Wakati
Bunge likieleza kuwa haliwezi kuzuia vituo vya televisheni nchini
kuonyesha moja kwa moja matangazo ya shughuli za vikao vya Bunge,
Serikali imetoa sababu tatu za Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC)
kupunguza matangazo hayo ya shughuli za chombo hicho chenye mamlaka ya
kutunga sheria.
Uamuzi
wa Serikali kuhusu TBC ulizua sintofahamu bungeni na kusababisha polisi
kutumika kuwatoa katika Ukumbi wa Bunge, wabunge wa upinzani waliokuwa
wakishinikiza kusitishwa kwa mjadala wa hotuba ya Rais John Magufuli,
badala yake lijadiliwe suala hilo la shirika hilo.
Naibu
Katibu wa Bunge, John Joel alisema jana kuwa hakuna televisheni yenye
mkataba na Bunge kurusha moja kwa moja matangazo hayo, zote zinazorusha
zinatumia gharama zao wenyewe.
Baada
ya TBC kupunguza matangazo ya moja kwa moja ya shughuli za Bunge,
televisheni zilizobaki ambazo zinarusha moja kwa moja matangazo hayo, ni
Star TV kupitia chaneli yake ya Star Bunge pamoja na Azam TV.
“Sisi
hatuna mkataba nao, wao wanarusha kwa gharama zao na Bunge haliwezi
kuwazuia, labda waulizwe wenyewe kama wataendelea kurusha matangazo hayo
ama laa,” alisema Joel huku akisisitiza kuwa hakuna zuio lolote.
Juzi
jioni Waziri wa Habari, Nape Nnauye alizungumza na waandishi wa habari
mjini Dodoma na kueleza sababu tatu za kupunguzwa kwa matangazo hayo.
Nape aliitaja sababu ya kwanza kuwa ni kupunguza gharama za uendeshaji, “Kwa
mwaka TBC ilikuwa inatumia Sh4.2 bilioni kurusha moja kwa moja
matangazo haya. Fedha hizi hazilipwi na Bunge wala Serikali, zinatokana
na matangazo madogo ya TBC, sasa pia hesabu tangu 2005 mpaka sasa
zimetumika kiasi gasi.”
Alisema
sababu nyingine ya kupunguza kurushwa kwa Bunge ni kutaka wafanyakazi
wa Serikali kufanya kazi kikamilifu, kwa madai kuwa wengi badala ya
kufanya kazi walikuwa wakifuatilia vipindi hivyo.
Alisema
utafiti uliofanywa na Serikali umebaini kuwa waendesha bodaboda,
mamalishe, wamachinga, wakulima, wafugaji na watu wenye shughuli nyingi
wanashindwa kufuatilia vipindi vya Bunge asubuhi na mchana kutokana na
kubanwa na shughuli zao.
Post a Comment