Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amemwagiza
Meneja wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), Mkoa wa Dodoma Eng.
Leonard Chimagu kuhakikisha ukarabati wa barabara katika eneo la
Kibaigwa unaanza jumapili.
Profesa
Mbarawa ameyasema hayo alipokuwa akikagua athari za uharibifu wa
barabara zilizosababishwa na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha katika
mikoa ya Iringa – Dodoma na kusababisha mafuriko yanayoharibu kingo za
barabara.
“Hakikisheni
Jumapili kazi ya ujenzi hapa inaanza na ikamilike kwa muda mfupi ili
kutoathiri huduma ya usafiri katika barabara hiyo kutokana na umuhimu
wake”, alisema Prof. Mbarawa.
Waziri
Mbarawa amewataka TANROADS washirikiane na Kikosi cha Usalama
Barabarani kudhibiti magari yanayoegeshwa katika maeneo yasiyo rasmi na
hivyo kusababisha ajali na uharibifu wa barabara hususani katika maeneo
ya Dumila mkoani Morogoro na Kibaigwa mkoani Dodoma.
Mapema
Waziri Mbarawa alikagua ujenzi wa kingo za barabara unaoendelea katika
eneo la Dumila mkoani Morogoro ambapo amemuagiza Meneja wa TANROADS mkoa
wa Morogoro Eng. Dorothy Ntenga kuhakikisha ujenzi huo wa kudhibiti
barabara na daraja la Dumila unakamilika kabla ya Februari 15 ili
kukabiliana na mafuriko wakati wa mvua za masika zinazokaribia kuanza.
“Chimbeni
mchanga kwenye mto ili kuwezesha maji kupita kwa urahisi na kuondoa
tishio la mafuriko yanayo athiri daraja hilo wakati wa mvua za masika”, alisisitiza Waziri Mbarawa.
Naye
Meneja wa TANROADS Mkoa wa Morogoro, Eng. Dorothy Ntenga amesema ili
kudhibiti mafuriko katika eneo la Dumila juhudi zinaendelea kupunguza
mchanga na hivyo kuwezesha kupita maji kwa urahisi.
Profesa
Mbarawa alikuwa katika ziara ya kukagua athari za mafuriko katika
barabara ya Morogoro-Dodoma ambapo maeneo ya Dumila na Kibaigwa
yameathirika zaidi.
Imetolewa na;
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
Mafundi
wakiendelea na ujenzi wa kingo za barabara zilizo athiriwa na mvua
zinazoendelea kunyesha katika mikoa ya Iringa na Dodoma na kusababisha
uharibifu wa barabara katika eneo la Kibaigwa mkoani Dodoma.
Meneja
wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Dodoma Eng. Leornad Chimagu
(kulia),akitoa maelezo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
Profesa Makame Mbarawa kuhusu athari za mafuriko katika kingo za
barabara ya Gairo-Dodoma eneo la Kibaigwa mkoani Dodoma.
Gari likipita sehemu iliyoathirika zaidi katika eneo la Kibaigwa barabara kuu ya Gairo-Dodoma.
Post a Comment