Wakati
wadau mbalimbali wa masuala ya kisiasa wakipinga kile kinachoendelea
Zanzibar, nao makamishna wawili wa tume ya uchaguzi ya Zanzibar (ZEC),
Nassor Khamis Mohamed na Ayoub Hamad wameibuka na kupinga uchaguzi huo
wa marudio.
Wakizungumza
na wandishi wa habari mjini Dar es salaam leo, makamishna hao wamesema
kuwa sababu kubwa ya kupinga kufanyika kwa uchaguzi huo ni kutokana na
kuvurugwa kwa katiba ya zanzibar tangu tukio la kufutwa kwa matokeo ya
uchaguzi wa oktoba 25, mwaka jana.
Makamishna
hao wa ZEC, wakizungumza kwa hisia na kujiamini, wamesema kuwa
mwenyekiti wa tume hiyo, Jecha Salim Jeche hakuwa na mamlaka ya kisheria
kufuta uchaguzi huo bila kuwashirikisha makamishna wa tume hiyo.
Tayari,
Jecha ametangaza kuwa uchaguzi wa marudio utafanyika siku ya Jumapili,
Machi 20, mwaka huu. Lakini wajumbe hao wa ZEC, kwa pamoja wamesema
wanapinga kufanyika kwa uchaguzi huo kutokana na ukiukwaji wa katiba:
“Tunapinga
marudio ya uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwezi wa Machi.
Uchaguzi huo si halali kulingana na matukio yaliyotokea tangu kufanyika
kwa uchaguzi halali wa Oktoba 25, mwaka jana,” walisema makamishna hao wanaowakilisha CUF ndani ya ZEC.
Wamesema
kuwa sababu nyingine inayowafanya kupinga uchaguzi wa marudio ni
kutokana na kukamilika kwa uchaguzi wa mwaka jana ambapo uchaguzi huo
ulikuwa umekamilika na baadhi ya washindi wa viti vya uwakilishi na
udiwani walishakabidhiwa vyeti vyao.
Wamesema
kurudiwa kwa uchaguzi huo ambao unatarajiwa kutumia zaidi ya shilingi
billion saba hadi kukamilika kwake ni matumizi mabaya ya fedha za
wananchi, kwani uchaguzi Zanzibar ulishafanyika na kinachoendelea ni
mbinu za kuubatilisha.
Wamesema
kuwa tukio la kufutwa kwa uchaguzi huo lilitanguliwa na matukio kadhaa
ambayo yalionyesha wazi kuwa kuna kikundi cha watu ambacho kinamshauri
Jecha, na sio maamuzi ya tume yote nzima.
“Tarehe
26 october mwaka jana CCM walileta barua ya malalamiko na kumtaka
mwenyekiti na tume kufuta uchaguzi huo wakati tayari tulishaanza kutoa
vyeti kwa washindi.
“Baada
ya hapo mwenyekiti aliitisha kikao cha tume na tuliamua kwa pamoja kuwa
maombi ya CCM hayakuwa na mashiko hivyo mchakato uliendelea.” amesema Nassor Khamis mmoja wa makamishna wa tume hiyo.
Amesema
kwamba baada ya maamuzi hayo ya tume, ndipo siku iliyofuata Jecha
(Mwenyekiti wa Tume), hakufika katika ujumuishaji wa matokeo kwa siku
nzima na baadaye walisikia tu kuwa ametangaza kufuta uchaguzi bila
kuwashirikisha wajumbe wengine wa tume.
Nassor amesema: “Baada
ya hapo ndipo ofisi yetu ilianza kuzungukwa na wanajeshi na kuamuriwa
tusifanye lolote huku Jaji wa mahakama kuu ya Zanzibar, naye akiwa
amekamatwa na kupelekwa polisi.”
Wajumbe
hao, wamesema kwa matukio kama hayo wanaamini kuwa tume hiyo imeacha
kufanya kazi zake kisheria na sasa inafanya kazi kisiasa, jambo ambalo
linampotezea sifa mwenyekiti wake kuendelea kuiongoza tume hiyo.
Aidha,
wamesema kuwa hali iliyopo ndani ya tume kwa sasa sio hali ya kawaidia
kuweza kusimamia uchaguzi wa haki kutokana na wajumbe wake kupingana
hovyo hovyo:
“Wajumbe
wamekuwa wakipingana kwa kila hoja inayoletwa…jambo ambalo linafanya
uchaguzi wa marudio kutiliwa mashaka na wajumbe wengi wa tume hiyo,” amesema wajumbe hao.
Makamishna
hao wamesema kuwa wametoa wito kwa wajumbe wengine wa ZEC, kuacha
kufuata mkumbo na kuamua kusimamia sheria inavyosema, ili kuwapatia
wazanzibar haki yao ya kikatiba..
Post a Comment