Karagwe forum Karagwe forum Author
Title: BALOZI AMINA SALUM ALI AMESEMA MGOGORO WA KISIASA ZANZIBAR HAUWEZI KUISHA.
Author: Karagwe forum
Rating 5 of 5 Des:
K ada aliyegombea urais kwa tiketi ya CCM, Amina Salum Ali amesema mgogoro wa kisiasa Zanzibar hautakwisha hata baada ya Uchaguzi wa m...

Kada aliyegombea urais kwa tiketi ya CCM, Amina Salum Ali amesema mgogoro wa kisiasa Zanzibar hautakwisha hata baada ya Uchaguzi wa marudio kwa kuwa ni wa kihistoria na baadhi ya viongozi hawana nia ya dhati ya kuendeleza Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) visiwani humo.

Balozi Amina pia amesema uamuzi wa CUF kususia uchaguzi wa marudio visiwani humo utasababisha mpasuko mkubwa zaidi na kumtaka katibu mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad kufikiria upya na kubadili msimamo huo kwa faida ya Wazanzibari wote.

Zanzibar imekuwa ikikumbwa na mgogoro wa kisiasa kila inapoingia kwenye Uchaguzi Mkuu kuanzia mwaka 1995 baada ya vyama vya upinzani kuruhusiwa, na vurugu za mwaka 2005 zililazimisha CUF na CCM kuingia kwenye mazungumzo yaliyozaa SUK.

Lakini dalili za SUK kuendelea sasa zinaonekana kufifia baada ya CUF kupinga uamuzi wa mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha wa kufuta matokeo ya uchaguzi wa rais wa, wawakilishi na madiwani visiwani humo Oktoba 28, mwaka jana na kutangaza uchaguzi mpya Machi 20, ambao chama hicho kikuu cha upinzani kimesema hakitashiriki.

Balozi Amina anaona kuyumba kwa Serikali hiyo ya umoja wa kitaifa kunatokana na Maalim Seif kutotambua kuwa maridhiano hutokana na kupata kitu fulani na wakati huohuo kukubali kupoteza kingine.

“Mimi namshauri Seif kujua kuwa katika uchaguzi kuna kushinda na kushindwa, afahamu kuwa Tanzania itajengwa na Watanzania na kwa upande wa Zanzibar, Wazanzibari wanataka maendeleo,” alisema.

“Seif analalamika wakati yuko serikalini, anakutana na mwenzake (Dk Shein) wanakula haluwa na kufurahi pamoja, lakini akitoka nje, anageuka. Tutafika wapi kwa siasa za namna hii?”

Amina alisema Zanzibar ilikuwa na bahati kumpata Dk Shein ambaye Maalim Seif angeweza kumtumia kufanya mambo anayotaka, lakini ameshindwa kugundua fursa hiyo na kuanza kujivuruga.

“Chini ya Dk Shein, Zanzibar imepata fursa nzuri ya kufikia maelewano. Shein anawawakilisha Wazanzibari wote na anajua siasa za Zanzibar ni mstahamilivu, ni mwenye busara, msomi na mpenda maendeleo,” alisema Balozi Amina na kuongeza kuwa:

“Hivyo huu ulikuwa wakati mzuri kwa Seif kushirikiana wafanye anachotaka kwa ajili ya maendeleo ya Wazanzibari.”

Alisema kitendo cha CUF kususia uchaguzi wa marudio kitaongeza mpasuko wa kisiasa badala ya kuupunguza, hivyo ni vyema Seif akaliangalia hilo vizuri na kubadili msimamo huo kwa faida ya Wazanzibari wote.

“Uchaguzi huu wa marudio ndio utakuwa kipimo cha kuonyesha nani anakubalika Zanzibar sasa Seif akisusa maana yake nini?” alihoji.

About Author

Advertisement

Post a Comment

 

This Template Is Designed By Jacksay | call 0764 031 242 for this service

Top