Mkuu wa ofisi na Mwakilishi wa
Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni
(UNESCO) Tanzania, Zulmira Rodrigues amewakumbusha wadau wa urithi wa dunia na
maeneo ya hifadhi kufanyakazi kwa pamoja kwa lengo la kuhifadhi na kuyaendeleza
maeneo hayo bila kuondoa ushiriki wa wananchi wanaozunguka maeneo hayo.
Kauli hiyo ameitoa katika mafunzo
yaliyoandaliwa na Shirika hilo kwa wadau
wa mazingira ya hifadhi na urithi wa dunia mjini Marangu Moshi, yaliyofanyika
katika hoteli ya Kilimanjaro Resort kufuatia makubaliano na serikali ya
Tanzania.
Akizungumza na washiriki amesema
kuwa UNESCO inachofanya ni kuanzisha safari ambayo inaweza kuwa ngumu na ndefu
lakini washiriki wake ni lazima kutambua namna ya kuendelea kufanya menejimenti
ya maeneo ya hifadhi na urithi wa dunia kwa manufaa ya kizazi cha sasa na
kijacho
Akifungua mafunzo hayo ambayo
wataalamu ni washiriki wenyewe wakitumia njia ya kuelewa ya methodolojia ya
uchambuzi wa vikwazo (Bottleneck Analysis Methodology) amesema safari ya
kufanikisha menejimenti ya maeneo hayo duniani na hasa hapa nchini Tanzania ni yenye changamoto nyingi na kwamba
wadau wote wanatakiwa kuwa pamoja kuvishinda vikwazo hivyo na kuifanikisha
safari yao.
Rodrigues akizungumza katika Warsha hiyo ambayo imechukua wadau mbalimbali
wa masuala ya urithi na menejimenti zake kutoka serikalini, taasisi zisizo za
kiserikali na wananchi wengine, amesema kwamba maeneo hayo yamezungukwa na
wananchi na pamoja na kuwawekea sheria za kutoharibu na kuyachakaza ipo haja ya
kushirikiana nao namna ya kupanga kuyaendeleza maeneo hayo huku yakiwa yamebaki
katika hali inayotakiwa.
Mafunzo hayo yamelenga kuwajengea
uwezo wa kupanga maendeleo katika maeneo ambayo ni ya urithi wa dunia, binadamu
na maeneo ambayo uhai unaweza kuwepo.
Aidha akifafanua zaidi amesema
mafunzo hayo yamelenga kuwapa wahusika nadharia zinazofaa katika safari ndefu
ambayo UNESCO nayo itashiriki na isingelipenda kumwacha hata mtu mmoja nyuma.
Mafunzo hayo yanatolewa kufuatia
mpango wa UNESCO wa kutaka kuwa na uhakika na kuhami maeneo hayo ya urithi;
huku mamlaka zikitoa ushirikiano ili kuwezesha malengo ya maendeleo endelevu,
ambayo ndiyo ajenda ya dunia kuelekea 2030, yanafikiwa bila kuathiri maeneo
tajwa
Post a Comment