Kamati ya Uongozi ya Bunge imepitisha majina matatu ya wabunge watakaowania nafasi ya uenyekiti wa Bunge.
Majina
hayo yamepitishwa na kamati hiyo iliyoketi jana kuanzia saa 3.00
asubuhi hadi saa 7.00 mchana ikiongozwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai.
Taarifa
za ndani kutoka katika kikao hicho, zilisema kikao kilikuwa na ajenda
mbili ambazo ni uteuzi wa majina ya wenyeviti wa Bunge na kujadili
ratiba ya Bunge.
Chanzo
hicho cha kuaminika kimesema kuwa waliopitishwa ni Mbunge wa Bariadi,
Andrew Chenge, Mbunge wa Viti Maalumu, Dk. Mary Mwanjelwa na Mbunge
mwingine wa Viti Maalumu, Najima Murtaza Giga wote kutoka CCM.
Chanzo
hicho kilisema wabunge hao wanakidhi matakwa ya kanuni inayoelekeza
kuwa mwenyekiti wa Bunge ni lazima awe aidha mwenyekiti wa kamati au
makamu mwenyekiti.
Katika
uteuzi wa kamati uliofanyika mwishoni mwa wiki, Chenge ni Mwenyekiti wa
Kamati ya Bunge ya Sheria Ndogo, wakati Mwanjelwa ni Mwenyekiti wa
Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii na Najima ni Makamu Mwenyekiti wa
Kamati ya Katiba na Sheria.
Kwa
mujibu chanzo hicho, majina hayo ambayo ni kati ya majina sita
yanayotakiwa katika kanuni, yatawasilishwa katika kikao cha kwanza cha
mkutano wa pili wa Bunge utakaoanza kesho.
“Kanuni
zinasema Spika atawasilisha bungeni majina sita yapigiwe kura na
baadaye yapatikane matatu, hawa ndiyo walioomba wamesimama wamejieleza
na kamati imewapitisha.
“Hadi
tunafanya uamuzi huu Ukawa walikuwa hawajaleta majina, sisi hatujui
kama wataleta au hawaleti, lakini majina yaliyopitishwa leo (jana) ndiyo
hayo,” kilisema chanzo hicho.
Bunge
lililopita wenyeviti wa Bunge walikuwa ni Mbunge wa Ilala, Mussa Azan
Zungu, aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalumu, Lediyana Mng’ong’o na aliyekuwa
Mbunge wa Uzini, Muhammed Seif Khatib.
Zungu
amekosa fursa ya kutetea nafasi yake kutokana na kukosa sifa na hivi
sasa yeye ni mjumbe wa kawaida wa Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii
inayoongozwa na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Peter Serukamba. Khatib na
Mng’ong’o hawakufanikiwa kurejea bungeni.
Kamati
ya Uongozi inaundwa na wenyeviti wote wa Kamati za Kudumu za Bunge,
akiwamo Spika wa Bunge, Job Ndugai, Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson na
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Wengine
ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju na Kiongozi wa
Kambi ya Upinzani, Freeman Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai (Chadema).
Majina
hayo yameteuliwa huku kukiwa na sintofahamu katika kambi ya upinzani
bungeni kuhusu uteuzi na mpangilio wa wajumbe katika kamati mbalimbali
za Bunge.
Vyama
vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), havijaridhidhwa na
uteuzi wa kamati hizo, hasa katika Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) na
ile ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) zinazopaswa kuongozwa na
wapinzani.
Kutoridhishwa
huko kumewafanya wabunge wa kambi hiyo kususa shughuli za kamati ikiwa
ni pamoja na kutoshiriki uchaguzi wa wenyeviti wa kamati, jambo
linaloleta taswira isiyoeleweka.
Post a Comment