Mahakama
ya Rufaa wiki ijayo inaanza kusikiliza kesi za rufani 50 za jinai na
madai katika Kanda ya Arusha ikiwamo rufaa ya makamishna wawili wa Jeshi
wa Polisi wanaogombea nyumba ya serikali iliyopo Uzunguni Arusha.
Maofisa
hao, Godfrey Nzowa ambaye ni Mkuu wa Kikosi cha Kupambana na Dawa za
Kulevya katika Jeshi hilo amemshitaki mahakamani aliyekuwa Kamanda wa
Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova akipinga kuuziwa
nyumba hiyo. Kamishna Kova hata hivyo amestaafu rasmi mapema mwaka huu.
Kwa
mujibu wa orodha ya kesi zitakazosikilizwa na majaji watatu wa Mahakama
ya Rufaa kwa mwezi mmoja mjini hapa, Nzowa anamlalamikia Kova na
wenzake kupinga kuuziwa nyumba hiyo aliyokuwa akiishi alipokuwa Mkuu wa
Upelelezi wa Makosa ya Jinai (RCO) wa Mkoa wa Arusha.
Nyumba
hiyo aliuziwa Kamishna Kova akiwa ameshahama mkoani Arusha na wakati
inauzwa Nzowa alikuwa akiishi katika nyumba hiyo, familia yake akiwa RCO
kabla ya kuhamishiwa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kuendelea na
wadhifa huo, Kova akiwa bosi wake.
Orodha
hiyo yenye jumla ya mashauri 50 inaonesha mahakama hiyo itasikiliza
rufani ya Wakili maarufu jijini Arusha, Median Mwale ambaye amekata
rufaa dhidi ya Jamhuri katika kesi yake ya kudaiwa kutakatisha fedha
chafu na kujipatia mabilioni ya fedha kwa njia ya udanganyifu akiwa na
wenzake watatu.
Rufani
hiyo namba 395 ya mwaka 2013 ya Wakili Mwale dhidi ya Jamhuri imepangwa
kusikilizwa na majaji watatu, Mbarouk Salim Mbarouk, Bernard Luanda na
Semistocles Kaijage watakaosikiliza pia mashauri mengine kabla ya kutoa
uamuzi Machi 5, mwaka huu.
Orodha
iliyotolewa na Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufaa, E.Y. Mkwizu
inaonesha kesi nyingine yenye mvuto ni ile ya wafanyabiashara Philemon
Mang’ehe na Gesso Bajuta iliyodumu kwa miaka 20 sasa.
Katika
kesi hiyo, Mang’ehe wa Kampuni ya Bukine anamdai fidia ya mamilioni ya
fedha Bajuta baada ya kudai kuharibiwa biashara yake ya kusambaza vifaa
vya ofisi katika Mahakama ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR) mwaka
1996.
Post a Comment