Aliyekuwa
mgombea urais kupitia Chama cha Wananchi (CUF) visiwani Zanzibar,
Maalim Seif Sharif Hamad, amewataka Wazanzibari na wapenda amani kuondoa
shaka na kwamba, atatangazwa kuongoza visiwa hivyo.
Maalim
Seif ametoa kauli hiyo kwenye viwanja vya Nngoma Hazingwa, Chake Chake
Pemba akiwa na viongozi wa wilaya, majimbo na jumuiya za chama hicho
ikiwa ni siku moja baada ya kufanya mkutano wa namna hiyo Unguja.
Kiongozi
huyo ambaye ni Katibu Mkuu wa CUF amesema kuwa, ukweli umedhihiri ndani
na nje ya nchi na kwamba hakuna sababu ya kutotangazwa kuwa mshindi wa
uchaguzi uliofanyika tarehe 25 Oktoba mwaka jana.
Amesema,
“Jumuiya na waangalizi wote wa uchaguzi wa kitaifa na kimataifa
wameshuhudia uchaguzi huo na kujiridhisha kuwa ulikuwa huru, haki na wa
uwazi na wanaendelea kushikilia msimamo wao kutaka mshindi wa uchaguzi
huo atangazwe.”
Amesisitiza
kuwa CUF haitoshiriki uchaguzi wa marudio uliopangwa kufanyika tarehe
20 Machi mwaka huu kauli ambayo pia imeungwa mkono na wafuasi wa chama
hicho Pemba kama ilivyokuwa Unguja.
Mapema
Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui amemtaja Maalim
Seif kuwa kiongozi aliyebobea kisiasa na anayejali maslahi ya
Wazanzibari.
Katika hatua nyingine mawakilishi na madiwani wateule wa CUF wamepanga kwenda mahakamani kutetea nafasi zao.
Wameeleza
kwamba, kwa kuwa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) imewapa hati za
ushindi baada ya kufanya uchaguzi mkuu tarehe 25 Oktoba 2015, mpaka sasa
hakuna aliyejitokeza kupinga ushindi wao.
Hata
hivyo, Maalim Seif amesema, viongozi hao waliochaguliwa na wananchi
katika uchaguzi huo na kisha kupewa shahada zao, watakwenda mahakamani
kutetea nafasi zao na kutoruhusu viongozi wengine wa ngazi hizo
kuchaguliwa tena kwa vile wao wanavyo vielelezo vyote vya kuchaguliwa
kwao.
Post a Comment