Mabalozi wa nchi zinazounda Umoja wa Ulaya (EU) wameeleza kusikitishwa na kitendo cha Tume ya Uchaguzi (ZEC) kutangaza tarehe ya marudui ya Uchaguzi wakati mazungumzo ya kutatua mgogoro yakiendelea na kumtaka Rais John Magufuli kutumia nafasi yake ya uongozi kutatua mtanziko wa kisiasa visiwani Zanzibar.
Taarifa
ya pamoja iliyotumwa kwa vyombo vya habari na mabalozi hao jana, pia
inamtaka Rais Magufuli kuendeleza wito wake wa kuzitaka pande zote
zitafute suluhu kwa amani.
Tamko
hilo limetolewa siku saba baada ya mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salum Jecha
kutangaza kuwa uchaguzi wa rais wa Zanzibar, wawakilishi na madiwani
utarudiwa Jumapili ya Machi 20, lakini siku tano baadaye CUF ilitoa
tamko la kutoshiriki uchaguzi huo wa marudio.
Kutokana
na sakata hilo, mabalozi hao wamelaani kitendo hicho wakisema kurudia
uchaguzi kwa kigezo kuwa utaratibu ulikiuka, kinawatia wasiwasi kwa kuwa
tume hiyo haikutoa ushahidi wa ukiukwaji huo.
Mabalozi
hao wamesema katika tamko lao kuwa ZEC imerudia kauli yake ya kuwa
uchaguzi ulikiuka taratibu licha ya waangalizi kutoka EU, Jumuiya za
Afrika Mashariki, Sadc Marekani na Jumuiya ya Madola kufanya tathmini na
kujiridhisha kuwa ulikuwa huru na haki.
“Tunasikitika
kuwa ZEC imetangaza tena kuwa uchaguzi utarudiwa Zanzibar, wakati
mazungumzo baina ya pande mbili yanaendelea. Kwa manufaa ya Watanzania
wote, tunasisitiza kuwa hali ya kisiasa ya visiwani humo ni bora
ikatatuliwa kwa pande mbili kukubaliana,” inasema taarifa hiyo.
Taarifa
hiyo iliyotumwa kwa ushirikiano wa mabalozi wa Uholanzi, Norway,
Hispania, Italia, Ujerumani, Finland, Ufaransa, Sweden, Uswisi,
Uingereza, Ireland na Marekani inasisitiza kuwa kitendo cha upande mmoja
kuamua kurudia uchaguzi, kinaweza kuzidisha hofu na taharuki miongoni
mwa Wazanzibari.
“Tunawaomba
Wazanzibari kuwa watulivu na wavumilivu nyakati hizi na tunazitaka
pande zote mbili na washirika wao kuendelea kufanya kazi pamoja ili
wapate suluhisho la amani,” ilisema taarifa hiyo.
Pia inasema ili uchaguzi uwe wa kuaminika, mchakato wake hauna budi kuziwakilisha pande zote na kuwa huru na wa haki.
Post a Comment