Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe, Ummy Mwalimu amepiga marufuku Hospitali na
vituo vyote vya afya vya Serikali kuacha mara moja kugawa au kutoa mafuta (vilainishi) vya kufanya tendo
la ndoa kwa watu wa jinsia moja hasa
wanaume .
Waziri Ummy Mwalimu ametoa msimamo huo wa Serikali akiwa
Mkoani Kagera leo tarehe 15.07.2016 mara
baada ya kuzindua wodi ya wazazi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera
iliyokarabatiwa na kupanuliwa kwa msaada
wa shirika la USAID wakati akiongea na wadau mbalimbali wa afya katika viwanja
vya Hospitali hiyo.
“Nawashukuru sana USAID kwa
msaada wenu ambao mmekuwa mkiutoa kwa Serikali yetu ya Tanzania lakini naomba
kuweka mambo sawa kuwa Serikali haipo tayari kuruhusu ugawaji wa vilainishi vya
kusaidia kufanya mapenzi ya jinsia moja katika vituo vyetu vya kutolea huduma
vya Serikali, nasema wazi kuwa hatutaruhusu
kabisa na nasema wazi hata viongozi wa dini wako hapa wataniunga mkono.”
Alikemea Waziri Ummy.
Aidha, alimwagiza Mkuu wa
Mkoa wa Kagera Mhe. Salim M. Kijuu kuhakikisha wafadhili wote wanaokuja Mkoani
Kagera kutoa misaada akae nao na kusoma makubaliano au mikataba yao vizuri na
kuhakikisha kuwa isiwe na mashariti
ambayo yanalenga kulazimisha masuala kama hayo katika jamii.
Pamoja na agizo hilo Waziri Mwalimu aliwapongeza USAID
kwa kufadhili mradi wa Jhpiego wa
Afya ya Mama na Mtoto (MCSP) ambao umewezesha utolewaji wa mafunzi na kujengewa
uwezo wahudumu wa afya wanaotoa huduma kwa kina mama, watoto wachanga, na
watoto chini ya miaka mitano ikijumuisha wale wanaofanya kazi katika hospitali
hiyo.
Ukarabati na upanuzi
wa wodi ya wazazi ulianza mwezi Oktoba mwaka jana na kukamilika mwezi Machi
mwaka huu, ikiwa ni utekelezaji wa ahadi iliyotolewa na Afisa Mtendaji Mkuu wa
Jhpiego, Dkt. Leslie Mancuso. Upanuzi wa jengo hilo umewezesha ongezeko la
vitanga kwa ajili ya kulaza akina mama wajawazito na wale waliojifungua na
ambao wanahitaji uangalizi.
Upanuzi huo umeongeza
idadi ya vitanda kutoka 28 hadi 66 na pia kuongeza vituo vya wauguzi katika
wodi hiyo ya wazazi pamoja na vyoo. Jumla ya gharama zilizotumika ni jumla ya Tshs. 136,532,166.92 (Milioni mia moja na thelathini na sita, laki tano
na thelathini na mbili elfu, mia moja sitini na sita na senti tisini na mbili).
Waziri
Ummy Mwalimu kabla ya kuzindua wodi ya wazazi aliongea na wadau mbalimbali wa
afya katika Mkoa wa Kagera kwenye Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera
mara baada ya kupokea taarifa ya Mkoa kutoka kwa Mhe. Meja Jenerali Mstaafu
Salum M. Kijuu na kuupongeza Mkoa kwa Juhudi unazozifanya katika kuboresha afya
za wananchi wa Kagera.
Waziri
Ummy alisema, anaupongeza Mkoa wa Kagera kwa kutoa chanjo kwa watoto wadogo na
kuvuka asilimia ya kitaifa ambayo ni 93% lakini Kagera imefikia asilimia 103%.
Pili wanawake wajawazito wanaojifungulia katika vituo vya afya Kagera ni
asilimia 83% wakati kitaifa ni asilimia 52%. Tatu ni Mkoa kupunguza vifo vya
akina mama wajawazito hadi kufikia vifo 70 tu kwa mwaka wakati kitaifa ni vifo
400 pia kupunguza vifo vya watoto chini ya miaka mitano.
Katika
utatuzi wa changamoto ya watumishi wa afya Waziri Ummy Mwalimu alisema kuwa
katika mwaka wa fedha 2016/2017 tayari Serkali imewaruhusu kuajili watumishi
katika kada mbalimbali za afya 10,000 na
kati ya hao amehaidi kutoa kipaumbele kwa Mkoa wa Kagera ili kupunguza tatizo
la watumishi.
Pia
Waziri Ummy ameziagiza Hospitali teule za Wilaya za Mkoa wa Kagera kuwa makini
kutokana na watumishi hewa kwani kati ya watumishi hewa 12,000 waliopatikana
nchini 4,000 wanatoka katika Hospitali Teule za Wilaya.
Aidha Waziri huyo wa
afya alihaidi kuwa kwa watumishi wenye sifa ambao walikuwa katika hospitali
hizo Serikali itaendelea kuwaajili na alitoa mfano katika Mkoa wa Kagera kuwa
kati ya watumishi 81 watumishi 48 wanazo sifa na Seriakli itaendelea kuwaajili.
Katika
kuunga mkono juhudi za mkoa wa Kagera Waziri Ummy alihaidi kutoa vitanda 20 na
magodoro 20 vinavyopelea katika Wodi ya wazazi. Pia alitembelea Hospitali Teule
ya Wilaya ya Muleba Rubya na anatarajia
kukamilisha ziara yake Tarehe 16.07.2016 katika Wilaya ya Bukoba kwa kutembelea
Kituo cha kulelea Wazee Kiilima.
Post a Comment