WAZIRI
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mh. Profesa Makame Mbarawa amemteua
aliyekuwa Mkurugenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius
Nyerere (JNIA), Mhandisi George Sambali kukaimu nafasi ya Mkurugenzi
Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), kufuatia kifo cha
aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Mhandisi Suleiman S.
Suleiman.
Mhandisi
Suleiman alifariki dunia tarehe 18 Januari, 2016 wakati akipelekwa
katika hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam baada ya kuishiwa nguvu
ghafla akiwa katika mazoezi ya kuogelea katika eneo la Feri, jijini Dar
es Salaam.
Akitangaza
uteuzi huo kwa niaba ya Waziri Mbarawa mbele ya Menejimenti ya TAA
Jumatano tarehe 20 Januari, 2016 katika Ofisi za Makao Makuu ya Mamlaka
hiyo kwa niaba ya Mh. Waziri, Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Sekta ya Uchukuzi, Dkt. Leonard Chamuliho, alisema uteuzi
wa Mhandisi Sambali umeanza rasmi tarehe 20 Januari, 2016.
Mhandisi
George Sambali alizaliwa mwaka 1965, mkoani Tabora na ana shahada ya
Uzamili ya Sayansi Uhandisi Uchukuzi na Barabara (MSc. Transportation
(Transport & Road) Engineering, aliyoipata mwaka 1999- 2001 nchini
Uholanzi.
Mhandisi
Sambali alihitimu shahada ya Kwanza ya Sayansi ya Uhandisi Ujenzi
(BSc.Civil Engineering) katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) mwaka
1995 .
Mhandisi
Sambali pia amepata mafunzo na kozi mbalimbali za masuala ya anga
kutoka katika vyuo vya hapa nchini na nje ya nchi, ikiwemo Stashahada ya
Uongozi wa Viwanja vya Ndege (Certificate in Airport Executive
Leadership) mwaka 2014 huko Montreal, Canada.
Pia
mwaka 2015 alitunukiwa Stashahada ya Wataalamu wa Kimataifa wa Viwanja
vya ndege (Post-Graduate Diploma in International Airports Professionals
(AIP) chini ya AMPAP nchini Canada.
Mhandisi
Sambali aliajiriwa na TAA mwaka 2001 kama Meneja Mipango, Usanifu na
Uthamini (Manager Design, Planning and Evaluation) na mwaka 2012
aliteuliwa kuwa Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Uhandisi na Ufundi.
Mwaka
2013, Mhandisi Sambali aliteuliwa kuwa Mshauri Maalum wa Mkurugenzi
Mkuu kabla ya mwishoni mwa mwaka jana kuteuliwa tena kuwa Kaimu
Mkurugenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA).
Mhandisi
Sambali ni mwanachama kwenye vyama mbalimbali vya kitaaluma kikiwemo
cha Wataalamu wa Kimataifa wa Viwanja vya Ndege chini ya Baraza la
Viwanja vya Ndege Duniani (ACI) na Shirika la Kimataifa la Usafiri wa
Anga (ICAO).
Pia
Mhandisi Sambali ni Mjumbe wa Taasisi ya Wahandisi Tanzania (IET);
Mjumbe katika Jukwaa la Kimataifa la Uendeshaji wa Uchukuzi Vijijini
(IFRTD); na Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB).
IMETOLEWA NA;
KITENGO CHA SHERIA NA UHUSIANO –TAA
Januari 25, 2016
Post a Comment