Karagwe forum Karagwe forum Author
Title: TAARIFA YA MKUU WA MKOA KUHUSU HATUA ZINAZOENDELEA KUCHUKULIWA NA SERIKALI KUKABILIANA NA JANGA LA TETEMEKO
Author: Karagwe forum
Rating 5 of 5 Des:
Ndugu Waandishi wa Habari, Kama mnavyojua Mkoa wetu wa Kagera ulipatwa na janga la tetemeko la ardhi tarehe 10.09.2016, k...





Ndugu Waandishi wa Habari, Kama mnavyojua Mkoa wetu wa Kagera ulipatwa na janga la tetemeko la ardhi tarehe 10.09.2016, kutokana na janga hilo Serikali kwa ikishirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo pamoja na wananchi tulichukua hatua za haraka ili kukabiliana na janga hilo, na leo nimewaiteni ili niwape taarifa tulizochukua mpaka sasa ili kunusuru wahanga waliokumbwa na janga hilo katika mkoa wetu.



Ndugu Waandishi wa Habari, Mara baada ya tetemeko hilo kutokea, kwenye mkoa mzima wananchi waliojeruhiwa ni 440 na kati ya majeruhi hao 253 walifika  katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, pia majeruhi 151 walilazwa ambapo majeruhi 113 tayari wametibiwa na kuruhusiwa. Katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wamebaki majeruhi 38 na kati ya hao majeruhi 23 walihitaji huduma za upasuaji na tayari wote wameishafanyiwa upasuaji huo na wanaendelea vizuri.







Aidha, majeruhi 187 walifika katika vituo mbalimbali vya kutolea huduma za afya katika Mkoa wa Kagera na walitibiwa na kuruhusiwa na kufikia jumla ya majeruhi ambao walitibiwa na kuruhusiwa 412 kati ya 440. Vifo vilivyosababishwa na janga hilo ni 17 hadi kufikia siku ya leo.





Ndugu Waandishi wa Habari, Tetemeko la ardhi mkoani Kagera hadi sasa limesababisha nyumba 2,063 kuanguka, Nyumba zenye uharibifu hatarishi 14,081. Nyumba zenye uharibifu mdogo 9,471.  Aidha, wananchi walioathirika na wanahitaji misaada ili kurudi katika mfumo wa kawaida wa maisha yao ni 126,315





Ndugu Waandishi wa Habari, Kufuatia madhara hayo yaliyojitokeza mahitaji mablimbali ya kibinadamu ya muda mfupi na muda mrefu yanahitajika. Mahitaji hayo ni madawa na vifaa tiba, Chakula, Vifaa vya Ujenzi kama simenti, misumari, mabati na mbao.






Hadi kufikia sasa Kamati ya maafa ya Mkoa wa Kagera tayari imepokea msaada wa mahitaji mbalimbali ikiwa ni Madawa na vifaa tiba, Chakula, (Matrubali, mahema mashuka na mablanketi), vifaa vya ujenzi kama mbao, misumari, mabati na simenti vyenye gharama ya zaidi ya shilingi milioni 431,715,800/=



Ndugu Waandishi wa Habari, Kwa upande wa dawa na vifaa tiba wadau mbalimbali pamoja na Serikali wameweza kuchangia dawa na vifaa tiba vya kutosha hadi sasa hakuna upungufu wa dawa na vifaa tiba katika hospitali zetu.




Aidha kwa mahitaji ya haraka tayari Kamati ya mkoa imegawa chakula kwa wahanga katika mkoa mzima kama ifuatavyo: unga wa sembe kilo 3750, mchele kilo 1850, sukari tani 6.5, maharage kilo 3470, bisukuti katoni 2600, na maji ya kunywa katoni 615. Pia wahanga wamegawiwa mahitaji muhimu kama mablanketi 480 mahema 119 na matrubali 320. Huo ulikuwa ugawaji wa mahitaji wa awali na kamati zinaendelea kugawa mahitaji hayo katika maeneo yaliyoathirika na yataendelea kugawiwa kadri tunavyopokea misaada ya mahitaji hayo.








Ndugu Waandishi wa Habari, Napenda sasa kutoa taarifa ya michango mbalimbali ambayo tayari tumeipokea kutoka kwa wadau mbalimbali; Katika Harambee tuliyoifanya jana tarehe 16/09/2016 tuliweza kukusanya kiasi cha fedha taslimu pamoja na hundi 7,800,000/=, ahadi ya fedha na vifaa ni shilingi milioni 770,502,000/= kama wadau hawa wote watatoa michango yao jumla tutakuwa tumepata shilingi milioni 778,302,000/=





Kupitia Akaunti yetu iliyoko  Benki ya CRDB inayojulikana kama “KAMATI YA MAAFA KAGERA CRDB BUKOBA” Akaunti Namba 0152225617300 tayari tumekusanya kiasi cha shilingi 623, 624,200/=. Aidha, baada ya Mhe, Waziri Mkuu kuzindua namba za simu za kuchangia maafa Kagera tayari wananchi wameanza kuchangia michango yao kupitia namba hizo ambazo ni (M.PESA 0768 196 669), (AIRTEL MONEY 0682 950 009), (TIGO PESA 0718 069 616).
















Ndugu Waandishi wa Habari, Napenda kuwashukuru wananchi na wadau mbalimbali wote wanaoendelea kujitoa kwa kuchangia maafa yaliyotupata katika Mkoa wetu wa Kagera pia natoa wito kwa kila Mwananchi, Mdau, Taasisi mbalimbali ambao hawajachangia kuendelea kuchangia kupitia akaunti ya benki na namba za simu zilizotajwa hapo juu kwani mahitaji bado ni makubwa sana.




Ndugu Waandishi wa Habari, Kabla ya kuhitimisha naomba kueleza mkakati wa Kamati yangu tunaondelea nao kuwa ni kugawa mahitaji mbalimbali kwa wahanga kadri tunavyoupokea. Pia wajumbe wote wa Kamati wamegawanywa katika maeneo mbalimbali ya mkoa yaliyopatwa na majanga ili kusimamia zoezi la kugawa mahitaji na kuhakikisha hakuna mwananchi aliyeathirika na janga la tetemeko ameachwa bila kusaidiwa.






Ndugu Waandishi wa Habari, Mwisho napenda kuwashukuru Waandishi wote wa Habari pamoja na vyombo vyao vya habari kwa kufanya kazi yao kwa ushirikiano mkubwa na Kamati yangu kwa kuwafikishia habari wananchi habari muhimu kuhusu janga lililotupata mkoa wetu.


MWISHO


About Author

Advertisement

Post a Comment

 

This Template Is Designed By Jacksay | call 0764 031 242 for this service

Top