WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema ataitisha kikao cha viongozi wa dini zote
hivi karibuni ili wapange na kuainisha ni mambo gani ambayo wanaweza
kutoa ushauri kwa Serikali na kupata njia bora ya kuwahudumia
Watanzania.
Alitoa
ahadi hiyo jana mchana (Jumapili, Februari 7, 2016) wakati akizungumza
na mamia ya waumini walioshiriki ibada ya kumsimika Askofu Mkuu wa Pili
wa Kanisa la Evangelistic Assemblies of God Tanzania (EAGT), Askofu Dk.
Brown Abel Mwakipesile iliyofanyika kwenye kanisa la EAGT la Mlimwa West
nje kidogo ya mji wa Dodoma.
Waziri Mkuu Majaliwa ambaye alihudhuria ibada hiyo kwa niaba ya Rais Dk. John Pombe Magufuli alisema: “Hivi
karibuni nitaitisha kikao cha viongozi wa dini zote kitakachojumuisha
Maaskofu Wakuu, Masheikh na baadhi ya wachungaji ili tukae na kubaini ni
nini kifanyike ili kuisadia Serikali namna nzuri ya kuboresha maisha ya
Watanzania.”
Akijibu
risala iliyosomwa na Katibu Mkuu wa kanisa hilo, Dk. Leonard Mwizarubi,
Waziri Mkuu alisema Serikali imeanza kufanya mapitio ambayo
yatawawezesha Watanzania kupata huduma kwa urahisi.
“Katibu
Mkuu pamoja na Baba Askofu Mkuu wamegusia suala la upandaji wa gharama
za vifaa vya ujenzi pamoja na suala la makazi bora. Mwezi ujao tunaanza
vikao vya Bunge vya kupitia bajeti ya Serikali, tutaliangalia hili kwa
kumshirikisha Waziri wa Fedha… tutafanya mapitio katika hili ili
mwananchi wa kawaida aweze kumudu maisha,” alisema huku akishangiliwa na waumini hao.
Aliwaomba
viongozi wa kanisa hilo pamoja na waumini wake waendelee kuiombea nchi
pamoja na viongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano kwani kazi ya kutumbua
majipu waliyoianzisha ina mitihani mikubwa.
“Kutokana
na maombi yenu kwa viongozi wakuu wa kitaifa nina imani Taifa hili
litafika tunakotaka liende. Endeleeni kutuombea kwa sababu kazi ya
kutumbua majipu ina mitihani mikubwa. Lakini pia napenda niwahakikishie
kuwa Serikali hii itatumbua majipu hayo kwa kufuata sheria, kanuni na
taratibu zilizowekwa. Hakuna mtu ambaye ataonewa,” alisisitiza Waziri Mkuu.
Kuhusu
mgogoro wa kiwanja cha kanisa hilo kilichopo eneo la Ipagala, Waziri
Mkuu aliahidi kulishughulikia suala lao Jumatatu( leo ) asubuhi kabla
hajaondoka kurejea Dar es Salaam.
“Kesho
( leo) asubuhi nitamuita Mkurugenzi Mkuu wa CDA na kumtaka anipe
taarifa sahihi kuhusu mgogoro huu. Najua suala hili liko mahakamani,
lakini naamini Mkurugenzi anaweza kuwa kiungo kizuri kati ya wananchi
waliojenga eneo hili pamoja na kanisa ambao mnamiliki kiwanja husika”.
“Kama
atapata eneo jingine na kupima viwanja, kisha akawapatia hawa wananchi
anaweza kuwa amesaidia kuondoa mgogoro huu. Wananchi walienda mahakamani
huku wakijua eneo lenu limewekewa uzio, sasa wanagoma kutoka kwa sababu
hawana mahali pa kwenda,” aliongeza.
Mapema,
akitoa hotuba yake, Askofu Mkuu Dk. Mwakipesile alisema kanisa
litaendelea kuiombea Serikali ya awamu ya tano ili nchi idumu katika
amani na utulivu.
Aligusia
eneo la kanisa lililopo kiwanja na 34, kitalu ‘E’, Ipagala East,
Dodoma, ambalo ujenzi wa shule yake umesimama kutokana na mgogoro baina
yao na wananchi waliovamia eneo lao kwa kujenga nyumba za kuishi licha
ya kuwa eneo hilo lilikwishawekewa uzio.
“Kama
kanisa tumeshindwa kukamilisha ujenzi wa shule kwa sababu wananchi hao
walifungua kesi mahakamani kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa. Tunaomba
uamuzi wa kesi hii uharakishwe,” alisema huku akishangiliwa.
Alisema
kanisa hilo lina majengo 4,670 nchini kote na viwanja 420 ambavyo ni
vya kujenga makanisa na vituo vya kutoa huduma mbalimbali za kijamii.
Kwa
upande wake, Katibu Mkuu wa kanisa hilo, Dk. Mwizarubi alisema katika
risala yake kwamba wanaiomba Serikali ifikirie kushusha bei ya vifaa vya
ujenzi ili wananchi waweze kuwa na nyumba bora za kuishi.
“Maisha
bora maana yake ni kuwa na nyumba bora. Tunaiomba Serikali yako
ipunguze bei ya vifaa vya ujenzi ili Watanzania waweze kuwa na makazi
bora,” alisema huku akishangiliwa.
Post a Comment