Karagwe forum Karagwe forum Author
Title: HISTORIA YA HATUA ZA AWALI ZA KUTAFUTANA KWA WAASISI WA MAGEUZI YA SIASA ZA VYAMA VINGI NCHINI TANZANIA
Author: Karagwe forum
Rating 5 of 5 Des:
Kunako majaliwa ninakusudia kuandika historia ya mageuzi ya siasa za vyama vingi hapa nchini. Inasikitisha, pengine kwa kuwa mwitikio wa...

Kunako majaliwa ninakusudia kuandika historia ya mageuzi ya siasa za vyama vingi hapa nchini. Inasikitisha, pengine kwa kuwa mwitikio wa wasomi kupigania mageuzi ya siasa za vyama vingi ulikuwa mdogo, historia ya vyama vingi hapa nchini haijaandikwa vya kutosha na bila kupotoshwa.


Kwa sasa tunaweza kusoma vipande kadhaa vya taarifa kuhusu harakati za siasa za mageuzi nchini ila si historia kamili na sahihi ikianinsha na kubainisha kumbu kumbu sahihi za muda wa na matukio makuu, sababu za matukio hayo, wahusika wakuu, michakato na minyukano, kupanda na kushuka kwa mashujaa wa kweli na wanyemeleaji wa historia ya mageuzi ya kisiasa nchini kuanzia 1989 hadi 2015.


Kwa kuanzia, nimeanza kwa kuweka kwa usahihi kumbukumbu kadhaa.





1. KONGAMANO LA KITAIFA LA MAGEUZI JUNI 1991
Juni 11-12/1991 kulifanyika Kongamano la kitaifa la mageuzi katika ukumbi wa Diamond Jubilee Dar es salaam. Wahusika wakuu wa kongamano hilo walikuwa [vijana wakati huo] Mabere Marando, Ringo Tenga, Ndimara Tegambwage, Prince Bagenda, Mashaka Nindi Kimoto (apumzike kwa amani)  na Mch. Christopher Mtikila (rip). Wazee [hawa wote ni marehemu kwa sasa na wapumzike kwa amani] walikuwa akina Chief Abdallah Said Fundikira, Kasanga Tumbo na Kasela Bantu.

 Hao walitafutwa mahsusi na kupewa nafasi za kuoneka mbele ili kufuta hisia madai ya demokrasia ya vyama vingi nchini yalikuwa ni matakwa ya vijana. Kwa Zanzibar walialikwa washiriki 11, wafuasi na wawakilishi wa Maalim Seif Sharif Hamad, aliyekuwa kizuizini wakati huo, wakiongozwa Mzee Shaaban Mloo (apumzike kwa amani) na aliambatana na Awesu Dadi na wenzake.




Aidha kulikuwa na Watanzania walikokuwa wanajulikana kwa misimamo yao ya kimageuzi tangu miaka ya 1960 ambao nao walialikwa pia, lakini pia wakimwakilisha Oscar S Kambona. hao ni Mzee Dastan Lifa Chipaka, Mzee Efraem Mwakitwange (apumzike kwa amani) - alikuwa mmiliki wa beach resort hotel ikijulikana kwa jina la Rungwe Oceanic), Mzee Kichoweko, Bwn. James Mapalala na wengineo. Chuo Kikuu walialikwa akina Prof. Mwesiga Baregu na wanafunzi akina James Mbatia, Anthony ABC Komu, Idrissa Al Nuru (amekwisha tangulia mbele ya haki, apumzike kwa amani) na wanafunzi wengineo.

2. MAAZIMIO YA KONGAMANO LA KITAIFA
Mwishoni mwa kongamano kulitolewa maazimio kumi, mojawapo likiwa ni Tanzania kuanzisha mfumo wa vyama vingi vya Siasa. Kisha iliundwa Kamati ya Mabadiliko ya Katiba, kwa Kiingereza, ikijulikana kwa jina la National Comiittee for Constitutional Reform (NCCR) ikiongozwa na Chief Abdallah Said Fundikira, na Katibu wake Mkuu akiwa Mabere Marando.


Kamati hiyo kwa upande wa Zanzibar iliitwa Kamati ya Uhuru wa Kisiasa (KAMAHURU) ikiongozwa na Mzee Shaaban Mloo lakini aliyekuwa defacto leader ni Maalim Seif Sharif Hamad.

Maazimio ya Kongamano hili yaliandikwa na kusambazwa katika kjitabu kilichojulikana kwa title ya TUNACHOTAKA SASA.

Katika Kongamano hilo la kitaifa hakuna kumbukumbu zinazoonesha Mzee Mtei, Freeman Mbowe na waasisi wengine wa Chadema kuhudhuria au pengine kufika tu hapo Diamond Jubilee. Kunako






3. KAMATI YA MAGEUZI NA UJIO WA CHAMA CHA NCCR -MAGEUZI NA VYAMA VINGINE




Februari 15/1992 NCCR [Kamati] ilijibadilisha jina na malengo na kisha kuwa Chama Cha Siasa kwa jina la National Convention for Construction and Reform (NCCR)- Mageuzi. Kwa hiyo NCCR [Kamati] ceased to exist right from 15/02/1992. Lengo lilikuwa ku-maintain jina (NCCR) na historia ya harakati za mabadiliko ya kisiasa nchini (Mageuzi). Wakati huo, kwa sababu mbali mbali, wakongwe akina Mzee Fundikira, Mzee Kasanga Tumbo, na mzee Kasela Bantu walishaamua kuondoka na kuanzisha chama chao cha UMD kikiongozwa na Chief Fundikira, James Mapalala akishirikana na Alec Chempnda (huyu sijui iwapo bado anaishi) walianzisha  Chama Cha Wananchi (CCW), baadaye kiliungana na KAMAHURU na kujiita jina la CUF.

 Mch. Christopher Mtikila akishirikiana na Kaoneka, Mwinnjilist Kamara Kusupa Mwingandoshi (apumzike kwa amani) na mtu mmoja aliitwaKabati walianzisha chama chao kikiitwa Chama Cha Demokrasia (CCD) na kisha baada ya kugombana na Mtikila CCD ilibaki na Mwenyekiti wake Kabati, Mch. Mtikila (mjanja) alibadirisha  CCD kutoka jina la Kiswahili kuwa jina la Kiingereza (Democratic Party /DP).
Kaoneka baadaye aliajiriwa Chadema kwa nafasi ya usimamizi wa ofisi (office supervisor), Kisutu, dar es Salaam, na Mtikila aliendelea na DP (CCD kwa Kimombo) yake, kwanza akiwa mshauri na baadaye Mwenyekiti wa taifa hadi mauti yalipo mfika 2015. 

Mzee Mwakitwange hakuelewana na wafuasi wa Mzee Kambona wakiongozwa na Mzee Dustan Lifa Chipaka na hivyo kuzaliwa vyama viwili, Popular National Party (PONA) kikiongozwa na Mwenykiti wake Mzee Mwakitwange na Katibu Mkuu Peter Terry (sijui kama bado anaishi). Kundi la wafuasi wa Mzee Kambona likiongozwa na Mzee Chipaka lilianzisha chama cha Tanzania Democratic Alliance (TADEA). 


Aidha kabla ya Julai 1992 vilianzishwa vyama vya Liberal Democratic Party (LDP) kilichoongozwa na Mzee Hilal Mapunda, aliyekuwa mhadhiri wa Chuo cha Chama Kivukoni; National Reconstruction Alliance (NRA/NAREA) kilichoongozwa na Mzee Abubakar Olotu na baadaye Profesa Kigoma Ali Malima (muda mfupi sana-apumzike kwa amani); na chama cha National League for Democracy (NLD) kilichoongozwa na Dr. Emmanuel Makaidi (apumzike kwa amani) hadi alipofikwa na mauti mwaka 2015.    








4. UJIO WA CHADEMA NA MZEE EDWIN MTEI 
      
Kunako April 1992, Prince Bagenda akiambatana  na James  Mbatia alitumwa na viongozi wenzake kumfuata Mzee Mtei Nyumbani kwake, Usa River, Arusha. Kabla ya hapo kulikuwa kumefanyika mazungumzo ya simu kati ya Mzee Mtei na Mabere Marando, kumshawishi mzee Mtei ajiunge  NCCR-Mageuzi. Mzee Mtei alishauri apelekewe  Katiba na andiko la Seraza Chama cha NCCR- Mageuzi. Kwa hiyo, safari ya Bagenda ilikuwa kwenda kuongea naye ana kwa ana lakini pia kumpatia nyaraka za chama alizokuwa amesahuri azisome na kuzielewa kabla ya kufanya uamuzi wa kujiunga NCCR-Mageuzi.

Baada ya Mzee Mtei kupokea  nyaraka hizo aliahidi kuja Dar es Salaam kukutana na 'vijana' na kisha kuwapa msimamo wake. [sikumbuki tarehe, ila ni mwezi huo huo wa Aprili /92] Marando, Bagenda na Chimoto walipopata taarifa kuwa Mzee Mtei tayari alikuwa amerejea Dar es salaam walifanya miadi kwenda kumwona na kisha kupata jibu lake, wakiwa na matumani kuwa angejiunga na chama cha NCCR -Mageuzi.


Walipofika nyumbani kwake na kumkuta, Mzee Mtei aliwakaribisha na kisha kuwaambia maneno haya, "kuna watu wenye means and substance wamekuwa wakinishawishi kuanzisha chama.

 Nimeamua kuanzisha chama kwa hiyo ninyi vijana mwende mvuje chama chenu kisha mje kujiunga kwenye chama change nitakachoanzisha". Kwa kauli hiyo vijana hao walipoa, ila Marando alimjibu na hapa ninamnukuu, "Mzee Mtei tumetumia muda, akili, nguvu, pesa na kunyeshewa na mvua nyingi wakati wa kuanzisha chama cha NCCR -Mageuzi, tunakushauri uendelee na juhudi zako ila tunaamini huko tuendako mvua itakunyeshea pia, na ikiwa hivyo, kisha ukitafuta mahali pa kujikinga tutakukaribisha kujikinga pamoja".

Kesho yake tulipata taarifa kuwa saa 5 mchana juu ya alama Mzee Mtei  alikuwa aongee na waandishi wa habari pale Motel Agip. 

Mwandishi aliyekuwa ametumwa na NCCR-Mageuzi alirejesha feedback kuwa Mzee Mtei akiwa na marafiki zake wa enzi zake - Bob Makani, Edward Barongo na wengineo, alikuwa ametangaza kuanzisha chama mara baada ya kuwepo kwa sheria ya kuruhusu Tanzania kuwa nchi ya vyama vingi vya Siasa. Kwamba chama hicho kingeitwa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA); na kwamba kwenye mkutano huo waasisi wote waliokuwepo walikuwa wamevaa sare - walifunga tai, makoti yakiwa yamening’inizwa ukutani na suruali zao zikining'nia kwenye suspenders.


Taarifa hiyo haikushangaza viongozi na wanachama wa NCCR Mageuzi ila nyaraka walizopewa waandishi wa habari zilikuwa ni zile zile (copy right) Prince Bagenda alizompelekea Mzee Edwin Mtei Nyumbani kwake Usa River - Katiba na Sera za NCCR Mageuzi isipokuwa kubadilishwa (replace with) maneno 'NCCR-Mageuzi' kwa  'CHADEMA' basi. Ukiangalia nembo ya NCCR -Mageuzi utaona kuwa hata maneno Demokrasia na Maendeleo yalitolewa humo. Maneno ya Mzee Mtei na wenzake kwa jina CHADEMA ni [CHA] tu, DEMA ilichomolewa kwenye nembo ya NCCR-Mageuzi.

Hii ni historia kwa kifupi sana ya kutafutana na kukutana kwa waasisi wa mageuzi wakati wa harakati za awali za kuasisiwa [tena] kwa mfumo wa siasa za vyama vingi hapa nchini Tanzania.


Imeandikwa na Bubelwa Kaiza

About Author

Advertisement

Post a Comment

 

This Template Is Designed By Jacksay | call 0764 031 242 for this service

Top