusudi zinahitajika katika kufikia malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025 ya kujenga uchumi wenye hadhi ya kipato cha kati. Msukumo mkubwa wa Serikali utawekwa katika mikakati ya kuongeza mapato, kupunguza gharama na matumizi ya uendeshaji wa Serikali na kudhibiti ulimbikizaji wa madeni.

43.    Mheshimiwa Spika, Wizara, Idara Zinazojitegemea na Wakala, Sekretarieti za Mikoa, Mamlaka za Serikali za Mitaa, Mashirika na Taasisi za Umma zinaelekezwa kuzingatia Mwongozo katika kuandaa mipango na bajeti zao. Vile vile, zinaelekezwa kuzingatia maeneo ya kipaumbele yaliyoainishwa katika Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa  Mwaka 2018/19.

44.    Mheshimiwa Spika, kabla ya kuhitimisha hotuba yangu napenda kutoa shukurani za dhati kwa wadau na wananchi wote kwa juhudi wanazoendelea kufanya katika utekelezaji wa mipango na bajeti. Natoa rai kwa Sekta Binafsi na wananchi wote kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali hususan katika ujenzi wa uchumi wa viwanda kwa kuwekeza na kutekeleza wajibu wa kulipa kodi.

45.    Mheshimiwa Spika, hotuba hii pamoja na vitabu vya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Mwaka 2018/19 na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2018/19 vitapatikana pia katika tovuti za Wizara ya Fedha na Mipango (www.mof.go.tz na www.mipango.go.tz).
 
46.    Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo naomba sasa Bunge lako Tukufu lipokee, lijadili, kutoa maoni na kuishauri Serikali kuhusu Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Mwaka 2018/19 na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2018/19.

47.    Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.

About Author

Advertisement

Post a Comment

 

This Template Is Designed By Jacksay | call 0764 031 242 for this service

Top