Serikali
ya Tanzania imesikitishwa na inalaani vikali kitendo cha udhalilishwaji
alichofanyiwa mwanafunzi wa kike wa Kitanzania na Kundi la watu katika
jimbo la Bangalore nchini India.
Kauli
hiyo imetolewa na Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje,
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Ramadhani
Muombwa Mwinyi alipokutana na Wandishi wa Habari kwa ajili ya kuwaeleza
hatua zilizochukuliwa na Serikali kufuatia kitendo hicho cha
kudhalilishwa kwa mwanafunzi wa Kitanzania nchini India.
Balozi
Mwinyi alisema kuwa, hatua zilizochukuliwa ni pamoja na Ubalozi wa
Tanzania nchini India kuiandikia Serikali ya nchi hiyo kuomba maelezo
kamili kuhusu tukio hilo pamoja na kuitaka Serikali ya India
kuwachukulia hatua za kisheria watu wote waliohusika pamoja na
kuimarisha usalama katika maeneo wanayoishi wanafunzi wa Kitanzania.
Aidha,
Balozi Mwinyi alieleza kuwa amemwita Balozi wa India hapa nchini, Mhe.
Sandeep Arya na kumweleza masikitiko ya Serikali ya Tanzania kufuatia
kitendo hicho cha kushambuliwa na kudhalilishwa kwa mwanafunzi wa kike
kutoka Tanzania.
Katika
mazungumzo yao, Balozi Arya alieleza bayana kuwa Serikali ya India
imesikitishwa na tukio hilo la udhalilishaji na kwamba Serikali imeahidi
kuwachukulia hatua za kisheria wale wote watakaobainika kutekeleza uovu
huo.
Alisema
kuwa Waziri Mkuu wa Jimbo la Bangalore aliongea na umma kuelezea
masikitiko yake kuhusu uovu huo na kuahidi kuwa mamlaka za jimbo hilo
zitaimarisha usalama katika maeneo yote wanayoishi wanafunzi wa Tanzania
na raia wengine kutoka nje.
Balozi
Arya aliihakikishia Serikali ya Tanzania kuwa India inaheshimu
ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na nchi yake, hivyo itashughulikia
suala hilo kwa ukamilifu na hadi wakati huu tayari watu watano
wanashikiliwa na vyombo vya usalama wakituhumiwa kuhusika na tukio hilo.
Sanjari
na taarifa hiyo, Balozi Mwinyi aliwaomba Watanzania kutohusisha tukio
hili la uhalifu na ajali ya Mtanzania, Bw. Christian Benjamin Mlyansi
iliyotokea nchini India jana usiku na kusababisha kifo chake.
Alisema
kuwa Bw. Mlyansi alipata ajali ya kawaida alipokuwa anaendesha pikipiki
ambapo ilipoteza mwelekeo na kugonga ukingo wa kati wa barabara.
Post a Comment