WATUMISHI sita wa Halmashauri ya Mji wa Kahama mkoa wa Shinyanga, wamekamatwa na Polisi.
Wafanyakazi
hao ni miongoni mwa waliosimamishwa kazi hivi karibuni na wengine
kuwekwa katika uangalizi maalumu kwa tuhuma za kula njama za kujipatia
zaidi ya Sh milioni 800, zilitolewa na Mgodi wa dhahabu wa Buzwagi.
Fedha hizo zilitolewa na mgodi huo kwa lengo la kutekeleza miradi ya maendeleo ya wananchi wa halmashauri hiyo.
Waliokamatwa
ni Katibu wa Bodi ya Zabuni, Joseph Maziku ambaye ni Ofisa Ugavi na
Wajumbe, Kulwa Ntaudyimara (Ofisa Utumishi) na Annastazia Manumbu (Ofisa
Elimu Sekondari).
Wengine
ni Joachim Henjewele ambaye ni Mkuu wa Idara ya Ardhi, Elius Mollel,
Ofisa Biashara na Gervas Lugodisha kutoka Ofisi ya Ugavi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga Mika Nyange, alikiri kukamatwa kwa watumishi hao.
Alieleza
kuwa leo atatoa ufafanuzi juu ya hatua iliyofikiwa kuhusu tuhuma za
watumishi hao, baada ya kuwasiliana na Mkuu wa Polisi wa wilaya ya
Kahama.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Anderson Msumba, alisema watumishi hao
walikamatwa juzi na Polisi baada ya kampuni moja, kati ya kampuni nyingi
zilizohusika katika fedha hizo, kujitokeza katika ofisi za halmashauri
kudai malipo, wakati nyaraka zake zinapishana na za kampuni iliyopewa
kazi na Bodi ya Zabuni.
Nyaraka
za Halmashauri zinaonesha kuwa Bodi ya Zabuni iliipa kazi Kampuni ya
Noble Cliff Construction na kuonesha malipo yatafanyika kupitia akaunti
ya benki ya NMB, huku madai ya kampuni hiyo yalionesha kulipwa fedha
kupitia Benki ya Afrika (BOA).
Baada
ya kuwepo mabishano ya kutofautiana kwa mikataba, Msumba alidai
alimtuma Mweka Hazina wake kwenda kukagua akaunti hizo na kukuta ile ya
BOA, ambayo kampuni hiyo ilidai ilipwe, ilishafungwa siku nyingi na ya
NMB ambayo ilipitishwa na Bodi ya Zabuni, ilikuwa ikimilikiwa na mtu
binafsi.
Msumba
alidai hali hiyo ilionesha kulikuwa na kasoro katika mchakato wa utoaji
wa zabuni. Wajumbe wote wa Bodi ya Zabuni ya Halmashauri ya Mji wa
Kahama, wamekamatwa kutokana na sakata hilo na hadi jana walikuwa
mahabusu katika Kituo Kikuu cha Polisi cha wilaya.
Mkuu
wa Wilaya ya Kahama, Vita Kawawa alitoa tuhuma kuhusu fedha hizo za
Buzwagi katika kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo hivi
karibuni.
Baada
ya hapo, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Abel Shija, aliwasimamisha
kazi watumishi watano kwa tuhuma hizo za kutumia vibaya fedha za Mgodi
wa Buzwagi. Aliagiza waliohamishwa na wanatuhumiwa, warejeshwe kujibu
tuhuma zao.
Post a Comment