TAARIFA KWA UMMA KUHUSU KUIMARISHA UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU YA BARAZA LA TAIFA LA HIFADHI NA USIMAMIZI WA MAZINGIRA-NEMC
Katika
kikao kilichoitishwa na Mhe. January Makamba (Mb), Waziri wa Nchi Ofisi
ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira tarehe 24 January 2016, kuhusu
kuimarisha utendaji ndani ya Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa
Mazingira-NEMC maamuzi yaliyofikiwa ni kama ifuatavyo:
1.
Kuhusu suala la kiwanda cha kusindika minofu ya punda mkoani Dodoma,
imegundulika kulikuwa na ukiukwaji mkubwa, wa makusudi na wa wazi wa
miiko ya kazi kwa watumishi wa NEMC walioshughulika na kiwanda hicho.
Hivyo, Mhe. Makamba ameagiza watumishi wa NEMC wafuatao wasimamishwe kazi mara moja:
a. Dkt. Eladius Makene -Afisa Mazingira Mwandamizi,
b. Wakili Heche Suguta Manchare - Mwanasheria Daraja la II
c. Mhandisi Boniface Benedict Kyaruzi, Afisa Mazingira.Hatua nyingine za kinidhamu na kisheria zitafuatia
2.
Vilevile, imebainika kwamba usimamizi wa watumishi wa NEMC siyo makini
na thabiti na kusababisha malalamiko mengi kuhusu utendaji wa Baraza.
Hivyo, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Mhandisi Bonaventura Baya apewe barua ya onyo kali na la mwisho kwa udhaifu katika usimamizi wa watumishi wa Baraza.
3.
NEMC kama chombo muhimu nchini kilichopewa jukumu la kusimamia
utekelezaji wa Sheria ya Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira inatarajiwa
kazi zake zifanyike kwa ufanisi wa kiwango cha juu kulingana na majukumu
yaliyoko kwenye Sheria.
Hivyo,
kwa mapungufu yanayojitokeza Mhe. Makamba, ndani ya wiki moja ataunda
jopo la wataalamu wasiozidi watano ili kutathmini utendaji wa NEMC na
changamoto mbali mbali katika usimamizi wa hifadhi ya mazingira na
kuishauri Serikali ipasavyo.
4.
Ili kuimarisha ufanisi na udhibiti wa utendaji wa NEMC, ndani ya wiki
moja litatolewa Tangazo litakalokuwa na mambo yafuatayo:
Anwani
ya barua pepe (email), Nukushi (fax), Namba ya simu, Namba ya Whatsapp
ili mtu yeyote mwenye malalamiko au aliyewahi kuombwa rushwa chochote na
watumishi wa NEMC ambacho ni kinyume na maadili ya kazi yao atoe
taarifa mara moja ili uchunguzi ufanyike na hatua zichukuliwe.
5.
Kutokana na mapungufu yanayojitokeza katika utekelezaji wa Tathmini ya
Athari kwa Mazingira, ndani ya wiki moja, NEMC ipitie upya orodha ya
wataalamu na taasisi elekezi zilizosajiliwa na kufuta wataalamu na
taasisi zote ambazo zimekuwa zikikiuka maadili ya kazi zao likiwemo
suala la kuwasilisha taarifa zilizo chini ya viwango, kuchelewesha kazi
za wateja wao na kutowasiliana na wateja wao kuhusu hatua za utekelezaji
wa maombi yao.
6.
Ndani ya wiki tatu uitishwe mkutano wa dharura wa Bodi ya NEMC kujadili
na kufanya maamuzi juu ya changamoto za utendaji katika Baraza.
IMETOLEWA NA
IDARA YA MAZINGIRA,
OFISI YA MAKAMU WA RAIS
TAREHE 24.01.2016
Post a Comment