Paul Chagonja
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amefanya
uteuzi wa Makatibu Tawala wawili wa mikoa ya Mwanza na Katavi ili kujaza
nafasi za Makatibu Tawala wa mikoa hiyo.
Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue amesema Rais amemteua Kamishna wa Polisi, Clodwing Mtweve kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, ambako anakwenda kujaza nafasi iliyoachwa wazi na Faisal Issa ambaye uteuzi wake ulitenguliwa.
Kabla ya Uteuzi huo, Kamishna Mtweve alikuwa Kamishna wa fedha na Utawala wa Jeshi la Polisi Tanzania.
Balozi Sefue amesema Rais Magufuli pia amemteua Kamishna wa polisi Paul Chagonja kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Katavi ambako anakwenda kujaza nafasi iliyoachwa wazi na Madeni Kipande ambaye uteuzi wake ulitenguliwa.
Kabla ya Uteuzi huo, Kamishna Chagonja alikuwa Kamishna wa Mafunzo na Operesheni wa Jeshi la Polisi Tanzania.
Aidha,
Balozi Ombeni Sefue amesema Rais Magufuli ameamua kuwateua Makamishna
hawa wa Polisi kama alivyowateua Majenerali wa Jeshi la Wananchi
Tanzania kuwa Makatibu Wakuu wa Wizara, kwa lengo la kujenga nidhamu
katika utumishi wa umma.
Makamishna
Clodwing Mtweve na Paul Chagonja pamoja na Mheshimiwa Mahadhi Juma
Maalim ambaye ameteuliwa kuwa Balozi Mpya wa Kuwait, wataapishwa kesho
Jumamosi tarehe 30 Januari, 2016 Ikulu Jijini Dar es salaam, saa nne
asubuhi.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam.
29 Januari, 2016
Post a Comment